Home Kitaifa KIIZA-MSHAMBULIAJI MWENYE ‘NJAA YA MAGOLI’ NA MWENYE ‘SHABAHA’ ANAONEKANA KUPWAYA MBELE YA...

KIIZA-MSHAMBULIAJI MWENYE ‘NJAA YA MAGOLI’ NA MWENYE ‘SHABAHA’ ANAONEKANA KUPWAYA MBELE YA POPPE ‘MR. KAZI NYINGI’

586
0
SHARE
Hamisi Kiiza akishangilia goli lake la kwanza dhidi ya Stand United kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga

Hamisi Kiiza akishangilia goli lake la kwanza dhidi ya Stand United kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga

Baraka Mbolembole

Mchezo wake wa kwanza tu akiwa na jezi ya Simba SC akafunga goli, akafunga tena katika game ya pili na kufikia mchezo wa tatu akiwa na timu hiyo mshambulizi Mganda, Hamis Kizza akawa amefunga ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika msimu wake wa nne katika ligi kuu Tanzania.

Kizza alifunga dhidi ya African Sports, JKT Mgambo na kufunga magoli matatu kwa mpigo katika game ya tatu ya Simba mwezi Septemba 2015. Kwa kweli kama mshambuliaji Kiiza amevuka hata matarajio yake mwenyewe kwa kufanikiwa kufunga jumla ya magoli 19 katika mechi zisizodizi 25 katika ligi kuu.

Bila shaka mshambulizi huyo wa timu ya Taifa ya Uganda atashinda tuzo ya mfungaji bora katika michuano ya FA Cup msimu huu baada ya kufunga magoli matano katika game tatu wakati Simba ilipoishia robo fainali ya michuano hiyo. Amefunga kila mchezo katika michuano hiyo ambayo Simba walitolewa na Coastal Union.

Licha ya kuanza msimu vizuri katika klabu yake hiyo mpya, nilikuwa nikiandika kuhusu timu yao kukosa umoja na upendo miongoni mwa wachezaji wao nyota na viongozi wa juu.

Pamoja na kuwapo kwa misuguano ya mara kwa mara kati uongozi, Kiiza licha ya kusajiliwa na wachezaji kadhaa wapya kabla ya kuanza kwa msimu bado aliendelea kutajwa na kutazamwa kwa ‘matarajio’ makubwa ya Simba kushinda ubingwa wao wa kwanza baada ya kushindwa kufanya hivyo tangu msimu wa 2011/12 waliposhinda VPL kwa mara ya mwisho.

Kwa mchezaji ambaye alicheza Yanga SC (mahasimu wa Simba) kwa misimu mitatu na kutemwa kwa sababu za kushuka kwa kiwango chake bila shaka presha ilikuwa kubwa sana kwa Kiiza. Simba iliyokosa makali bila mshambuliaji mfungaji msimu wa 2014/15 ilianza kampeni zao katika ligi kuu kwa ushindi mfululizo katika mechi nne za mwanzo kabla ya kupoteza mechi ya kwanza ya msimu mbele ya Yanga kwa kulazwa 2-0.

Mchezo wa kwanza kwa Kiiza kutofunga msimu huu. Katika mechi zote alizoichezea Simba msimu huu hadi ile ya kichapo dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Taifa, Kiiza alikuwa ‘mtu wa mashabiki’ na ‘hatabanduka’ midomoni mwetu baada ya kumalizika kwa msimu.

Mshambuliaji mwenye ‘njaa ya magoli’ na mwenye ‘shabaha’ anaonekana kupwaya mbele ya viongozi wa timu yake na hata kwa baadhi ya waandishi kwa kuwa tu ‘alidai mshahara wake uliochelewa kwa wiki moja!’

Ambaye hakucheza mpira wa ushindani hawezi kuona thamani ya Kiiza na jitihada zake, ila kwa mwanasoka ataelewa ni kiasi gani Kiiza anastahili kudai mshahara wake au kuulizia masaa 24 baada ya muda wake wa malipo kupita.

Mpira usifananishe na kazi nyingine yoyote ile, hii ni kazi ngumu zaidi ambayo mchezaji anaifnya mfululizo kwa zaidi ya miezi kumi kati ya 12 ya mwaka, hakuna muda wa kupumzisha mwili kama ‘wewe na peni yako’. Kila siku mchezaji anatoka jasho kila sehemu ya mwili wake. Soka ni kazi ngumu ndiyo maana ina thamani kubwa zaidi ulimwenguni.

Kiiza amekuwa na kiwango cha kufadhaisha katika baadhi ya mechi (game mbili na Yanga, nyingine dhidi ya Toto Africans, Mwadui na Tanzania Prisons) wakati Simba iliposhindwa kupata matokeo katika michezo hiyo.

Tabia ya Kizza iko kwa kila mtu kuiona, lakini kama mwanadamu wakati mwingine kwa mambo mabaya, kama kitendo chake cha kukataa kupanda gari la pamoja na sare za wadhamini na kutumia usafiri binafsi.

Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Simba itaachana na wachezaji wote wanaotanguliza maslahi badala ya uzalendo kwa klabu.

Naona nikuulize wewe ‘BOSI KUBWA AMBAYE UNAFANYA KILA UTAKALO HAPO SIMBA’ ukiwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ambayo mimi binafsi siwataki muwepo, KUNA MCHEZAJI AMBAYE ULIMSAINI NA KUWEKA MAKUBALIANO YA UZALENDO KWANZA KABLA YA MALIPO?

Kama yupo mtaje! Hakuna ‘mpira mapenzi’ miaka hii tena ‘NYIE WENYEWE VIONGOZI MKIWAAMBIA WACHEZAJI WENU KUWA SIMBA SI YA BABA ZAO’ nani leo hii achezee timu yenu kwa mapenzi bila kulipwa? Kiwango kibovu cha ufikiri na utoaji maamuzi ya wazi kwa utawala ndicho kimeshusha matarajio ya timu.

Poppe nikwambie ukweli kwamba ‘Simba si Yako’ na maamuzi yako unayokurupuka kila mara unawaumiza sana maelfu ya wana Simba. Kama Simba itamuacha Kiiza nawashauri wanachama na wapenzi wa Simba kususia kununua baadhi ya bidhaa za klabu, kuhudhuria michezo ya maandalizi ya msimu wa 2016/17.

Sidhani kama Simba inahitaji tena fedha za Poppe ‘MR. KAZINYINGI,’ kama atatoa tena hata shilingi yake katika usajili ujao, Simba mmekwisha, mjiandae kwa msimu wa tano wa mateso. ‘Timu haitashuka ila cha moto mtaendelea kukipata’  Kwa mwana Simba ni machungu sana kuona mwenendo wa klabu hivi sasa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here