Home Kitaifa BAADA YA KUONDOKA KWA BENO KAKOLANYA, NAHODHA WA PRISONS AMEYASEMA HAYA…

BAADA YA KUONDOKA KWA BENO KAKOLANYA, NAHODHA WA PRISONS AMEYASEMA HAYA…

773
0
SHARE
Laurian Mpalile, Nahodha wa kikosi cha Tanzania Prisons 'Wajelajela'
Laurian Mpalile, Nahodha wa kikosi cha Tanzania Prisons 'Wajelajela'
Laurian Mpalile, Nahodha wa kikosi cha Tanzania Prisons ‘Wajelajela’

Na Baraka Mbolembole

MLINZI wa pembeni na nahodha wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Laurian Mpalile amesema hakutaharibika kitu katika kikosi chao licha ya timu hiyo kumpoteza mlinda lango wake namba moja, Beno Kakolanya aliyejiunga na mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC wakati huu wa usajili.

“Tulikuwa na msimu mzuri lakini siwezi kusema ni wa kujivunia sana licha ya kuvuka malengo tuliyojiwekea. Kabla ya kuanza kwa msimu tulijiwekea malengo ya kumaliza ndani ya nafasi Tano za juu, lakini tunamshukuru Mungu tumepata hii ya nne”, anasema Mpalile ambaye alijiunga na Prisons akitokea katika timu za chini mkoani Mbeya mwaka 2009.

Akiwa amedumu hapo kwa misimu 9 sasa, beki huyo namba mbili alikuwapo katika kikosi kilichoteremka daraja msimu wa 2009/10. Alicheza ligi ya chini kwa misimu miwili (2011 na 2012) na kuwasaidia tena mabingwa hao wa Tanzania mwaka 1999 kurejea ligi kuu msimu wa 2012/13.

Chini ya kocha Jumanne Chale timu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya pili VPL mwaka 2002 na msimu wa 2007/08 ikanusurika kushuka siku ya mwisho ya msimu wa 2013/14.

Baada ya kuinusuru timu hiyo kutoteremka tena daraja la kwanza, kocha David Mwamaja hakuwa na msimu mzuri 2014/15 na mambo yalipoelekea kubaya zaidi, Mbwana Makatta akapewa nafasi yake na aliweza kuingoza timu hiyo katika game nane mfululizo za mwisho bila kupoteza na kwa mara nyingine Prisons ikanusurika kushuka daraja siku ya mwisho ya msimu wa 2014/15.

Timu ikaangukia kwa aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Salum Mayanga ambaye pasipo kutarajiwa na wengi ameweza kuiongoza timu hiyo kumaliza msimu katika nafasi ya nne-nafasi yao ya juu zaidi tangu mwaka 2008.

“Wakati mimi naingia katika timu nikiwa na miaka 22 mwaka 2009, Prisons ilikuwa na utaratibu mzuri wa kuingiza wachezaji vijana katika timu. Baada ya kina Osward Morris kustaafu kutokana na umri kuwatupa mkono, kukisuka kikosi kipya ikawa kazi ndiyo maana uliona jinsi tulivyo tetereka kidogo. Lakini baada ya kukisuka kikosi kipya ikiwemo kuingia kwa vipaji bora vichanga katika timu, sasa hivi angalau tumeanza kusimama kidogo.”

Anasema Mpalile mwenye miaka 29 wakati nilipofanya naye mahojiano marefu siku ya Jumatano hii akiwa mapumzikoni mkoani Mbeya baada ya kumalizika kwa msimu. “Misimu yote malengo ya Prisons ni kumaliza katika nafasi 3 za juu katika ligi na tunajipanga kuhakikisha tunasogea juu zaidi ya tulipomaliza msimu huu.”

“Kipindi fulani nyuma utaratibu wa kuwapindisha wachezaji vinaja ulipungua na ni sababu kubwa ya Prisons kuyumba katika misimu michache iliyopita.”

Prisons ilikuwa na mchezo mzuri wa kushambulia huku wakiwa wagumu kufungika hawakupoteza mchezo wowote katika uwanja wa nyumbani kati ya 15 waliyocheza Sokoine Stadium. Wachezaji vijana kama Lambert Sibiarka, Mohamed El-Fadhil, Beno, Jeremiah Juma na Mohamed Mkopi waking’ara kwa kiasi kikubwa.

“Prisons imekuwa ikipoteza wachezaji wake nyota tangu miaka ya nyuma lakini baada ya kutetereka kidogo sasa unaona timu kama Mtibwa nayo ikiingia katika utaratibu wa kuuza wachezaji. Lakini ninavyokumbuka mimi wachezaji kama Herry Morris, Samson Mwamanda, Primus Kasonso, Geofrey Bonny, Stefano Mwasyika, David Baruani wote wamewahi kuhama hapa na kujiunga na timu nyingine kubwa.”

“Hivyo sioni kama tutatetereka ikiwa wachezaji wengine kama Beno na hawa wanaotakiwa na timu kubwa kama Jeremiah na Mkopi wakiondoka. Nafahamu baadhi ya vitu katika uchezaji huwa vinapungua ikiwa timu inajengwa na kubomolewa ndani ya muda mfupi. “

“Kuondoka kwa Beno kunafungua nafasi ya kipaji kingine tena ambacho na chenyewe kitakuja kuwa staa baadaye. Sisi wachezaji tutakaokuwepo tutajitahidi kujenga timu nyingine nzuri ili tuzidi kuwa bora.”

“Naweza kusema mwalimu (Salum Mayanga) ni sababu kubwa ya kwanza ya ubora wetu msimu uliopita. Alipokuja katika timu alikuta vichwa vya wachezaji vimevurugika na kujiona kama timu isiyostahili kushindana.”

“Tulikuwa kama wachezaji tulio katika ligi kwa ajili ya kucheza tu ligi. Kitu cha kwanza mwalimu alichokifanya ni kutusaidia kutujenga kisaikolojia, na kutuambia kuwa ‘tunaweza’ kushinda na kufanya vizuri tofauti na tulivyokuwa tukiamini sisi baada ya kunusurika kushuka mara mbili.”

Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here