Home Kitaifa MIKASA YA LIGI YA TANZANIA – Part V

MIKASA YA LIGI YA TANZANIA – Part V

650
0
SHARE

Beki wa Mbeya City Abubakar Shabani akimdhibiti beki wa Simba Mohamed Hussein Tshabalala

Na Zaka Zakazi

1969 ulikuwa msimu wa tano wa mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya taifa, ligi ya taifa.

Mwaka huu ulitawaliwa na figisu, visa na mikasa kuliko misimu yote iliyotangulia.

Mwanzo kabisa wa msimu, Sunderland ilitoka sare ya 1-1 na African Sports ya Tanga.

Baada ya mchezo huo, Sunderlad walikata rufaa FAT wakilalamika kwamba Sports walimchezesha kipa ambaye tayari alikuwa ameshachezea timu nyingine ya Ujamaa ya Tanga pia, kwenye msimu huohuo.

Ilidhihirika baadaye kwamba kumbe FAT waliombwa na Sports kuiruhusu timu hiyo kumchezesha kipa mwingine kwa sababu kipa wao namba moja alikuwa anaumwa macho na kipa namba mbili alikuwa safarini.

FAT ilikubali maombi hayo pasipo kutaka kujua kwamba kipa huyo anaitwa nani na anatoka timu gani.

Baada ya mivutano, FAT walikubali makosa ilipobainika kwamba kipa huyo aliichezea Ujamaa msimu huo huo.

Kosa hili pamoja na makosa mengine mengi ya kiutawala yaliifanya serikali kuivunja FAT na kuunda kamati ya muda.

Hata hivyo, Sunderland waliendelea kudai wapewe ushindi kutokana na makosa ya Africans Sports kumchezesha kipa asiyestahili. Wakaweka masharti kwamba endapo hawatopewa ushindi, basi watajitoa kwenye ligi.

Tishio hilo la Sunderland lilizua hofu ya kutokuwepo kwa mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, uliopangwa kufanyika kwenye uwanja wa taifa (siku hizi Uhuru) Machi 3, 1969. Hii ingekuwa mara ya kwanza kwa Yanga na Simba kupambana uwanja wa taifa, kabla ya hapo mechi zote zilichezwa Ilala Stadium (Karume)

Hali ilitulia na matumaini ya kuwepo kwa mchezo huo yakarudi pale kamati ya muda ya FAT ilipoirudishia Sunderland fedha walizolipa kukata rufaa. Sunderland na mashabiki wakaamini kwamba kamati hiyo itaipatia Sunderland ushindi walioujitaji.

Lakini hata hivyo, kamati hiyo iliikata Sunderland maini kwa kusema kosa lililofanyika halikuathiri matokeo ya mchezo ule moja kwa moja.

Sunderland ikakerwa na uamuzi huo na kususa kucheza mchezo uliokuwa ukifuata dhidi ya Yanga na kuwafanya Yanga wapate ushindi wa mezani.

Kamati ya muda ikaidhibu Sunderland kwa kuipiga faini ya shilingi mia tano na endapo ingeshindwa kulipa basi ingeondolewa kwenye ligi.

Lakini baadaye busara ilitumika na pande zilizokuwa zikizongana zilikaa pamoja na kuyazungumza.

Sunderland hawakulipa faini na kamati ya muda haikuipatia Sunderland ushindi dhidi ya African Sports.

Msimu huu uliisha kwa Yanga kuibuka mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.

0718171078

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here