Home Kitaifa VAN PLUIJM: ‘CHA KWANZA NI KUFUNGA, CHA PILI, HAWATAKIWI KUPATA GOLI, MAMBO...

VAN PLUIJM: ‘CHA KWANZA NI KUFUNGA, CHA PILI, HAWATAKIWI KUPATA GOLI, MAMBO HAYA YATATUBEBA’

573
0
SHARE
Hans van der Pluijm, kocha mkuu wa club ya Yanga SC
Hans van der Pluijm, kocha mkuu wa club ya Yanga SC
Hans van der Pluijm, kocha mkuu Yanga SC

Na Baraka Mbolembole

“Tumejiandaa ipasavyo kwa wiki nzima na kila mchezaji yuko katika hali nzuri ya kukabiliana na Al Ahly. Ni timu ambayo ni imara na ni changamoto kwetu na ni nafasi ya kuonesha kile ambacho wachezaji wetu wanacho.“

“Katika mpira kila  kitu kinawezekana na hakuna kisichoshindikana. Morali katika ‘camp’ ilikuwa juu.” ni maneno ya kocha Hans Van der Pluijm wakati nilipomuuliza kuhusu mtazamo wake kuekekea mechi ya kesho Jumamosi kati ya timu yake ya Yanga SC dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Yanga itashuka uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwakabili mabingwa hao mara nyingi wa michuano hiyo (mabingwa mara 8) katika mchezo ambao wengi wanataraji kuona wakicheza mchezo wa kushambulia.

TELELA ACHUKUE NAFASI YA NIYONZIMA, MBUYU ACHEZE NAMBA 6

Kukosekana kwa kiungo-mchezesha timu, Haruna Niyonzima kunaweza kupunguza ufanisi katika idara ya kiungo ambao Niyonzima ametengeneza ushirikiano ‘bab-kubwa’ na Thaban Kamusoko.

Salum Telela alicheza vizuri katika game ya ushindi dhidi ya Kagera Sugar wiki iliyopita nadhani anafaa kuanza mahali kwa Niyonzima na hivyo kumnyima nafasi kiungo mshambulizi wa pembeni, Saimon Msuva.

Mbuyu Twite ni mzuri katika kuzuia na kupandisha timu haraka akicheza kama kiungo-namba 6. Kama, Mbuyu, Kamusoko na Telela wataanza mechi kwa pamoja Yanga watakuwa na lengo zaidi la kushambulia kwa sababu, Deus Kaseke, Amis Tambwe na Donald Ngoma wataanza kama washambuliaji watatu katika mfumo wa 4-3-3.

AL AHLY WALISHINDA 5-3 JUMAPILI ILIYOPITA

Katika michezo 22 waliyokwisha cheza katika ligi kuu ya Misri kikosi cha kocha Martin Jol kimepoteza mara mbili tu huku kikiongoza msimamo kwa alama 9 zaidi ya wapinzani na mahasimu wao Zamalek. Al Ahly wamekuja kucheza na Yanga huku pia mabingwa hao wa VPL wakiwa wamecheza michezo 22 katika ligi na kupoteza mara moja tu.

Kwa maana hiyo timu zote mbili zinakutana zikiwa zimecheza michezo 22 katika ligi zao kuu lakini Yanga licha ya kuwa alama nne nyuma ya vinara wa VPL, timu ya Simba SC imekusanya alama 3 zaidi ya Al Ahly ambayo imekusanya alama 50 katika ligi kuu ya Misri.

Jol alishuhudia timu yake ikifunga magoli manne ndani ya dakika 45′ siku ya Jumapili iliyopita, lakini El Shorta iliyo nafasi ya 3 kutoka mkiani pia ikitingisha nyavu zao mara 3 katika pambano lao la mwisho kucheza katika ligi kuu ya Misri.

Momen Zakaria alifunga goli lao la kuongoza dakika ya 18′, mlinzi-wing mzoefu, Ahmed Fathy akaongeza lingine dakika tano baadaye. Mlinzi wa Shorta, Mohamed Abdi alijifunga dakika ya 45′ baada ya kushambuliwa mno, dakika hiyohiyo ya 45′, Fathy akafunga tena na kufanya matokeo kuwa Shorta 0-4 Al Ahly.

Timu hiyo dhaifu katika ligi ya Misri ikapata goli la kwanza dakika ya mwisho kabla ya filimbi ya mapumziko na kufikia dakika ya 58′ matokeo yalikuwa Shorta 3-4 Al Ahly. Matokeo hayo ya mwisho si kipimo cha ubora wa Al Ahly katika game dhidi ya Yanga lakini yanamaanisha kuwa Waarabu hao wanafungika wanaposhambuliwa lakini pia ni hatari kwa kufunga magoli ya harakaharaka.

ANACHOAMINI HANS VAN DER PLUIJM

Nilimuuliza Hans ataichezesha timu yake katika mtindo wa kushambulia au ataihofia  Al Ahly kutokana na ubora wake, pia nilitaka kufahamu ni mfumo gani hasa atautumia katika mchezo huo wa nyumbani.

“Sikiliza rafiki, katika mchezo cha kwanza ni kufunga kama unahitaji matokeo mazuri katika ardhi ya nyumbani. Cha pili, hawatakiwi kupata goli. Hii ndiyo kanuni ya mchezo. Mfumo hauchezi mpira, ila ni wepesi, ufundi, mbinu, kujitambua na nidhamu za kimchezo ndizo zinaweza kuleta matokeo yale tunayohitaji.“

“Kama unavyojua mpira ni mchezo wa makosa, atakayefanya makosa machache ana nafasi kubwa ya kuibuka mshindi. Huo ndiyo mpira. Utakuwa ni mchezo mgumu lakini tukiwa na hali nzuri ya upambanaji kila kitu kinawezekana.” ananijibu Hans wakati nilipofanya nae mahojiano kwa njia ya mtandao siku ya Ijumaa.

VIUNGO AL AHLY NI TATIZO KULIKO WASHAMBULIAJI

Makosa makubwa pekee ambayo nafikiri Yanga wanapaswa kuyapunguza ni kukubali mashambulizi mfululizo na kucheza faulo katika robo yao ya kwanza ya uwanja. Al Ahly inataraji kumpanga mshambulizi mmoja kijana, Amir Gamal lakini wana viungo hatari katika ufungaji.

Mkongwe, Hossam Ghaly, Zakaria na kijana mwenye miaka 18, Ramadan Sobhi ni kati ya wachezaji wa kuchungwa sana. Sobhi anatajwa kuwa Abou Trika mpya katika soka la Misri amefunga magoli matatu,

Zakaria amefunga mara 6 na mtu hatari zaidi ni mkongwe, Abdalla El Said amefunga jumla ya magoli 7 kwa maana hiyo viungo watatu wa Al Ahly wamefunga magoli 16.

Kamusoko tayari amefunga magoli nane katika michuano yote, sawa na Msuva na goli moja la Mbuyu Twite linatengeneza idadi ya magoli 17 yaliyofunngwa na viungo hao watatu wa Yanga.

Washambuliaji watatu wa Al Ahly ( Evouna, Amir Gamal na mkongwe, Emad Moteab) wamefunga jumla ya magoli 14, wakati wale wa Yanga, Donald Ngoma, Amis Tambwe na Deus Kaseke wamefunga jumla ya magoli 37 katika michuano yote.

Yanga wana nafasi kubwa ya kushinda game ya Jumamosi. Mungu ibariki, Yanga, Mungu ibariki Tanzania.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here