Home Ligi EPL Guardiola vs Mourinho: Vijembe walivyowahi kurushiana huko nyuma

Guardiola vs Mourinho: Vijembe walivyowahi kurushiana huko nyuma

586
0
SHARE

pep-vs-jose

Ule wakati tuliokuwa tukiusubiria kwa hamu, sasa umefika. Sahau kuhusu Batman vs Superman – hili ndio pambano kali zaidi la mwaka: Pep Guardiola dhidi ya Mourinho. Manchester City dhidi ya Manchester United. Pambano hili la Jumamosi laweza kuwa moja ya mapambano yaliyopewa ‘kiki’ zaidi katika Ligi Kuu ya England kabla ya kuchezwa.

Guardiola na Mourinho walikuwa marafiki wa karibu wakati wote walipokuwa Camp Nou, lakini walipokuja kuwa wapinzani hasa katika mechi za Real Madrid na Barcelona, urafiki wao wa zamani haukuonekana tena kuwepo wala kufanania kama urafiki mkubwa uliwahi kuwepo kati yao.

Ukiongeza na ule ushangiliaji wa Mourinho wakati alipopata ushindi dhidi ya Barcelona, 2010, katika mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya UEFA basi hapo ndipo utakapokumbuka kumbe ‘balaa la ushindani’ halianzi Jumamosi hii bali lipo tangu zamani.

shaffihdauda.co.tz imekusanya vijembe vikali zaidi ambavyo makocha hawa wamewahi kurushiana huko nyuma kabla ya vipya ambavyo tunategemea kuvipata Jumamosi hii.

Vijembe vya Mourinho dhidi ya Guardiola

Uchambuzi wa Mourinho kuhusu mechi ya fainali kati ya Chelsea na Barcelona, Stamford Bridge (Hii ilikuwa mwaka mmoja baadae na Mourinho alikuwa ameshafukuzwa kazi Chelsea)

‘Mwaka mmoja uliopita Chelsea walikuwa wanalia na Barca walikuwa wanacheka na refa. Walicheka kwa sababu refa aliwanyima vijana wangu wa Chelsea haki yao sahihi’

Baada ya Guardiola kulalamika kuhusu goli la Pedro kukataliwa baada ya kuonekana alikuwa offside katika mechi ya Copa de Rey…

‘Mpaka sasa kuna kundi dogo sana la makocha ambao hawaongelei kuhusu marefa na kundi kubwa ambalo huongelea. Sasa, baada ya maneno ya Pep, tumeanza kuwa na kundi la tatu, hili lina mtu mmoja tu, mtu ambaye anamkosoa refa pale anapofanya maamuzi sahihi. Hiki ni kitu kipya kabisa kwangu.’

Baada ya Barca kuipiga Real 2-0 kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa…

‘Siku moja nitapenda Josep Guardiola ashinde kombe hili kwa haki. Nikiwaambia UEFA kitu ninachohisi na kuwaza, kibarua changu kitaota nyasi sasa hivi. Badala yake nitauliza swali ambalo nina matumaini siku moja nitapata majibu: Kwa nini? Kwa nini Ovrebo? Kwa nini Busacca? Kwa nini De Bleeckere? Kwa nini Stark? Kwa nini? Kwa sababu kila nusu fainali vitu vilevile vinatokea. Tunaongelea kuhusu timu nzuri sana ya mpira, lakini kwa nini wanahitaji vitu vile? Kwa nini?

‘Kwa nini timu nzuri kama walivyo wanahitaji kitu kingine cha ziada ambacho kipo wazi kila mtu anaona? Sijui kama ni kwa sababu ya udhamini wa UNICEF au kwa sababu wao ni watu wema sana. Sielewi. Wao wana nguvu, sisi hatuna nafasi. Kitu nachoweza kufanya ni kuacha swali hili hapa hewani na kutumaini siku moja nitapata jibu. Inabidi waingie fainali, na wataingia. Josep Guardiola ni kocha mzuri sana, Lakini mimi nina makombe mawili ya Ligi ya Mabingwa na yeye ameshinda moja tu – na hilo ni moja linaloweza kuniaibisha.

‘Nitajiskia aibu kushinda kombe huku nikiwa na skendo ya Stamford Bridge (Scandal of Stamford Bridge – ni ile mechi kati ya Barca na Chelsea iliyopigwa Stamford Bridge na kuisha 1-1) Kama akishinda kombe mwaka huu basi itakuwa ni skendo ya Bernabeu.  Ndani kabisa, wao ni watu wema, hawataonja ladha ile tamu ya ushindi. Natumaini siku moja Guardiola atakuwa na nafasi ya kushinda kombe (la Ligi ya Mabingwa) bila skendo yoyote.’

Mourinho juu ya aina ya uchezaji wa Barcelona baada ya kushinda Super Cup ya Spain, 2011…

‘Sitasema kwamba tunafuraha kwa sababu hatukushinda Super Cup, huo utakuwa ni unafiki. Lakini tulipanga kucheza kama wanaume na sio kuanguka chini kwa kuguswa kidogo tu. Nimefundishwa kucheza kama mwanaume na sio kuanguka wa kwanza.’

Mawazo yake katika mapumziko ya sabato ya Guardiola kwa mwaka mmoja…

‘Ni maisha yake, lakini kwa mimi haingii kichwani kuchukua mapumziko ya sabato. Yeye ni mdogo kwangu, lakini mimi bado sijachoka.’

Baada ya mechi ya Chelsea na Bayern Munich kwenye Super Cup ya UEFA…

‘Timu bora ilipoteza. Walifunga penati moja tu zaidi yetu.’

Juu ya viwango vya maamuzi ya marefa…

‘Kila siku nikicheza na Pep, ninamaliza na wachezaji kumi. Itakuwa ni kama sheria flani ya UEFA’

Maoni ya Mourinho juu ya kufanana kwao…

‘Wapo watu, wana akili kuliko mimi, wanaoweza kuuza picha zao, tofauti kabisa na ya kwangu, lakini ndani kabisa, wako kama mimi’

Akiongelea kuhusu picha yao wakiwa pamoja Barcelona enzi hizo…

‘Ndiyo, bado  nina picha. Tulikuwa karibu.’

Kwa nini upinzani wao ndani ya Ligi Kuu ya England hautakuwa na shinikizo kubwa…

‘Uzoefu wangu hauniruhusu kuwa mjinga. Nilikuwa Spain kwa mika mitatu, ambapo bingwa alikuwa mimi au yeye. Kule, upinzani baina ya watu, unaleta maana kwa sababu unaweza kuathiri matokeo ya mshindi wa kombe.

‘Kama nikiamua kumfuatilia yeye na Manchester City na kama yeye akiamua kunifuatilia mimi na Manchester United, mtu mwingine atakuwa bingwa. Kiwango cha Ligi Kuu ya England kinaenda kupanda kutokana na wachezaji na makocha watakaokuja.

‘Mabingwa wanne katika miaka minne, inaonesha ni kiasi gani kuna ushindani, na pia inaonesha ni jinsi gani haki za matangazo ya televisheni na usambazaji, ambavyo vitachochea ukuaji wa ligi na timu zake zote. Ni tofauti na ligi zingine ambazo Papa siku zote atakuwa ni Papa tu.

Vijembe vya Guardiola kwa Mourinho

Kwa nini Guardiola huwa anakaa kimya…

“Namjua Mourinho na anajaribu kunichokoza ili nikasirike, ila hataweza. Siwezi kukasirika. Siendi kumjibu, ila pale tu ambapo nitaona ni muda sahihi.’

Kabla ya mechi yao ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa 2011…

‘Kwa kuwa Mourinho ameniita Pep, na mimi naenda kumuita yeye, Jose. Kesho saa 3:45 tutakutana uwanjani. Nje ya uwanja, ameshashinda. Amekuwa akishinda nje ya uwanja kila msimu. Inabidi wampe kombe la Ligi ya Mabingwa ili alifurahie, aende nalo nyumbani.

‘Kwenye chumba cha mikutano, yeye ndio boss na mtu anayejua kuliko mtu mwingine yeyote.  Nitamkumbusha kwamba tulikuwa pamoja, mimi na yeye, kwa miaka minne. Ananijua na mimi namjua. Hiyo inatosha kwangu.

‘Kama anapenda kuyapa thamani maneno ya waandishi ambao wanatoa habari zao moja kwa moja kutoka kwa Florentino Perez kuliko uhusiano tuliokuwa nao kwa miaka minne, basi hilo ni chaguo lake. Najaribu kujifunza kutoka kwa Jose uwanjani, lakini najaribu kujifunza kidogo kadri niwezavyo kutoka kwake awapo nje ya uwanja.

Juu ya muda wao chini ya Bobby Robson…

‘Tulikuwa tukibadilishana mawazo. Ulikuwa ni urafiki, uhusiano uliokuwa hai.’

Akizungumza kuhusu hali ya urafiki wao…

‘Nikiwa na Mourinho, mambo mengi yalitokea. Mambo mengi kweli.’

Pale alipoambiwa kwamba wanafanana…

‘Kama hilo ni kweli, itabidi niangalie tabia yangu upya.’

Baada ya Guardiola kuchaguliwa kuwa kocha wa City…

‘Nadhani Jose amesema vizuri tu. Sio kuhusu yeye au mimi. Chochote kile mlichokiona kabla sio mada sasa hivi, tumeshindana mara nyingi na namjua vizuri.’

Kuhusu msimu huu wa Ligi Kuu…

‘Sioni hilo kama swali. Anataka kushinda, na mimi nataka kushinda, tunajuana vizuri toka zamani wakati tupo Barcelona.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here