Home Kitaifa SIMBA WANA HOJA KWENYE SAKATA LA KESSY

SIMBA WANA HOJA KWENYE SAKATA LA KESSY

1005
0
SHARE

IMG_0363

Hivi karibuni kumeibuka sakata kati ya klabu ya Simba dhidi ya beki wao wa zamani Hassan Kessy, Simba wakidai kwamba mchezaji huyo hakufata taratibu na alivunja mkataba wakati akijunga na Yanga, Simba wanahoja ya msingi katika hili.

Kiukweli mchezaji alikosea kwa kitendo chake cha kuvaa jezi ya Yanga na kujihusisha na klabu hiyo wakati akijua wazi kuwa mkataba aliokuwanao na klabu ya Simba ulikuwa haujamalizika.

Taratibu za uhamisho wa mchezaji anayemaliza mkataba

Kwa mujibu wa taratibu za kawaida za mchezaji kuhama kutoka klabu moja kwenda klabu nyingine, sababu ya msingi ambayo inaruhusu mchezaji kuondoka ni pale anapokuwa amemaliza mkataba na timu aliyokuwa anaitumikia kabla ya kujiunga na klabu nyingine.

Kuna kipengele kinachomruhusu mchezaji kufanya mazungumzo na klabu nyingine akiwa amebakiza miezi sita kwenye mkataba wake na timu anayoitumikia kwa wakati huo ili pale mkataba utakapomalizika aweze kujiunga na klabu inayomhitaji.

Hiyo haimaanishi katika kipindi ambacho anatumikia miezi sita ya mwisho wa mkataba wake na klabu anayoitumikia kwa wakati huo, basi aanze kujihusisha na shughuli za klabu mpya anayotarajia kujiunga nayo kwasababu tu wameshafikia makubaliano.

Kessy ajihusisha na masuala ya Yanga kabla ya kumaliza mkataba Simba

Kinachotakiwa kufanyika, ni wao kukubaliana na kusaini mikataba lakini hairuhusiwi mchezaji kuanza kujihusisha na klabu mpya hadi pale mkaba wake na timu anayoitumikia (kwa wakati huo) kumalizika. Kwahiyo kitendo cha Kessy kuonekana akijihusisha na klabu nyingine akiwa bado kwenye mkataba na klabu ya Simba, ni kosa.

Sasa ili pande mbili zisitunishiane misuli, inabidi mchezaji aiombe radhi klabu ya Simba kwa kufanya kitendo ambacho naamini kabisa yeye alikuwa hakijui, lakini kitu ambacho kinaweza kumgharimu ni tamaduni za vilabu hivi vikongwe kwenye soka la Bongo, Simba na Yanga.

Ni kweli Yanga hawakujua Kessy anaigia chaka?

Siamini kama viongozi wa klabu ya Yanga kama walikuwa hawalitambui hili, lakini kwasababu ya kutaka kuoneshana umwamba kama si ubabe walimwigiza ‘kingi’ Kessy kwa kumrubuni na kumdanya Kessy na hatimaye kuingia kwenye huu mvutano.

Upande wa Yanga hususan kocha wao Hans van Pluijm, huyu ni kocha wa kimataifa ambaye anajua taratibu za uhamisho wa mchezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine. Kitendo cha kukubali kumchukua Kessy kwenye kikosi chake na kusafiri naye kwenda Uturuki huku akifahamu mchezaji huyo bado hajamaliza mkataba na klabu yake, pia hakwepi lawama katika hili.

Darasa kwa wachezaji wa Bongo

Mwisho wa siku wachezaji wa kitanzania inabidi wawe na wasimamizi sahihi, lakini Kessy tunafahamu anamtu anayemsimamia ambaye ni Othman Tippo, sasa sijui alikuwa wapi wakati yote haya yanatokea na kushindwa kumshauri mchezaji wake kuto jihusisha na jambo hili.

Mara baada ya Kessy kukubaliana na Yanga, alitakiwa kutulia wakati huo akiwa anatumikia adhabu ya kusimamishwa na Simba kwa mechi tano huku akisubiri mkataba wake umalizike na hatimaye kujiunga na klabu mpya aliyokubaliana nayo ambayo ni Yanga. Kitendo cha kujihusisha na klabu ya Yanga hili ni kosa lilifanyika.

Kessy usishupaze shingo, waangukie Simba

Kessy tayari amefanya makosa, Simba wasifanye maamuzi ya kumkomoa jambo la busara kufanyika hapa ni Simba kumsamehe mtoto wao kwasababu wao ni kama baba kwa Kessy. Kikubwa ni kuendelea kumsaidia na kumfundisha kijana wao huku Kessy akiendelea kuwa mpole na kutii kwasababu alishakosea.

Pogba, Luiz, ni mfano

Katika dirisha la usajili barani Ulaya lililofungwa usiku wa August 31, tumeona wachezaji kadhaa wamerejea kwenye vilabu vyao vya zamani. Paul Pogba, David Luiz na wengine wengi ni mfano wa wachezaji ambao wamerejea kwenye vilabu vyao vya zamani tena kwa thamani kubwa ya pesa.

Jambo la kujifunza hapo ni kwamba, kama wachezaji hao wangeondoka na kuacha migogoro kwenye vilabu vyao vya zamani je, leo hii wangeweza kurejea? Lakini kwakuwa mambo yalifanyika kitaalam na kwa kufuata ueledi, wanarejea kwenye vilabu walivyowahi kuvitumikia wakiwa wanafurahiwa na kushangiliwa na kila mtu.

Kwahiyo Kessy kuondoka Simba isiwe sehemu ya malumbano kuonekana yeye ameonewa, yeye anatakiwa atulie kwasababu hakuna anayejua nini kitatokea siku zijazo.

Ushauri wangu

Kessy amekosea lakini Simba wanatakiwa wamuangalie kama mchezaji mwingine wa kitanzania ili waweze kumsaidia iwe mfano na fundisho kwa wachezaji wengine. Kikubwa Simba wanatakiwa walinde kipaji cha mchezaji huyu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here