Home Kitaifa NAISUBIRI ‘AZAM ACADEMY’ 2016/17, KAWEMBA NA WAHISPANIOLA WAKE…

NAISUBIRI ‘AZAM ACADEMY’ 2016/17, KAWEMBA NA WAHISPANIOLA WAKE…

825
0
SHARE

Kawemba 2

Na Baraka Mbolembole

AZAM FC imesema kwamba haitasajili mchezaji ye yote mpya raia wa Tanzania katika usajili wao mpya na badala yake watajikita zaidi katika mpango wa kuendeleza vijana walio na uwezo kutoka timu yao ya pili. Ni mtazamo mzuri sana si kwa klabu tu bali hadi kwa maendeleo ya timu ya Taifa Stars.

Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure boy’ na nahodha wa mabingwa hao mara moja wa VPL, John Bocco ni mfano bora wa timu hiyo katika ‘ulezi na uendelezaji wa vipaji.’ Kwa miaka takribani nane wachezaji hao wa timu ya Taifa wamedumu hapo huku wakicheza michezo mingi kuliko wachezaji wote waliopo katika timu hiyo ambayo ilipanda ligi kuu na kucheza msimu wao wa kwanza 2008/09.

Aishi Manula, Kelvin Friday, Wazir Salum, Joseph Kimwaga ni wachezaji wengine vijana kutoka timu B ya Azam ambao wanakumbukwa kwa mchango wao mkubwa katika ubingwa wa 2013/14.

Azam FC wana mpango mzuri lakini nao wanachekesha sana wakati mwingine kwa maana huwezi kumsaini kipa ambaye ni wazi atakuwa msaidizi wa Aishi ambaye ni kipa bora wa Tanzania hivi sasa. Mwadini Ally amemaliza mkataba wake katika timu hiyo ya Chamanzi lakini inakuwaje sasa ‘Mpango A-kuwapandisha vijana’ usichukue nafasi yake?

Huyu kipa raia wa Hispania amekuja kwa faida ya timu ya Taifa ya Hispania, Azam FC, wakufunzi wapya raia wa Hispania au yeye binafsi?

Naisubiri kwa hamu kubwa Azam FC mpya, ambayo itakuwa na sura za ‘academy’ ya timu hiyo ambayo tayari imewatoa mastaa kama Farid Musa. Azam ambayo itakuwa na raia zaidi ya watano katika timu na bechi la ufundi. Azam ambayo mtendaji wake mkuu ni Saad Kawemba.

Sina shaka hadi sasa na timu hiyo kwa maana tayari ndani ya kikosi cha sasa kuna wachezaji wengi makini na wenye ubora na uzoefu wa ligi kuu na michuano ya kimataifa. Mtazamo wao kuhusu timu mpya ni mzuri na mara zote umekuwa na matokeo sahihi. Wafanye kweli tu, kila kitu kitakwenda vizuri.

KUPATA MATOKEO

Makocha huwa wanafukuzwa katika timu ikiwa watashindwa kupata matokeo yenye mwelekeo kwa timu. Kitimu na kiuzoefu uwanjani Azam bado ina kikosi tishio lakini wasiwasi mkubwa utakuwa kwa makocha wao wapya ambao kimsingi watakuwa wakianza ujenzi mpya kabisa wa timu hiyo ambayo katika misimu yake 8 iliyopita imekuwa na mafanikio makubwa.

Uzoefu unaweza kuwaangusha makocha wao wapya, ugenini na mazingira mapya ya kazi barani Afrika pia itakuwa ni tatizo. Ila uvumilivu ukiwepo katika timu ya uongozi si ajabu kuanzia Januari mwakani panapo majaliwa timu hiyo itakuwa kali ndani ya uwanja.

Mwanzoni mwa msimu lazima watayumba tu, lakini ukweli ukitazamwa na makocha wapya wakapewa nafasi zaidi mambo yatakwenda vile wanavyotaraji kwa maana tayari ndani ya timu kuna vipaji vya kutosha. Naisubiri ‘Azam Academy’ 2016/17, Kawemba na Wahispaniola wake…

Azam watasafa kupata matokeo mwanzoni mwa msimu ujao, lakini watakuwa tishio katika mbio za ubingwa hadi siku ya mwisho ya msimu kama watavumiliana na kukubali ukweli kwamba hawakuwa na mwazo mzuri kutokana na aina ya mipango yao kiutendaji na kitimu. Yetu ni macho, na nina isubiri kwa hamu.

Picha zote kwa hisani ya azamfc.co.tz

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here