Home Kitaifa JICHO LA 3: SABABU 5 MUHIMU ZILIZOWAPA YANGA ‘NDOO YA 26’ VPL

JICHO LA 3: SABABU 5 MUHIMU ZILIZOWAPA YANGA ‘NDOO YA 26’ VPL

1204
0
SHARE

IMG_0450

Safari ya taji lao la 26 la ligi kuu Tanzania Bara (VPL) ilianza kwa style ambayo haikuzoeleka hata kwa mashabiki wa Yanga SC wenyewe kwa maana wamezoea kuona mwanzo mbaya wa timu yao kila msimu na kuanza kuimarika kadri ligi inavyosonga mbele.

Yanga ilishinda game tano mfululizo za mwanzo wa msimu na kukusanya alama 15. Ilianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga, 13 Septemba, 2015. Siku tatu baadae wakaichapa 3-0 Tanzania Prisons ya Mbeya.

Moto huo haukuzimika, wakairarua 4-1 JKT Ruvu, Jumamosi ya Septemba 19. Mechi zote hizo walipata ushindi wakiwa wenyeji na mechi yao ya kwanza ya ugenini ilikuwa dhidi ya mahasimu wao Simba SC, wakashinda 2-0.

Siku ya mwisho ya mwezi Septemba, Yanga walisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam na kwenda Morogoro kuwavaa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri sehemu ambayo hawakuwahi kupata ushindi tangu mwaka 2009. Wakashinda tena 2-0 na kumaliza mwezi Septemba wakiwa na pointi 15 sambamba na timu ya Azam FC.

Matokeo yao hayo yalinishangaza hata mimi kwa maana nilizoea kuona timu hiyo ikianza ligi kwa matokeo mabaya. Mechi dhidi ya Mbeya City FC siku ya Jumanne wiki hii imeipa rasmi Yanga taji la msimu huu, likiwa ni la pili mfululizo na la 26 kihistoria.

Hawa ni mabingwa wa ukweli ukizingatia wamepoteza mara moja tu katika game 29 walizokwisha cheza. Ikiwa tayari wamekabidhiwa kombe lao katika game ya Jumamosi hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (wakiwa wageni wa Ndanda SC) ‘Jicho langu la Tatu’ limeutazama msimu wa 2015/16 na ‘kung’amua’ baadhi ya sababu muhimu za ndani na nje ya uwanja zilizowapa taji hilo timu ya Yanga.

MAANDALIZI MAZURI

Kabla ya kuanza kwa msimu Yanga ilikwenda mkoani Mbeya na huko wakaweka ‘kambi tulivu’ ambayo iliwasaidia baadhi ya wachezaji wapya kuzoeana na wale wa zamani. Kutolewa katika hatua ya robo fainali na Azam FC katika michuano ya CECAFA Kagame Cup mwezi Julai kulitazamwa kama kigezo cha msimu mgumu katika VPL hivyo timu ilishikamana kwa uhakika wakati wakiwa Mbeya kisha Zanzibar.

Ikiwa na wachezaji wapya kama Mwinyi Hajji, Thaban Kamusoko (Zimbabwe,) Vicent Bossou (Togo,) Deus Kaseke, Malimi Busungu, Geofrey Mwashuiya, Donald Ngoma (Zimbabwe,) Matheo Anthony bila shaka wakufunzi Hans Van der Pluijm na Charles Boniface Mkwassa (kabla hajateuliwa kuwa mkufunzi wa timu ya Taifa-Taifa Stars) walipata muda wa kutosha kutengeneza mifumo yao ukizingatia walikuwa wamewapoteza wachezaji kama Mrisho Ngassa, Kpah Sherman (Liberia,) Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Jerson Tegete.

Wakati akiwa kocha wa Sunderland nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane alikuwa akiwaambia wachezaji wake kwamba, ‘ Kushindwa kujiandaa ni kujiandaa kushindwa.’ Maandalizi ya Yanga yalikwenda vizuri na yalichangia kwa kiasi kikubwa makali yao mwanzoni mwa msimu.

HANS VAN DER PLUIJM

Nimekwisha andika makala kadhaa kuhusu mtaalamu huyu wa ufundishaji raia wa Holland ambaye amejipa mwenyewe alama ya mapinduzi klabuni hapo kwa kuifanya Yanga icheze mchezo wa kupanga mashambulizi yenye uhakika na kushambulia kwa kasi huku wakipasiana kwa kwenda mbele.

Ikiwa ndiyo mara yake ya kwanza kuanza maandalizi ya msimu akiwa amefanya usajili wake mwenyewe Hans ni sababu ya pili kubwa iliyowa Yanga taji. Hajawahi kuwa na tofauti na wachezaji wake licha ya mara kadhaa baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa na tofauti na wachezaji wake, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi, Amis Tambwe.

Hans ni mtu anayejiheshimu na umri wake wa zaidi ya miaka 65 umemfanya kujenga mshikamano, kuheshimiana na busara katika timu yake. Ni kama alisoma alama za nyakati jinsi ya kuwaendesha wachezaji wake na wakampa mafanikio.

Kama baba anahitaji mafanikio zaidi, ni rahisi kwa mtoto kutamani hivyo pia. Hans amejipa mwenyewe majukumu ya baba bora na wachezaji wamekuwa watoto watiifu. Timu yake ilipoteza game kwa mara ya kwanza katika mzunguko wa 16, tena kichapo cha kufadhaisha kutoka kwa Coastal katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili wakiwa Mkwakwani Stadium, Tanga.

Akashuhudia timu yake ikisawazisha kwa mkwaju wa penalti dhidi ya Prisons zikiwa zimesalia dakika 7 game kumalizika katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. Wapinzani wao wakaanza kuwapiga ‘vijembe’ na kusema wameanza kuchoka. Kilichofuata ni stori kuwa ‘Yanga wanabebwa.’

TIMU KWA MAANA YA TIMU NZIMA

Ndani ya uwanja hadi kufikia mchezo wa 20 Yanga walikuwa wamecheza jumla ya mechi 15 pasipo nyavu zao kutikiswa huku mchezo wao wa kwanza kumaliza dakika dakika 90 pasipo kufunga goli ukiwa ule wa Desemba 12 ugenini dhidi ya JKT Mgambo ya Tanga-game iliyomalizika 0-0. Ilikuwa ni mechi yao ya kumi ya msimu.

Hii inamaanisha kuwa timu yote ilifanya kazi nzuri. Washambulizi wamefanya kazi ipasavyo tena kwa ufanisi mkubwa sana kiasi cha kufanikiwa kufunga magoli 68 hadi sasa. Viungo walifanya kazi yao vizuri kwani timu ilikuwa ikicheza katika muonekano wa kucheza kuanzia nyuma, katikati kisha mipira kwenda kwa washambuliaji.

Safu ya ulinzi licha ya kukabiliwa na uchovu wa kucheza mfululizo imeweza kuilinda timu yao kwa kushirikiana na walinda mlango wao kiasi cha kuruhusu magoli 16 tu. Yanga wamejibeba wenyewe kwa mbinu zao, umoja wao katika kazi na moyo wa kujitolea wa benchi la ufundi na wachezaji.

Kuna wachezaji mmojammoja wamefanya kazi nzuri zaidi, mfano, washambuliaji, Amis Tambwe na Donald Ngoma ambao wamefunga jumla ya magoli 39 katika VPL pekee lakini vipi kuhusu kazi nzuri ya kina Saimon Msuva, Kamusoko, Salum Telela, Kaseke, Ally Mustapha, Deogratius Munish, Oscar Joshua, Juma Abdul, Kelvin Yondan, nahodha, Nadir Haroub, Mwinyi, Niyonzima, Mwashuiya, Bossou, Matteo, Hans, Mkwassa, Juma Mwambusi, timu ya watabibu na safu ya utawala?

Yanga wamefanikiwa kama timu licha ya kuwepo pia kwa jitihada binafsi za wachezaji na mbinu zao bora kiucheza ji.

YUSUPH MANJI

Mwenyekiti huyo wa klabu alizungumza na kila mchezaji kwa njia ya simu kabla ya Yanga kucheza na City siku ya Jumanne. Kila mchezaji alijiona mwenye kuthaminiwa na tajiri huyo. Ni kielelezo cha Manji kuwatii wachezaji wake na kuwapa shukrani ya kile walichofanya kwa msimu mzima.

Ikumbukwe mwishoni mwa mwezi Desemba 2015 Yanga ilitangaza kusitisha mkataba wake na Niyonzima kufuatia mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda kuchelewa kurejea klabuni baada ya kumalizika kwa michuano ya Cecafa Challenge Cup nchini Ethiopia.

Niyonzima alijitetea kwa kudai kwamba alikuwa mgonjwa na alirudi akiwa amefunga plasta ngumu (P.O.P) katika kifundo chake cha mguu na alisema alilazimika kujitibu kabisa kwa kushirikiana na madaktari wa timu yake ya Taifa kwani alikuwa akicheza na maumivu kwa muda mrefu.

Tiboroha alificha nyaraka hizo wakati Niyonzima alipotuma kwa klabu. Sijui ni kwanini ila Manji alijua kuhusu ubora wa Haruna na nidhamu hivyo akafanya uchunguzi na ikaonekana katibu alificha nyaraka za matibabu ya Niyonzima ziliposilishwa kwake.

Alitaka Niyonzima afukuzwe, lakini tatizo hili lilimalizwa na mwenyeki huku akimuondoa Tiboroha na kumrejesha Haruna, naye amejibu kwa kiwango cha aina yake. Manji alifanya kazi yake kama bosi wa timu.

KUREJEA KWA HARUNA NIYONZIMA

Baada ya kuepuka kutupiwa virago, Haruna aliwaomba msamaha wapenzi na wanachama wa Yanga, kocha wake Hans na wachezaji wenzake wakampokea kwa moyo mkunjufu. Urejeo wake ulikuwa kama usajili mpya klabuni na amechangia kwa kiasi kikubwa sana Yanga kutetea ubingwa wao.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here