Home Ligi EPL TIMU YA MSIMU YA LIGI KUU YA UINGEREZA KULINGANA YA NICASIUS AGWANDA...

TIMU YA MSIMU YA LIGI KUU YA UINGEREZA KULINGANA YA NICASIUS AGWANDA (COUTINHO SUSO)

1001
0
SHARE

plMawazo na imani za watu wengi zimepishana sana kwa wakati huu kila mtu akifikiri na kuwaza lake linalomfaa. Kuna wasiohitaji Leicester atwae ubingwa, kuna wale wasioamini nafasi vilabu vyao vilipo na kuna wale waliokata tamaa na kinachoendelea kutokea. Lakini wote wanabaki kuwa watizamaji wa ligi pendwa ya Uingereza.

Wachambuzi wengi watakuwa tayari kutoa vikosi vyao vya msimu baada ya kumalizika kwa mechi za mwisho pengine na kutaja wachezaji wao bora mpaka wakati huo. Lakini sijaona haja ya kusubiri hayo yote, na mpaka kufikia hapa nawaletea wasomaji wa tovuti pendwa ya http://shaffihdauda.co.tz/ kikosi changu bora mpaka sasa.

NICASIUS EPL TEAM OF THE SEASON

NI

GOLIKIPA 

Wengi wangeweza kumtamani David De Gea lakini kwa upande wangu pamoja na ubora wake bado timu yake kwa ujumla imeendelea kumwangusha kwa namna ambavyo imekuwa ikipata matokeo pamoja na juhudi zake kubwa. Hivyo huku makipa kama Adrian, Kasper Schmeichel na Jack Butland wakiwa nao wanafaa, bado golikipa Hugo Lorris amekuwa kiongozi bora wa klabu ya Tottenham na pia kawa muhimili mkubwa wa kuikoa klabu yake katika nyakati ngumu.

MABEKI

HECTOR BELLERIN

Kuna mengi ya kuandika juu yake lakini sijui kama Arsene Wenger ataendelea kuwa naye ukizingatia maisha ya Alves yanavyoelekea ukingoni pale Barcelona. Hakuna beki wa kulia aliyekuwa na mwendelezo bora wa kiwango hata timu yake inapofanya vibaya zaidi ya huyu.

AARON CRESSWELL

Pengine jina la Danny Rose wa Tottenham lingeweza kuja kichwani, lakini muda mwingi Mauricio Pochettino amekuwa akimbadili na Davies katika upande huo hivyo hakidhi moja kwa moja. Nacho Monreal naye ni mchezaji sahihi sana kuwepo hapo lakini bado kura yangu nampa Aaron Cresswell. Amekuwa moja ya mihimili mikubwa sana ya West Ham msimu huu.

TOBY ALDERWEIRELD

Kiwango bora cha mchezaji huyu kimewachagiza sana Tottenham kuwa hapo walipo. Amekuwa nguzo imara hata alipoumia Jan Vertonghen, na huwezi kuwa na maneno mengi kusema dhidi yake. Amekuwa kisiki kikubwa sana.

ROBERT HUTH

Watu wengi wanaweza kuwa hawamkumbuki vyema mchezaji huyu ama wengi walipata kumtizama vyema akiwa Stoke City lakini ukweli ni kuwa anarudisha fadhila kwa baba yake Claudio Ranieri. Huyu ndiye aliyemleta kwenye picha ya soka la ulaya pale darajani Chelsea akiwa na umri wa miaka 17 tu. Na kama Leicester watatwaa ubingwa basi uzoefu wake akiwa moja ya wachezaji waliotwaa ubingwa wa Uingerez chini ya Mourinho mara mbili utakuwa umechangia kwa kiasi kikubwa. Napenda kumwita jabali.

KIUNGO.

N’GOLO KANTE.

Hapa sihitaji kusema mengi. Kiungo wangu bora kabisa wa eneo la ukabaji kwa sasa. Mchezaji asiyetaka kelele na anayefurahi kufanya kazi za punda (donkey jobs). Pengine Makelele amerudi uwanjani kupitia jina hili na sura hii. Ukitafuta sababu tatu za kwanini Leicester wapo pale walipo basi katika mbili za mwanzo, mojawapo ni huyu kijana.

RIYAD MAHREZ (KULIA)

Kiungo mbunifu wa kisasa kabisa. Huyu ndo haswaa aliyeikimbiza Leicester mpaka kufikia hapo walipo. Anafunga magoli sahihi sana huku pia akiwa hajakaukiwa pasi za mwisho miguuni kwake. Kayafanya maisha ya Leicester katika eneo la ushambuliaji kuwa mazuri na yenye starehe ndani yake.

DIMITRI PAYET (KUSHOTO)

Nilitamani Delle Alli awepo ndani ya uwanja akiwa pamoja na Kante katika dimba lakini nafasi ni chache na binafsi sioni sababu ya kutokuwepo Payet mbele ya Alli. Payet ndio West Ham na West Ham ni Payet. Hizi ni moja ya sababu unazoweza kujiuliza kama Wenger ni mtu mwenye akili zaidi duniani au asiyekuwa mwerevu zaidi, maana aliwahi kumtaka. West Ham ilitetereka baada ya kuumia kwake lakini karejea kwa kishindo kikubwa. Bahati nzuri uwepo wake kikosini unanipa nafasi ya kuwa na mpigaji mzuri wa mipira iliyokufa.

MESUT OZIL (SHIMONI)

Madrid wanateseka na Isco kisha James Rodriguez lakini ukweli unaofinya mioyo yao mingi ni kuwa wanaweza wasipate mchezaji anayeweza kukuletea sahani yenye mabao kama huyu. Binafsi huwa naamini macho yake hayaoni vizuri kwani Mungu aliamua kuongeza makali ya mboni zake katika miguu yake. Akiwa na watu sahihi miguu yake ni nadra kuipata katika kiwanja cha mpira. Ile miguu inayoweza kupenyeza mpira kwenye ukuta wa chuma na bado ukamfikia mlengwa. Christian Eriksen angeweza kuketi hapa, lakini huna sababu za msingi kumwondoa mtu huyu.

WASHAMBULIAJI

JAMIE VARDY

Umeuona wapi roho ngumu kama hii tangu Wayne Rooney atundike daruga la ushambuliaji bora na kuamua kuwa mshambuliaji wa kawaida. Anaweza asiwe amebarikiwa kipaji kikubwa lakini nia, nguvu na ufungaji wake vinamtosha kuwa hapo.

HARRY KANE

Huna sababu ya kuwazuia Waingereza kumlinganisha na mshambuliaji yoyote nje ya Suarez, Messi, Ronaldo na pengine Lewandowski. Ameendelea kuthibitisha kuwa ni bora na msimu uliopita hakubahatisha. Bahati nzuri umri wake unamruhusu kuja kuwa bora zaidi na kuendelea kujifunza. Kwa umri wake naamini ni Neymar peke yake ambaye angeweza kuwa hatari mbele ya goli kumzidi.

SUBS. De Gea, Dier, Drinkwater, Dembele, Lukaku, Eriksen, Delle Alli.

MCHEZAJI BORA WA MSIMU.

RIYAD MAHREZ.

Natamani kumuweka Harry Kane lakini, Riyad Mahrez amekuwa mchezaji mwenye msimu bora zaidi. Ukitizama namna alivyomaliza msimu uliopita na wapi timu yake ilikuwepo ni dhahiri kuwa amekuwa na mabadiliko makubwa sana, na uwezo wake wa kufunga na kutoa pasi nyingi za mabao unanifanya nimnyime Harry Kane tuzo hii anayostahili.

MCHEZAJI BORA CHIPUKIZI

HARRY KANE

Mashabiki wa Liverpool lazima wanang’ata meno kwanini uongozi wao haukumsajili Delle Alli wakati anahitaji kujiunga nao kabla ya kutua Tottenham. Mchezaji huyu kwa umri wake anakupa imani kuwa atakuja kuwa bora sana. Natamani ndiye ambaye angetwaa tuzo hii lakini namrudishia Harry Kane ambaye aliishinda msimu uliopita. Ubora wake na magoli yake unampa kiburi kikubwa Pochetino.

NAKUNG’ATA SIKIO KATIKI HILI.

Tangu msimu wa mwaka 2011/12 ni msimu wa mwaka 2013/2014 pekee ambapo tuzo hii haikwenda kwa mchezaji ambaye anacheza nje ya Tottenham. Washindi walikuwa Kyle Walker, Gareth Bale, Eden Hazard kisha Harry Kane.

Na katika washindi 23 wa tuzo hii katika historia ya ligi kuu ya Uingereza 15 wamekuwa raia wa Uingereza.

TOA MAONI YAKO PIA HAPA CHINI

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here