Home Ligi EPL ACHANA NA 2016-17, WAINGEREZA WATAITEKA DUNIA 2017-18

ACHANA NA 2016-17, WAINGEREZA WATAITEKA DUNIA 2017-18

917
0
SHARE

The Big five

Na  Ayoub Hinjo

Mzunguko wa maisha yetu ya kila siku ndiyo unafanya tuzidi kuheshimiana kwasababu tupo kwenye madaraja tofauti. Kwahiyo lazima tuishi kwa kutegemeana. Unadhani binadamu wote tungekuwa matajiri nani ange-mheshimu mwingine? Au tungekuwa masikini nani angetoa heshima kwa mwenzake? Lakini madaraja ya maisha yameleta usawa kati yetu.

Katika stori hii ya maisha Waingereza walijitenga na dunia yote. Walijifungia vyumbani kutafuta nini kimewasibu katika dunia ya soka hawasikiki tena zaidi ya ligi yao kuwa maarufu zaidi na kupendwa duniani. Waingereza walijifungia ndani wakitafakari kwanini hawatoi washiriki kwenye tuzo kubwa za duniani kama Ballon d’Or basi kama hapo imekuwa ngumu kwao kwa kipindi hiki hata kuingiza mchezaji kwenye kikosi bora cha dunia hawana? Waingereza wapo na mengi ya kutafakari kwa sasa tuwaache kwanza najua wakipata majibu watatoka kwenye vyumba walivyojifungia kuleta usawa wa madaraja tena.

Wahispania wameiteka dunia kwa sasa. Kila kilicho bora kinatoka kwao kuanzia mchezaji bora wa dunia, mfungaji bora na hata idadi kubwa ya wachezaji walio katika kikosi cha dunia wanatoka katika himaya yao ndani ya La Liga. Ni zaidi ya misimu saba sasa Wahispania wanatoa washiriki watatu wanaogombea tuzo ya Ballon d’Or na mwishowe ndani ya misimu hiyo saba wamechukua mara saba zote wao. Kwa hali hiyo unaweza kuona kwanini Waingereza wamejifungia ndani na kutafuta majibu ya kwanini ubora wao umepotea ghafla mno.

Majibu ya Waingereza yataanza kuonekana kuanzia msimu ujao wa 2016-17. Lakini majibu hayo hayatokuja na jibu kamili kwasababu Wahispania watahitimisha msimu wa nane kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia kupitia mambo makubwa waliyofanya msimu wa 2015-16. Pamoja na msimu wa 2016-17 hautokuwa na majibu sawia lakini walau tutaweza kushuhudia Waingereza wakirejea kwenye ubora wao wa miaka ya nyuma. Ule ubora wao wa kushindana hadi hatua ya mwisho au ule ubora wa kuishia nusu fainali ni mafanikio pia.

Uwepo wa Mourinho, Guardiola, Conte na Klopp una majibu makubwa mno kwa Waingereza na ligi yao. Hao ndiyo wamewatoa Waingereza vyumbani walimo jifungia na sasa Waingereza watakapo iteka dunia ndiyo watatambua kuwa binadamu tunategemeana na usawa upo kati yetu.

Uwepo wa makocha hao bora kabisa duniani unavuta hisia za wachezaji bora kutoka sehemu mbalimbali kujumuika nao sababu wanaamini kuwapo chini ya vichwa hivyo hawawezi kutoka mikono mitupu bila kuambulia ubingwa. Hapo ndipo tunakumbuka mara ya mwisho Waingereza kutoa mshiriki kwenye Balloon D’Or ni miaka 8 iliyopita alikuwa Cristiano Ronaldo.

Ligi ya Uingereza ni ligi maarufu na yenye ushindani mkali duniani lakini pamoja na vyote hivyo wachezaji wa viwango vya kawaida walikuwa wamejaa katika misimu hii ya karibuni. Tena wachezaji hao wamejaa kwenye timu ambazo wao wanaamini ni timu kubwa katika ligi yao. Msimu wa 2016-17 tutashuhudia Leicester City akiiwakilisha Uingereza katika michuano ya Ulaya. Timu ya Leicester haina wachezaji wa madaraja ya juu na wala sio kivutio kwa wachezaji wa juu lakini ndiyo mabingwa na wataiwakilisha nchi.

Kelele za vyombo vya habari vya Uingereza vitaanza kutamba kuanzia msimu ujao ambao Guardiola atakuja Manchester City na wachezaji bora. Mourinho atahamia United na wachezaji bora. Klopp atavyosajili majembe ya hatari pale Anfield na Conte atavyofundisha wachezaji bora pale darajani. Hapo ndipo ligi ya Uingereza itarejea na kuanza kutamba duniani.

Maingizo mapya ya makocha yao, yana maana kubwa mno kwao. Wamekuja kufufua upya ligi hiyo na kelele za wenye ligi yao. Msimu wa 2016-17 Waingereza watakaa kimya sababu wanajua wawakilishi wao hawana ubavu wa kupambana na Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid, Bayern Munich, Juventus na wengine hadi mwisho lakini msimu wa 2017-18 Waingereza watanyanyuka na kuanza kuimba nyimbo zao ambazo hawaimbi kwa sasa.

Kuwaondoa Wahispania na Wajerumani moja kwa moja ni kosa kubwa mno lakini kurejea kwa Waingereza kutafanya vita iwe kubwa katika kila watakacho shindana. Muda wa Waingereza kurejea haupo mbali. Amini hivyo kuanzia 2017-18 Waingereza wataiteka dunia.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here