Home Kitaifa KAMA NI OMOG UELEKEO WA SIMBA SC NI HUU, MAYANJA+MAYANGA NI BORA...

KAMA NI OMOG UELEKEO WA SIMBA SC NI HUU, MAYANJA+MAYANGA NI BORA KULIKO…

1379
0
SHARE

Omog

Na Baraka Mbolembole

KUZUNGUKA huku na huko kusaka kocha kisha kuangukia kwa Mcameroon, Joseph Omog ni sawa na kushindwa mapema vita ya msimu ujao.

Nafikiri Simba SC walipaswa kumuajiri Mganda, Jackson Mayanja kama mkufunzi mkuu na kumsaini kocha wa Tanzania Prisons, Salum Mayanga kama mkufunzi msaidizi kwa kuwa safari zote za Zacharia Hans Poppe nje ya nchi zimeshindwa kumpata kocha sahihi waliyemtaka!

Mayanja na Mayanga wangeweza kuisaidia sana Simba kiufundi na kuimarisha viwango vya wachezaji vijana na kuwafanya wawe bora. Makocha wote hawa (Mayanja na Mayanga) ni wafuasi wa mpira wa chini, kupasiana, kutengeneza nafasi na kusaka magoli, lakini hawawezi kupewa kazi ya kuisuka timu hiyo kwa kuwa viongozi wa Simba wanajaribu kushindana na Yanga SC na Azam FC katika kila kitu.

Omog mtu ambaye aliifanya Azam iachane na mpira wake wa kupasiana na kucheza mchezo wa ‘moja kwa moja’ anakuja Simba kufundisha nini? Sikuona uwezekano wa kocha wa timu ya Taifa ya Zimbabwe kukubali kuacha nzuri aliyoifanya-Kuipeleka nchi hiyo katika fainali za CAN 2017 na kuichukua timu ambayo ndani ya miaka miwili iliyopita imebadilisha makocha zaidi ya wanne.

Nilijua Poppe ameenda kwa ajili ya kujitangana na kujionyesha kwa watu anafanya kazi. Kama Omog atatangazwa kuwa kocha wa Simba ni pigo lingine kwa timu hiyo baada ya kuendelea kuchemsha katika sajili za wachezaji.

Mayanja ni kocha mzuri sana na kama Simba imeshindwa kupata kocha mpya kabisa, wangempa u-bosi Mganda huyu. Ni mtu makini na mjuzi kuliko Omog na stahili ya uchezaji wa vikosi vyake unaendana na ‘tamaduni ya kiuchezaji’ ya klabu hiyo-Kucheza katika kiwango bora, wakipasiana na kutengeneza nafasi za kufunga magoli.

Bila shaka Omog ni chaguo la katibu mkuu mpya anayetaraji kutangazwa muda wowote. Kumpa timu Mayanja ambaye kwa miezi minne ameifundisha kwa kiwango cha kuridhisha, kisha kwa namna yoyote kumchukua Mayanga kutoka Prisons kisha kuwapa uhuru wa kusuka kikosi kipya kungeisaidia sana Simba na pengine walimu hao wa mpira wangetengeneza kikosi kabambe chenye wazawa wengi kwa maana ni wafuasi wa vipaji vya ndani ya Afrika Mashariki.

Mizunguko yote ya Poppe kusaka kocha haikufika kwa Bobby Williamson raia wa Scotland anayeinoa timu ya Taifa ya Kenya. Kama Simba ilihitaji chaguo jipya la kocha katika ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao, upande wangu Bobby pekee ndiye anayewafaa.

Ila kama wameshindwa kupata kocha mpya kabisa wasingekuwa na haja ya kujifikiria mara mbilimbili kwa maana Mayanja ni mtu mjuzi. Ameucheza mpira na sasa ni kati ya makocha bora waliopo Afrika Mashariki. Omog aliwashusha viwango kina Kipre Tchetche kutokana na mbinu zake za kupeleka mashambulizi ya kustukiza.

Ndiyo hakupoteza game yoyote kati13 za mzunguko wa pili Azam FC iliposhinda taji lake pekee 2013/15, mabadiliko ya Omog mara nyingi yaliigharimu timu hiyo katika michezo muhimu. Vipigo kutoka kwa JKT Ruvu, Ndanda SC na namna Azam ilivyopoteza 3-0 dhidi ya El Merreikh ya Sudan katika CAF Champions league mwaka uliopita vilichangiwa mbinu za kiuchezaji za Omog.

Anapenda sana timu zake zijilinde na Simba si timu imara katika kujilinda. Ubora wao katika kumiliki mpira ndiyo silaha inayoibeba Simba katika nyakati zake za mafanikio. Baada ya miezi 6 Simba itasaka kocha mwingine.

Mafionso! Watu wabaya sana na wanapoingia katika madaraka makubwa mafanikio ya jumla ni jambo la kusikia kwenye ‘bomba.’ Mimi nitaendelea kufurahi tu, kwa maana ‘Simba si ya baba yangu (mwenyezi Mungu amrehemu) wala ya mama yangu.’

Njoo Omog, nafasi ya 4 mara ya 3, imetosha! njoo utusogeze hadi nafasi ya 5 msimu ujao. Kama ni Omog uelekeo wa Simba SC ni huu, Mayanja+Mayanga ni bora kuliko.

Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here