Home Kitaifa DONALD NGOMA ‘SMG’ YENYE MAGOLI 20 YANGA, MABEKI WANAWEZA KUMZIMA HIVI…

DONALD NGOMA ‘SMG’ YENYE MAGOLI 20 YANGA, MABEKI WANAWEZA KUMZIMA HIVI…

3860
0
SHARE
Donald Ngoma wa Yanga (kulia) akikimbia na mpira kumuacha beki wa Simba Hassan Isihaka
Donald Ngoma wa Yanga (kulia) akikimbia na mpira kumuacha beki wa Simba Hassan Isihaka
Donald Ngoma wa Yanga (kulia) akikimbia na mpira kumuacha beki wa Simba Hassan Isihaka wakati wa mchezo wa VPL raundi ya kwanza msimu wa2015-16

Na Baraka Mbolembole

Nimekuwa nikisema, na ninarudia tena kusema kwamba, Kitu kikiwa kizuri huleta furaha ya siku zote katika maisha. Thamani ya kitu kizuri ni shida sana kushuka chini kwa sababu ya ubora wake. Kitu kizuri hakitoki nje kikajitembeza kwa watu, lakini watu wana kawaida ya kwenda kukitazama hata kama kina hali ya namna gani, kitu kama hicho hutakiwa na watu kadha wa kadha. Watu hukipa sifa kubwa kitu hicho kisha hutaka kwenda kukizuru, ila kila kitu kizuri kina maisha ya milele.

Namaanisha ‘shujaa huyu mmojawapo wa Yanga’

Si rahisi kuzoea mazingira ya eneo jingine ambalo hukuwapo awali, lakini katika mazingira ya sasa mshambulizi wa Yanga SC, Donald Ngoma ameweza kuzoeana haraka na wachezaji wenzake na kumudu mfumo wa timu kiuchezaji kama si kuongeza ufanisi zaidi.

Magoli yake 14 katika michezo ya ligi kuu inayoendelea Tanzania Bara, magoli yake manne katika game 6 za klabu bingwa Afrika ‘Ligi ya mabingwa,’ na magoli mengine mawili katika michuano ya kombe la FA yanamfanya mshambulizi huyo wa Zimbabwe ‘kufukia’ kila tarajio baya la kushindwa kufanya vizuri nchini ambalo wengi ‘tulilijenga’ mara baada ya mchezaji huyo kulambwa kadi nyekundu katika mchezo wake wa kwanza akiwa mchezaji wa Yanga.

Julai 18, 2015 katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Cecafa Kagame Cup (klabu Afrika Mashariki na Kati) kati ya Yanga na Gor Mahia FC ya Kenya, Ngoma alitolewa uwanjani kwa kadi mbili za njano baada ya kuonekana kushindwa kuzuia hasira zake kufuatia ‘uchezaji wa kisumbufu’ kutoka kwa walinzi wa Gor katika game hiyo ambayo Yanga walipoteza kwa kichapo cha 2-1.

Baada ya mchezo kumalizika wengi tulimlaumu mshambuliaji huyo na kusema kama atakuwa na mwenendo huo atashindwa kupata mafanikio kwa sababu ya uchezaji wa ‘ukamiaji wa mastaa wa kigeni’ unaofanywa na walinzi wa klabu za VPL.

‘Tulijidanganya wenyewe’ kwani mchezo wake wa pili tu na wa kwanza kuikabili timu ya Tanzania akafunga goli wakati alipoisaidia timu yake kushinda 2-0 dhidi ya KMKM, Julai 24, 2015. Mchezo wake wa kwanza katika VPL akafunga goli na kuisaidia Yanga kushinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, Septemba 13, 2015.

Akaonekana kama anabahatisha vile. Akafunga tena na tena wakati Yanga iliposhinda mfululuzo na hadi kufikia mzunguko wa kumi wa VPL, Mzimbabwe huyo alikuwa amekwishathibitisha ubora wake uwanjani.

Amejibadilisha yeye mwenyewe kutoka katika ‘mwonekano wa kupaniki mchezoni  ‘ hadi kuwa mshambulizi hatari zaidi kwa mabeki katika VPL, huku ‘akicheza kwa tabasamu’ hata anapochezewa faulo zisizo za kiungwana.

Amekuwa na bahati njema zaidi katika msimu wake wa kwanza kama mchezaji wa Yanga-ni bahati kwa Yanga na kwa mchezaji mwenyewe ambaye aliichagua Yanga kama sehemu yake ya kwanza alipoamua kuvuka mipaka ya kwao na kusaka mafanikio mahala kwingine.

Mungu amemsaidia amekosa majeraha na jambo limemchochea kuwa na kiwango cha juu kila mechi huku akitafuta mbinu mpya za kuwamaliza walinzi ‘wakamiaji.’ Goli lake dhidi ya Mtibwa Sugar katika game ya mzunguko wa kwanza ilidhihirisha namna mshambulizi huyo alivyo na uvumilivu mchezoni.

Walinzi, Vicest Andrew na Salim Mbonde walijitahidi kucheza kwa mbinu zao zote lakini mwishoni wakajikuta wao wenyewe ‘wakipaniki’ na kumpa nafasi mshambulizi kufunga na kuisaidia Yanga kuishinda Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009 katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Mtibwa ilichapwa 2-0 goli la pili lilifungwa na Malim Busungu.

Kama ningekuwa mlinzi wa timu yoyote ya VPL ningejaribu kutazama zaidi upande wa kushoto ambao mchezaji huyo hugeukia mara baada ya kupokea pasi. Ningejaribu kucheza katika nafasi zaidi na si mwili wa mchezaji huyo kama wanavyocheza walinzi wanayekabiliana naye.

Ngoma anatuonyesha kwa vitendo udhaifu mkubwa wa walinzi wa kati raia wa Tanzania na pengine hata Kelvin Yondan na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub wangeingia katika kundi la ‘walinzi vibonde’  waliopata kumkabili mchezaji huyo wa zamani wa Platinum Stars ya Zimbabwe.

Nimegundua kwamba licha ya walinzi wengi kucheza kwa kukamia, hawana nguvu za kutosha za kushindana na Ngoma ambaye anakimbia kwa ukakamavu hata akiwa bila mpira, sasa basi, kitendo cha kushindana na mwili wake kina matokeo mengi.

Kitendo cha kucheza ‘jino kwa jino’ na mchezaji huyo kama mlinzi atakimudu basi timu itakuwa salama zaidi kwa maana Yanga wanategemea kufunga kupitia mchezaji huyo kwanza ambaye ana kasi, kontroo, nguvu, unyumbulifu, maarifa mengi binafsi na moyo wa kutokata tamaa.

Achana na Mrundi, Amis Tambwe ambaye magoli yake 52 katika misimu yake mitatu VPL yametudhihirishia udhaifu mabeki wetu katika uchezaji wa mpira ya juu-mipira iliyokufa-faulo, kona kwa Ngoma anatuonesha uwezo mdogo wa walinzi wa kati katika usomaji wa mbinu za wapinzani wao. Rejea pambano kati ya Simba na Yanga (mzunguko wa pili msimu katika VPL.)

Abdi Banda alifanya faulo mbili za kufanana baada ya kumparamia mchezaji huyo wa Yanga. Huyo Ngoma licha ya uwezo wake wa kutengeneza faulo zenye madhara kwa wachezaji wa timu pinzani sidhani kama angeweza kutamba kwa stahili hiyo nyakati za kina Amri Said, Geofrey Magori, Gerrard Hillu, John Mwansasu ndiyo maana hata Mark Sirengo alipotangaza kwamba atafunga goli zaidi ya 40 katika ligi kuu bara mwaka 2002, akawa kama amejichochea moto.

Hakumudu kufunga hata goli nane katika ligi iliyokuwa na timu 24 (zikigawanywa katika makundi A na B kisha washindi wanne wa juu katika kila kundi, hufuzu kucheza ligi ya 8 bora.)

Ngoma anaweza kucheza na akili ya mabeki na uelekeo wao wakiwa na mpira ndiyo maana aliwahi pasi ya kurudi nyuma iliyopigwa na Hassan Kessy kwenda kwa golikipa wake, Vicent Aghban.

Huyu si tu ni mfungaji mwingine makini wa kigeni sambamba na Tambwe, Mu-ivory Coast, Kipre Tchetche, Mrundi, Didier Kavumbagu, bali Ngoma ni mshambuliaji wa aina yake ambaye si tu hufunga magoli bali anaweza kutengeneza nafasi nyingi za upatikanaji wa magoli kwa timu yake, huku pia akiwa na uwezo wa kupiga pasi za mwisho.

Magoli yake 20 hadi sasa katika michezo rasmi akiwa na timu ya Yanga, Mzimbabwe huyu ni ‘SMG’ ya hatari ambayo walinzi wa VPL hawataki kukutana nayo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here