Home Kitaifa AZAM FC ‘ITAWAPOTEZA’ ZAIDI SIMBA SC, YOTE HAYA YAMEANZIA HAPA…(Part III)

AZAM FC ‘ITAWAPOTEZA’ ZAIDI SIMBA SC, YOTE HAYA YAMEANZIA HAPA…(Part III)

936
0
SHARE
Said Ndemla (kulia) akijaribu kuzuia krosi ya Shomari Kapombe kwenye mechi ya raundi ya kwanza kati ya Simba dhidi ya Azam

Said Ndemla (kulia) akijaribu kuzuia krosi ya Shomari Kapombe kwenye mechi ya raundi ya kwanza kati ya Simba dhidi ya Azam

Na Baraka Mbolembole

Kama, Poppe ataendelea kubaki klabuni Simba SC kama mmoja wa viongozi waandamizi usitarajie timu hiyo kunyanyuka. Poppe ‘ametengeneza sura’ ya kuwafanya watu waamini kuwa yeye anaisaidia sana klabu lakini kama Aveva angechukua baadhi ya sera za aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika uchanguzi wa klabu Juni, 2014 angeweza kufanikiwa.

Michael Wambura ambaye si tu alikuwa na sifa zaidi za kuwa rais wa klabu hiyo baada ya kumalizika kwa muda wa utawala wa Aden Rage, bali sera yake ya kuifanya Simba ijitegemee kiuchumi, na kuta maendeleo ya ndani ya uwanja na nje ilikuja wakati mwafaka kwani nyakati hizi taasisi, makampuni na mashirika mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakihitaji kuwekeza mitaji mikubwa katika klabu za soka kwa lengo la kujitangaza.

Chini ya Aveva, Simba haina ushawishi wa kuweza kuwavutia wadhamini wapya na pengine hata kampuni ya bia nchini (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro inaweza kuachana na timu mara baada ya kumalizika kwa mkataba wao wa sasa. Kama timu haifanyi vizuri ndani ya uwanja hupunguza mvuto hata kama ni timu kubwa.

Mimi simuhitaji Poppe katika timu, wala sitapendezwa kuona timu hiyo ikiangukia kwa MO. Miaka mitatu iliyopita mmoja wa viongozi wa zamani wa Simba ambaye alikuwapo katika kikosi cha kukumbukwa mwaka 2003 aliniambia kitu fulani ambacho huwezi kuamini.

Aliyekuwa kiongozi wa juu wa klabu hiyo (wakati huo 2003 ) alitaka kuuza game ya marejeano kati ya Zamalek v Simba kwa dau la milioni 500. Kiongozi huyo upande wake alikuwa ameshakubaliana kila kitu na ‘wahongaji’ wake lakini yeye pekee asingeweza kufanikisha ushindi kwa ‘mabwana zake’ hivyo basi akaamfuata kocha James Siang’a ili kumuingiza katika mkumbo huo.

“Tulikuwa katika chumba kimoja pamoja na wachezaji tukizungumza habari za kawaida. Ghafla akaingia (jina nalihifadhi) na kumuomba kocha Siang’a wakazungumze.Mimi pia niliitwa hivyo tulikuwa mimi, kiongozi huyo na mwalimu Siang’a. Tukaenda nje kidogo ya chumba kile tulichokuwa.”

“Akasema, ‘jamani kuna milioni 500 jamaa wanataka kushinda mechi hii.’Kitendo cha kusema hivyo ilikuwa kama amemvuruga kocha. Haraka Siang’a huku akionekana kuwa na hasira akaondoka bila kusema chochote na kurudi katika chumba kile tulimowaacha wachezaji na viongozi wengine. Kocha akaingia na kuwaomba watu wote watulie ili wamsikilize.”

“Akasema kuanzia wakati huo mtu yeyote atakayemuona na (kiongozi huyo) asijihusishe tena katika game hiyo pia akasema tuendelee na maandalizi ya mechi ambayo tulipaswa kucheza kesho yake. Kama si Siang’a, Simba isingefika hatua ya makundi mwaka ule kwani wachezaji waliingia kucheza mechi wakiwa na hamasa kubwa waliyotoka nayo nyumbani baada ya kushinda mechi ya kwanza.”

“Unajua ni kwanini Siang’a aliondoka Simba? Kwanza aliundiwa mizengwe na wazi ilijengeka chuki kati yake na yule kiongozi baada ya kocha kukataa kuuza mechi ile.” Ukiwa mbali si rahisi sana kufahamu mambo kama haya lakini hivi ndivyo mambo yanavyoendeshwa.

Aveva naye amemkumbatia mtu huyo, labda ni kwa kuwa yeye pia alipewa nafasi wakati ule (2003) na kuwa sehemu ya viongozi waandamizi ila ukweli utawala wake umezungukwa na ‘mafionso-yaani Genge la Wahuni.

Watu wanaweza kuwasema vibaya wachezaji wao lakini kama uongozi hauna nidhamu si rahisi kukuta nidhamu hiyo kwa wachezaji.

Matukio ya mlinzi wa pembeni, Hassan Kessy kupigwa na golikipa wa timu yake, Vicent Agban eti kwa sababu Kessy aliondoshwa uwanjani kwa kadi nyekundu katika game dhidi ya Toto Africans siku ya Jumapili iliyopita, kulalamikiwa kuihujumu timu yao kwa mshambulizi kijana Ibrahim Ajib.

Pia kurushiana maneno kunakoripotiwa kutokea kati ya naodha msaidizi, Jonas Mkude, kusimamishwa kwa wachezaji kisha kuvuliwa unahodha kwa beki, Hassan Isihaka na mlinzi, Abdi Banda ni dalili nyingine za wazi kwamba katika timu ya Simba hakuna tena umoja, kuheshimiana, uwajibikaji, upendo na malengo ya pamoja kama timu.

Hii pia ni dalili ya utawala kushindwa kufanya yake vizuri. Adhabu ambazo zilitolewa nyakati tofauti kwa Isihaka na Banda licha ya viongozi kusifiwa kisha kujitangaza kuendelea ‘kuwakomesha’ watovu wote wa nidhamu, mambo yamekuwa hovyo zaidi.

Naweza kumtaja Mzee Hassan Dalali kama mmoja wa viongozi wazuri waliopita katika timu ya Simba. Licha ya kwamba Dalali hakuwa na wapambe wengi wenye pesa katika utawala wake, Mzee huyo aliweza kusimamia maamuzi yake kama mwenyekiti. Ila ni yeye ambaye ninamlaumu kwa kuwa aliwaaminisha sana wanachama wanaomuamini kuamini kuwa Aveva alikuwa mtu sahihi na si Wambura.

Jambo ambalo linawagharimu Simba hivi sasa limetokana na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa klabu, 2014, Wakili, Dr. Damas Ndumbaro kuliondoa jina la Wambura kwa kigezo kwamba katiba ya klabu inamkataa wakati haikuwa kweli.

Hiyo ilikuwa njia ya kwanza muhimu ya kumpeleka madarakani Aveva kama rais wa klabu kwa kuwa kamwe Wambura asingeangushwa na mtu asiye na uzoefu kiutawala katika chaguzi ile. Wakaamua kwa njia zao wenyewe kujipeleka madarakani lakini miaka yao miwili ya kwanza imekuwa ‘migumu kupita vile walivyotarajia hata wao wenyewe.’

Nimesikia kuwa Mkude ameamua kutangaza mwenyewe kwamba ataachana na timu hiyo kama hawatashinda ubingwa msimu huu. Mimi nadhani aende tu kwani hajawahi kuonesha nia ya kushinda VPL akiwa Simba.

Labda kuondoka kwake itakuwa njia mojawapo ya timu kuanza kufanikiwa. Ramadhani Singano, Haroun Chanongo, Miraj Athuman, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Edward Christopher, William Lucian, Hassan Khatib, Wilbert Mweta ni baadhi ya vijana ambao tayari wapo nje ya timu ambayo waliipenda na kuitumikia kwa moyo mmoja, walikuwa pamoja kama timu ya ushindi lakini walipopatwa na majeraha hata yale madogomadogo walitengwa na uongozi ukawa ukiwatazama kama ‘mizigo’ isiyo na faida kwao.

Tafadhali msomaji wangu naomba tuendelee kuwa pamoja hadi mwisho wa makala haya. Kwanini MO si mtu sahihi wa kuimiliki Simba? Kwanini kundi kubwa la wachezaji waliokuwa kikosi cha kwanza msimu huu wanaondoka?

Endelea kuwa nami katika sehemu ya nne siku ya kesho panapo majaliwa. Asante

NB: Kwa ukaribu zaidi unaweza ku-LIKE Page yangu BSports tukajuzana mambo ya mpira kama hapa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here