Home Kitaifa JERR MURO ‘ MPENDE MTU HUYU, LAKINI UNARUHISIWA KUTOMPENDA, POLENI TFF…’

JERR MURO ‘ MPENDE MTU HUYU, LAKINI UNARUHISIWA KUTOMPENDA, POLENI TFF…’

790
0
SHARE

IMG_0283

Na Baraka Mbolembole

JERRY MURO ‘mpende’ mkuu huyu wa kitengo cha habari klabuni Yanga SC! Lakini pia unaruhusiwa ‘kutopenda.’ Huyu ni ‘mtu aliye ndani ya mpira wa Tanzania’ anayechukiwa na wengi sana, lakini ukiachana na maneno yake ya mara kwa mara akiwakejeli ‘watani wao wa jadi’ Simba SC katika mbio alizoshinda kwa miaka miwili mfululizo, Murro aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Yanga kabla na baada ya game mbili za timu yake katika michuano ya makundi ya Caf Confederation Cup 2016 amekuwa tishio zaidi kwa baadhi ya watu waliopo ndani ya Shirikisho la mpira nchini-TFF.

Wakati mwingine usipoegemea upande wowote huyu ni mtu ambaye ‘wana-Yanga’ pekee watampenda. Lakini hilo linazidi kumtambulisha kama ‘mtu ngangari kinoma. ‘Alikwishawahi kupewa adhabu na kutakiwa kulipa milioni 5 na Shirikisho hilo la kandanda nchini. Sasa anatakiwa kwa mara nyingine kukutana na ‘wabaya wake’ siku ya Jumamosi hii ambao wamedhamilia kummaliza! Inashangaza kweli kweli, na inasikitisha kuona rais wa TFF akikubali ‘upuuzi’ wa kuitwa kujitetea kwa Murro katika ‘Kamati isiyo na jina.’

Ni wazi baadhi ya watendaji wa TFF wanachukizwa na namna ofisa huyo mwana-habari wa Yanga alivyo na ushawishi na jinsi anavyo-ibust timu, wanachama na mashabiki. Zaidi wamechukizwa na namna Yanga walivyobadilisha utaratibu wa mashabiki kutazama mechi, kutoka viingilio ghali hadi kuingia uwanjani kwa kuvaa fulana tu yenye kuendana na rangi zinazotumiwa na klabu hiyo (kijani, njano na nyeusi.)

Ni wazi kitendo cha Yanga kuwaingiza bure mashabiki 40,000 kimejenga ‘chuki mbaya’ kati ya Murro na kikamati kinachojitafutia jina ili kumfunga mdomo asiwasemee waajiri wake. Hawataweza. Murro si Yanga na kama angekuwa anajisemea yeye mwenyewe sidhani kama angekuwa na kazi hiyo hadi sasa. Murro anaisemea Yanga baada kuzungumza na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Katibu kama ni mambo ya kiutawala, anazungumzia Yanga itaweka kambi wapi, itakuwa wapi na muda gani watakuwa na mechi, wapi, siku gani, maandalizi ya timu yanategemea zaidi maelezo ya benchi la ufundi.

Kwa kawaida kama umechunguza mazungumzo yake mengi, uhamasishaji wa Jerry na usemaji wake huegemea kwenye uelekeo wa mechi au mashindano. ‘Madongo’ anayorusha kwa wapinzani wake na maneno yake ya kejeli huku akiisifu timu yake ( wachezaji, benchi la ufundi na utawala) hutia ‘mshawasha’ mkubwa. Mashabiki wa timu yake, wanachama, viongozi, wachezaji huvutika kusikiliza maneno yake ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa utamu wa timu yake.

Lakini kwanini mnataka kumfungia mtu huyu? Ifungieni Yanga SC si Murro, yeye anaingiza mkate wake na familia yake kwa ajili ya kuisemea Yanga si yeye binafsi. Kwanza tuijue hiyo kamati inayotaka kumfungia Murro halafu tuendelee kusema. Jerr Muro ‘ Mpende mtu huyu, lakini unaruhisiwa kutompenda, poleni TFF. Hii ni vita na haipaswi kuwa vita yenu na Muro bali iwe na Yanga.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here