Home Kimataifa JICHO LA 3: MPANGO ‘A’ UMEKWAMA, HUU NDIYO MPANGO ‘B’ UTAKAOIKOMBOA YANGA

JICHO LA 3: MPANGO ‘A’ UMEKWAMA, HUU NDIYO MPANGO ‘B’ UTAKAOIKOMBOA YANGA

852
0
SHARE

_DSC0666

Na Baraka Mbolembole

Miaka ya mwanzoni mwa 2000, aliyekuwa Waziri mwenye dhamana ya michezo, Mh.Juma Kapuya alishauri jinsi wanahabari wa michezo wanavyopaswa kufanya kazi yao hasa wakati wa matukio ya kimataifa. Wakati huo, timu za Taifa za Olimpiki zilikuwa na matokeo mabaya hadi kufikia kupachikwa jina la ‘Watalii.’

Katika soka, Taifa Stars na klabu zilikuwa na matokeo mabaya huku pia TFF (FAT wakati huo) ikitawaliwa na migogoro. Kapuya alitaka wanahabari kujifunza jinsi ya ‘kuficha ukweli halisi’ kama ilivyo kwa CNN ambayo ilikuwa ikitangaza habari zenye maslai na Taifa kwa mtindo wa kuficha ukweli. CCN ingetangaza vifo vya wanajeshi watatu licha ya kiuhalisia kuwa ni vifo vya wanajeshi 30!

Nimekumbuka yote haya mara baada ya wawakilishi wa Tanzania, timu ya Yanga SC kuchapwa 3-1 ugenini na Medeama SC ya Ghana katika Caf Confederation Cup 2016 jioni ya jana Jumanne huko nchini Ghana.

Yanga wamepoteza game ya 3 kati ya 4 walizokwisha kucheza katika hatua ya makundi. Tangu mwezi Februari mwaka huu wakati klabu za Yanga na Azam FC zilipoanza kampeni yao katika michuano ya Caf nilikuwa upande wao, na nitaendelea kufanya hivyo kwa klabu nyingine yoyote ambayo itakuwa ikituwakilisha Watanzania katika michuano ya kimataifa.

Kila mdau wa kandanda nchini anajua soka letu lipo katika daraja gani. Lakini kwa msomaji wa makala zangu utagundua kuwa mara zote hata kabla ya Yanga kuondolewa katika Caf Champions League na Al Ahly ya Misri niliamini Yanga watawaondoa mabingwa hao mara nyingi wa Caf na kufuzu kwa hatua ya makundi.

Lakini haikuwa hivyo. Yanga waliondolewa katika michuano kwa jumla ya magoli 3-2 mwezi April. Wakaangukia katika Confederation Cup na niliamini kwamba mabingwa hao mara nyingi zaidi wa Bara (26) walikuwa na kila sababu ya kuwaondoa Waangola, timu ya Esperanca na kufuzu katika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo.

Yanga ilisubiri kwa miaka 18 kufika hatua ya makundi katika michuano ya Caf. Mara yao ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1998 walipofuzu kwa hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mabingwa.

Kipigo kutoka kwa Medeama ni kama tayari kimeisukuma nje ya michuano timu hiyo ya Tanzania licha ya kwamba watalazimika kucheza michezo mingine miwili mwezi ujao dhidi ya Waalgeria, MO Bejaia (Taifa Stadium) na Wacongoman, TP Mazembe (Stade de TP Mazembe) ambao tayari waliwachapa katika mchezo ya mzunguko wa kwanza.

Yanga hawana tena nafasi ya kusonga mbele kwenda nusu fainali lakini wanapaswa kupambana kwa kila dakika iliyo mbele yao ili kupata ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi. Kusubiri miaka 18 kufika hatua ya makundi halafu unashindwa kupiga hatua hata moja ni kushindwa na kufeli hata katika matarajio ya chini.

Ikumbukwe, Yanga haikuwahi kupata ushindi katika game zao 6 za Makundi katika Champions league mwaka 1998, kushindwa tena katika michuano ya Confederation itakuwa ni kushindwa juu ya kushindwa na si ajabu wakasubiri kwa miaka mingine 18 ijayo kufuzu kwa hatua ya makundi Caf kwa mara ya tatu.

Kwa kiwango cha Yanga hivi sasa, klabu za VPL zijipange. Kama ni kwa kuhonga waamuzi, waandaaji, ama kwa njia nyingine yoyote ile ya upangaji matokeo, lakini ndani ya uwanja, Yanga wako katika kiwango cha timu ya kimataifa na wataendelea kuwanyanyasa wapinzani wao.

Kushindwa Caf si anguko kwao-kiuhalisia na haitakuwa rahisi kuvuliwa mataji yao ya ndani ya nchi kwa maana wana ubora wa juu kuliko timu nyingine zote.

Timu yoyote katika michuano huwa na mpango ‘A’  kushinda taji. Nadhani ilikuwa hivyo pia kwa Yanga katika michuano ya Confederation Cup 2016. Mpngo una asilimi 97 za kufeli baada ya kupoteza dhidi ya Medeama.

Lakini upi ni mpango ‘B’ ambao utaonesha kupiga hatua kwa timu hiyo katika michuano ya Caf? Mwaka 1998 walipachikwa jina la ‘Jamvi la wageni’ je, wataendelea tena kubaki hivyohivyo tu hadi leo hii wakiwa na mchezaji wa thamani ya milioni 200?

Yanga warudishe nguvu katika mpango wa pili kwa faida ya miaka ya mbeleni. Kushinda walau game moja kati ya mbili zilizosalia dhidi ya Bejaia na Mazembe yatakuwa mafanikio yao mapya katika michuano ya makundi baada ya kufikisha mechi kumi bila kupata ushindi. Sare 3 na vipigo 7 (kiujumla na champions league 1998.)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here