Home Kitaifa HEKO MAKONDA, NI WAKATI WA SOKA LA DAR KUPIGA BAO

HEKO MAKONDA, NI WAKATI WA SOKA LA DAR KUPIGA BAO

637
0
SHARE

IMG_0021

Watu wengi walikuwa wanatafsiri mashindano ya Ndondo Cup kuwa ni ya kihuni na hayana tija yoyote kwa jamii. Wala haiko hivyo, ukweli sasa umeonekana na umejitenga mbali na uongo na dhana potofu kwamba, mashindano ya soka la mtaani yapo kwa ajili ya wahuni au watu walioishiwa.

Kwanini nasema hivi? Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda jana (Juni 20) ameuthibitishia umma kwamba yuko sambamba kuunga mkono Ndondo Cup kwasababu ni mashindano yanayoibua vipaji kwa wachezaji ambao hawana uwezo wa kucheza kwenye uwanja wa taifa na viwanja vingine vikubwa na kuonekana na vilabu vya ligi mbalimbali. Bado unaamini Ndondo ni mashindano ya kihuni?

Viwanja kuboreshwa

Katika kuunga mkono mashindano hayo, Makonda ameahidi kuboresha viwanja vitatu kila mwaka katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzia na Kinondoni, Ilala kisha Temeke. Lakini wilaya mpya za Ubungo na Kigamboni nazo zipo katika mpango huo wa Mh. Makonda kuhakikisha soka linakuwa na kuchezwa katika mkoa wa huu.

Si jambo dogo kuboresha viwanja vitatu katika wilaya moja ndani ya mwaka mmoja, lakini kwa kuzingatia umuhimu wa michezo hususan soka mchezo ambao  kwa sasa unazalisha ajira nyingi zaidi huku watu wakivuna vitita vya fedha na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Ndiyo maana Mh. Makonda ameamua kuboresha miundo mbinu ya viwanja ili vijana wapambane kutafuta ajira hizo.

Ukifanya hesabu za haraka unapata viwanja tisa katika wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam ambavyo vitakuwa na hadhi ya kuchezewa soka angalau kuliko hali ilivyo sasa. Ndani ya miaka mitano kutakuwa na viwanja 15 ndani ya jiji hili, kwa hakika wapenda michezo watakuwa wamefarijika na matunda haya.

Kwa mujibu wa Mh. Makonda, ukarabati huo utahusu sehemu ya kuchezea (pitch), majukwa pamoja na sehemu nyingine muhimu ikiwa ni pamoja na kujenga maduka kuzunguka eneo la uwanja ili kutoa fursa nyingine kwa wafanya biashara.

Wavamizi wa viwanja imekula kwenu

Hakuishia hapo, bado akatoa agizo kwa madiwani kwa kushirikiana na wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanarejesha viwanja vyote ambavyo vimevamiwa na watu ambao si waadilifu na kujenga baa, nyumba za kulala wageni pamoja na makazi.

Maeneo mengi ya wazi ambayo yalitengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo yamekuwa yakivamiwa na baadhi ya watu ambao wamejenga na kuanzisha makazi bila kujali lengo mama la maeneo hayo, lakini Mh. Makonda ameahidi kula nao sahani moja ikiwa ni pamoja na kuvunja nyumba ikiwa itathibitika eneo husika lilitengwa kwa ajili ya uwanja wa michezo na si vinginevyo.

Kwanini Makonda anaunga mkono Ndondo Cup?

Lengo kubwa la michuano ya Ndondo Cup ni kuwapa jukwaa vijana wenye vipaji vya soka kuonesha uwezo wao mbele ya watanzania ili kujipa soko katika vilabu vya madaraja mbalimbali nchini ambako wanaweza kusajiliwa na kucheza huko kama njia ya kufikia malengo yao waliyojiwekea katika kuhakikisha wanakwenda mbali zaidi kisoka.

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuunga mkono juhudi zinazofanywa na waandaaji na wasimamizi wa Ndondo Cup ni za kupongezwa kwasababu wanaofaidika ni walengwa ambao ni wale hasa vijana wa mtaani ambao wanatamani kunyanyuka kisoka lakini wanaishia chini kwasababu hakuna mfumo unaowafanya wapige hatua mbele.

Kwa hili la kuboresha viwanja vitatu kwenye kila wilaya ni jambo la kushukuriwa na wapenda soka wote wa mkoa wa Dar es Salaam, kwasababu moja ya changamoto ambazo michuano hii imekutana nayo ni pamoja na kukosa viwanja vyenye ubora angalau unaofanya mpira kuchezwa katika hali nzuri. Mara kadhaa mashindano haya yamekuwa yakichezwa kwenye viwanja vya shule za msingi na sekondari au kwa kuomba katika taasisi binafsi na kuwa kwenye wakati mgumu hasa pale na wao wanapokuwa wakivitumia.

Kaahidi kuleta makocha 

Jambo lingine kubwa ambalo Mh. Makonda ameahadi ni kuleta makocha wa kigeni kwa ajili ya kufundisha na kuendeleza soka la mkoa wa Dar es Salaam: “Tutengeneze timu ambayo inaundwa na wachezaji wa mashindano haya na tuitafutie waalimu. Tulikaa na balozi wa Ufaransa kuona namna gani tunaweza kupata waalimu, wenzetu wapo tayari,” alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari alipoelezea ni namna gani atashirikiana na Ndondo Cup kupitia chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam.

Je ni Makonda pekeyake anaeunga mkono Ndondo Cup?

Lakini si Makonda pekeyake ambaye ameonesha jitihada za kuunga mkono mashindano ya Ndondo Cup, hata Waziri mwenye dhamana ya michezo Mh. Nape Nnauye na yeye kwa wakati wake alitembelea kwenye uwanja wa Bandari pale Tandika kushuhudia moja ya mechi za mashindano haya na kuonesha kuvutiwa na jinsi ambavyo mashindano yenyewe yanaendeshwa licha ya kuwepo changamoto kadhaa zinazokabili michuano hii.

Pongezi pia zinaenda kwa wadhamini wote wa mashindano haya Dr. Mwaka, Azam TV, Mwanaspoti, Clouds Media Group pamoja na Star Times ambao kwa kuona umuhimu wa kuendeleza mashindano haya kwa manufaa ya wakazi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wameamua kuwekeza na kuunga mkono juhudi za kuhakikisha vijana wanacheza soka, ni jambo la kupongezwa.

‘Heko Mh. Paul Makonda, ni wakati sasa wa soka la mkoa wa Dar es Salaam kusonga mbele.’

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here