Home Kimataifa MICHUANO YAKE YA TANO KAMA KOCHA WA BRAZIL, DUNGA BILA NEYMAR BRAZIL...

MICHUANO YAKE YA TANO KAMA KOCHA WA BRAZIL, DUNGA BILA NEYMAR BRAZIL ITAFANYA NINI USA?

859
0
SHARE

Neymar-Dunga

Na Baraka Mbolembole

Carlos Dunga anajiandaa kwa michuano yake ya tano mikubwa kama kocha wa Brazil. Nahodha huyo wa zamani wa ‘Five time Champions’ alishinda ubingwa wa Copa America mwaka 2007 (taji la mwisho la Brazil katika michuano hiyo.)

Dunga aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa kocha wa ‘Selecao’ mara baada ya mabingwa hao mara tano wa kihistoria wa kombe la dunia walipo ‘chemsha’ katika michuano ya Ujerumani mwaka 2006 chini ya mkufunzi-mshindi wa taji la dunia 1994, Carlos Alberto Perreira.

Michuano ya pili ya Dunga akiwa kocha wa Brazil ni ile ya Olimpiki, Beijing, 2008 ambayo Brazil walikomea nusu fainali mbele ya mahasimu wao Argentina (Brazil ilifungwa 3-0.)

Kushindwa kutwaa medali ya dhahabu katika michuano hiyo ambayo Brazil haijawahi kushinda kulimfanya Dunga kuwaacha wachezaji wengi vijana ambao aliwaingiza katika timu kama mbadala ya wazoefu kama, Ronaldo De Lima, Ronaldinho, Roberto Carlos, Adriano, Lucio, Emerson ambao walionekana sababu ya Brazil kuanguka katika michuano ya Ujerumani chini ya utawala wa Perreira.

Rafinha ambaye nakumbuka alipata kadi nyekundu ya ‘kipuuzi’ wakati Brazil ikiwa pungufu kufuatia kadi ya kwanza ya mlinzi, Miranda. Anderson, Marcelo, Hernanes ni vijana wengine ambao ‘waliwekwa kando’ na Dunga na mwalimu huyo akakimbilia barani Ulaya kujaribu kutengeneza timu ambayo angekwenda nayo katika kombe la dunia 2010 Afrika Kusini.

Kiukweli, Brazil chini ya Dunga haijawahi kuwa na mchezo wa kuvutia sana kama ilivyozoeleka. Dunga hutumia mbinu za kujilinda na mashambulizi ya uhakika ya kustukiza. Alishinda kombe la mabingwa wa FIFA wa mabara 2009 nchini Afrika Kusini.

Akiwa na Luis Fabiano, Robinho, na Hulk katika safu ya mashambulizi, Ricardo Kaka’, Filipe Melo na Giberto Silva katika idara ya kiungo, Maicon, Michael Bastos, Lucio na Juan katika idara ya ulinzi na golikipa Julio Cesar, bado Brazil ya Dunga haikuwa timu tishio licha ya kuzifunga timu kama Misri, Italia na Marekani na kushinda taji lake la pili kama kocha wa Brazil.

Kuonyesha ni namna gani hakuwa na timu bora, Brazil iliyokuwa imecheza kwa kiwango cha chini dhidi ya Korea Kaskazini, Ivory Coast na Ureno katika hatua ya makundi ilikosa mbinu na kuchapwa 2-1 na Holland na kuondolewa katika robo fainali ya michuano ya kombe la dunia 2010. Ulikuwa ni mwisho wa kwanza wa Dunga kama kocha wa Brazil.

Kurejea kwake kwa mara ya pili natazama kama ‘njia ya Selecao’ kukwepa timu yao kuangukia kwa kocha wa kwanza wa kigeni kufuatia kushindwa kwa Mano na Big Phill.

Brazil imekosa mbinu za kisasa?

Hispania wametawala mpira wa Ulaya tangu walipofanikiwa kushinda ubingwa wao wa kwanza wa kimataifa baada ya miaka 44 mwaka 2008. Baada ya taji lile la Euro lililoambatana na kiwango cha juu na kandanda la kuvutia, La Roja wakaenda Afrika Kusini na kushinda taji la dunia-Ikawa timu ya kwanza ya Ulaya kufanya kutwaa WC nje ya bara la Ulaya.

Na baada ya kushinda taji lao la tatu kubwa-mfululizo mwaka 2012 nchini Austria, Hispania ikawa ikitajwa kama timu bora zaidi kuwahi kutokea duniani. Spain walikuwa wakicheza vizuri zaidi ya hata Brazil iliyoshinda ubingwa wao wa tano na wa mwisho wa dunia mwaka 2002 nchini Japan.

Wakati Mano alipochukua timu kutoka kwa Dunga Julai, 2010 alisema ‘Brazil imeziacha timu za Ulaya zicheze mpira wao na wao kucheza mpira ambao Ujerumani walikuwa wakiucheza zamani.’

Lakini naye alishindwa, licha ya kutegemea vipaji vichanga kama Neymar, Oscar, David Luiz. Big Phili aliporejea kuchukua nafasi ya Mano baada ya Brazil kufanya vibaya katika michuano ya Olimpiki, London, 2012 alijaribu kutengeneza timu ya mpito kwa ajili ya WC 2014.

Ushindi wa 3-0 dhidi ya Hispania katika fainali ya mabingwa wa mabara Juni, 2013 si tu ulimaliza maswali kama La Roja ni timu bora zaidi kuwahi kutokea, bali uliambatana mchezo wao maarufu wa ‘samba.’ Brazil ilikuwa na Fred, Hulk na Neymar katika mashambulizi na Scorali alienda na safu hiyo katika BRAZUCA ila bado haikutosha.

Baada ya michuano mizuri ya mabara ambayo walishinda ubingwa kwa mara ya nne, Brazil ya ‘ilikutana na aibu kubwa ya michuano’ kufuatia kuchapwa 7-1 na Ujerumani katika game ya nusu fainali. Ulikuwa mwisho wa Pili wa Big Phill huku akifungua milango kwa mara ya pili kwa Dunga kuichukua timu hiyo.

Michuano iliyopita ya Copa America 2015 nchini Chile ilishuhudia mabingwa hao mara nane wa Copa America wakishinda mara mbili tu katika michezo minne ambayo Dunga alishuhudia timu yake ikicheza mpira mbovu.

Ilianza kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Peru-shukrani kwa goli la dakika za mwisho kutoka kwa kiungo Douglas Costa. Selecao walilazimika kutoka nyuma na kushinda game hiyo ya kwanza katika hatua ya makundi, lakini wakajituka wakianguka mbele ya Colombia katika game ya pili baada ya kuchapwa 1-0.

Ilibidi wapambane haswa ili kuifunga Venezuela 2-1 katika mchezo wa mwisho katika kundi. Mechi dhidi ya Colombia ilimfanya Neymar kufungiwa na hivyo akashindwa kuichezea Selecao dhidi ya Venezuela kisha katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Paraguay.

Neymar alionekana katika vurugu kati yake na Carlos Bacca na adhabu yake hiyo imeinyima nafasi katika michuano inayotaraji kuanza mwishoni mwa wiki hii nchini Marekani. Dunga anakumbuka namna timu yake ilivyobanwa na kulazimishwa sare ya kufungana 1-1 kisha kupoteza kwa penalti 4-3 dhidi ya Paraguay mwaka uliopita.

Uteuzi wake safari hii si mbaya kwa maana amechukua wachezaji walio fiti na ubora Brazil haitakuwa na Neymar, Costa, David Luiz, Thiago Silva, Oscar, Fernandinho, Fernando lakini uwepo wa nyota wazoefu kama Dan Alves (33,) Miranda (31,) Filipe Luis (30,) Ricardo Kaka’ (34,) Elias (31,) Jonas (32,) na Hulk (29,) kunaweza kuziba vizuri mapengo ya kina Neymar.

Dunga amewaita washambuliaji, kinda wa miaka 19, Gabriel Barbosa kutoka Santos FC, Hulk na Jonas anayekipiga Benfica ya Ureno.

Katika kiungo, Kaka’, kijana wa La Masia, Rafinha (23,) kiungo mchezesha timu, Phillipe Coutinho (23,) Willian (27,) Renato Agusto (28) wa Beijing Guoan, Luiz Gustavo (28,) Lucas Lima (25) kutoka Santos, Elias kutoka Corinthians na Casemiro (24.)  

Katika beki, ukiachana na Alves, Miranda, kocha Dunga amewaita pia Fabinho (22) kijana huyo anachezea AS Monaco ya Ufaransa, Douglas Santos (22) kutoka Atletico Mineiro, Rodrigo Caio (22) kutoka Sao Paulo na mlinzi wa PSG ya Ufaransa, Maquinhos.

Je, michuano yake ya tano kama kocha wa Brazil, Dunga bila Neymar ‘Five time Champions’ watafanya nini USA?

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here