Home Kimataifa KAMA USAJILI WA EURO MIL 90 WA HIGUAIN JUVE NI KWA AJILI...

KAMA USAJILI WA EURO MIL 90 WA HIGUAIN JUVE NI KWA AJILI YA UEFA, BASI WAMETUPA PESA ZAO

800
0
SHARE

Gonzalo

Na Mahmoud Rajab

Pesa, pesa, pesa. Pesa ni kitu cha ajabu sana hapa ulimwenguni. Inaweza kufanya chochote kile kwa mantiki ya kutimizwa matakwa fulani. Katika soka ndiyo usiseme, imekuwa ni kama makaratasi tu, zinatolewa ovyo kwa nia ya kupata saini za wachezaji mbalimbali.

Hivi inawezekanaje Juventus kutoa fedha nyingi kiasi hiki kumsajili Gonzalo Higuain, wakidhani kwamba ni mtu sahihi kuwapa taji la Uefa? Nini hasa kimewashawishi Juventus kuona kwamba Higuain ni mtu sahihi wa kufanya kazi hiyo?

Juve wametoa kiasi cha euro mil 90 kumsajili Higuain kutoka klabu ya Napoli. Rais wa Napoli Aurelio De Laurentiis alisema kwamba ni kichaa pekee ambaye anaweza kutoa kiasi hicho cha pesa kufanya usajili huo, Sasa yametimia. Je, Juventus wameamua kucheza ‘pata potea’ kwenye usajili huo wa Higuain?

Higuain ameamaliza kiu ya muda mrefu ya Juventus kutafuta mtu mwenye makali mbele ya lango. Hilo ni sawa kabisa. Wamekosa mtu ambaye anaweza kuwa mfungaji bora kwenye ligi kwa takriban muongo mmoja sasa. Licha ya kufanya hivyo akiwa Napoli, hakuna uhakika wowote kwamba Higuain ataweza kufanya hivyo tena akiwa na Juventus. Hawana tatizo sana na ligi michuano ya ndani kwani kwa muda mrefu sana wamekuwa wakitawala.

Ikumbukwe tu wamemsajili pia Miralem Pjanic. Usajili huu ni kama kuzidi kuwadidimiza wapinzani wao. Higuain amethibitisha ubora wake kwenye ligi ya Italy baada ya kufunga jumla ya mabao 71 kwenye michezo 100. Msimu uliopita alikuwa mfungaji bora, na msimu ujao kama atakuwa fiti anaweza kufanya hivyo kwa mara nyingine. Je, hiyo ndiyo kazi iliyomleta pale? Jibu ni hapana.

Hapana shaka kwamba, msimu ujao Juventus watashinda tena taji la Serie A, na kufanya kuwa wamechukua kwa mara sita mfululizo. Sasa hivi si wakati tena wa wao kuhangaika na taji la ligi kwasababu imekuwa ni desturi yao sasa. Hawajamsajili Higuain kwa sababu ya kushinda Scudetto. Lengo kuu la usajili huo ni kushinda kombe la Uefa lakini sioni kama Higuain ni mtu sahihi wa kuwapa taji hilo. Juve kulipa euro mil 90 haimaanishi kwamba thamani yake ni euro mil 90.

Napoli walimsajili Higuain nusu ya pesa ambayo Juventus wamewapa. Wakati anaondoka Madrid alikuwa ni mchezaji ambaye alishindwa kuhimili presha ya kucheza vilabu vyenye presha kubwa. Alifunga magoli tisa tu kwenye Ligi ya Mabingwa katika misimu saba aliyoitumikia Real Madrid. Kwenye mechi 50 alizocheza amefunga magoli 13 tu. Je, hapo huoni kana kwamba kuna walakini kwa Muargentina huyo kuuzwa kiaisi kikubwa cha fedha kama hicho, na tuseme kwamba Juve wameingia mkenge.

Kuna utani unavuma kwamba, kabati la Lionel Messi lingekuwa limejaa mataji ya kimataifa kama isingekuwa Higuain. Aliikosesha Argentina nafasi nyingi kwenye fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 na fainali ya Copa America mwaka jana na zaidi ya hapo mwaka huu pia kwenye Copa America Centenario.

Atakumbukwa pia kwa nafasi aliyokosa mwaka 2010 kwenye hatua ya 16 bora wakati Real Madrid walipokuwa wakicheza na Lyon na kusababisha watupwe nje ya michuano kwa kwa faida ya goli la ugenini. Unakumbuka ile nafasi alyokosa dhidi ya Barcelona akiwa yeye na goli katika mchezo wa nusu fainali ya  Copa del Rey ambapo, Real Madrid walitupwa nje. Higuain si mtu ambaye anaweza kuamua matokeo ya mchezo hasa inapotokea timu inamhitaji kufanya hivyo.

Walau magoli yake aliyofunga akiwa  Napoli yamesaidia tena kumrejesha kwenye ramani kwa muda. Kitu kikubwa ambacho Juve walitakiwa kufanya ni kumwamini zaidi Paulo Dybala ambaye anaonekana kuwa na future kubwa zaidi. Lakini kwa ujio huu wa Higuain, tafsiri yake ni kwamba, sasa Dybala si tena mtu anayepaswa kuangaliwa na kufanywa kama ‘focal point’ ya timu kwenye safu ya ushambuliaji ya Juve.

Kama rekodi yao mbovu kwenye fainali za Uefa ya kupoteza fainali nne kati ya nne walizofanikiwa kuingia ndiyo sababu kubwa ya kumleta Higuain, basi hapo watakuwa wamechanga karata zao vibaya. Huu ni usajili ambao kimsingi hauwezi kuwapa chochote Juventus katika Michuano ya Uefa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here