Home Kitaifa MBEYA CITY VS COASTAL UNION: VITA YA KUFA AU KUPONA ZAIDI YA...

MBEYA CITY VS COASTAL UNION: VITA YA KUFA AU KUPONA ZAIDI YA SIMBA, YANGA, AZAM, KUWANIA UBINGWA

605
0
SHARE

Mbeya City-kikosi

Baada ya kusimama kwa muda kupisha mechi za kimataifa, ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara leo April 2 itaendelea kwa michezo miwili kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya kati ya Mbeya City dhidi ya Coastal Union wakati mchezo mwingine utakuwa kwa wachimba Almasi ndani ya Mwadui Complex kati ya wenyeji Mwadui FC dhidi ya Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro.

Mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Coastal Union unatazamwa kuwa ni wakufa au kupona kwa timu zote mbili kutokana na sababu nyingi za kimchezo hasa katika kipindi hiki ambacho timu hizo zimesaliwa na michezo sita tu (kabla ya mchezo wa leo) zimalize michezo yao kwenye ligi wakati huo timu zote zikiwa hazina uhakika wa kuwepo kwenye ligi kwa msimu ujao.

Nafasi zilizopo timu hizo kwenye ligi

Mbeya City FC

Wagonga nyundo hao wa jiji la Mbeya wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 24. Mbeya City imeshacheza mechi 24 na kufanikiwa kushinda michezo 6 pekee, imetoka sare mara 6 na kupigwa mwenye mechi 12 msimu huu. City tayari imefungwa magoli 33 huku yenyewe ikiwa imefunga magoli 23 na kutengeneza wastani wa magoli ya kufungwa na kufunga kuwa -10.

Mbeya City ipo nafasi  4 juu ya timu inayoburuza mkia (Coastal Union) kwa tofauti ya pointi 5 tu hali inayohatarisha pia nafasi ya Mbeya City kusalia kwenye ligi kwa msimu ujao 2016-17.

Coastal Union

‘Wagosi wa Kaya’ kutoka jijini Tanga wao ndiyo wanashika nafasi ya mwisho (nafasi ya 16) kwenye msimamo wa ligi na wako hatarini kucheza ligi kuu msimu ujao kama hazitafanyika jitihada za ziada kujikwamua mahali walipo sasa. Timu hiyo imeshacheza michezo 24 pia ikiwa imefanikiwa kupata ushindi mara 4 tu, sare 7 na kuangushiwa vipigo mara 13 na kufanikiwa kupata pointi 19.

Coastal imefungwa jumla ya magoli 30 wakati yenyewe imetupia kambani mago 14 tu na kutengeneza tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kuwa ni -16.

Hatari ya kushuka daraja kwa timu zote mbili.

Msimu huu timu tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi zitaiaga ligi hiyo na kuteremka hadi ligi daraja la kwanza, Coastal Union ipo kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja kutokana na nafasi iliyopo sasa pamoja na hali ya timu yao. Wachezaji wa timu hii walishawahi kugoma wakidai malimbikizo ya mishahara yao pamoja na posho. Lakini kwa sasa kuna ‘mvurugano’ kwenye uongozi wa timu hii kiasi cha kukosekana kwa umoja na ushirikiano ndani ya timu.

Inaonekana hakuna mipango thabiti ya kuinusuru timu kushuka daraja huku baadhi ya watu wakiwa wamesusia na kujiweka pembeni wakushuhudia kinachoendelea kwa sasa.

Mbeya City wao mambo yao kidogo ni tofauti na Coastal, wao wamekuwa hawapati matokeo mazuri kwasababu nyingi za uwanjani. Kuondokewa na nyota wao wengi kwa wakati mmoja kumeifanya timu yao kuyumba sana, Peter Mwalyanzi, Deus Kaseke na Paul Nonga ni baadhi ya mihimili iliyoondoka wakati timu ikiwa haijapata mbadala wao.

Kuondokewa na makocha wao

Makocha wa timu hizi mbili ambao walianza msimu huu wa ligi na timu waliondoka kwa nyakati tofauti na kuziacha timu zao baada ya kupata ofa kwenye vilabu vikongwe vya Simba na Yanga.

Juma Mwambusi alipata deal jipya ndani ya Yanga kama kocha wa kumsaidia Hans van Pluijm baada ya Mkwasa kukabidhiwa timu ya taifa.

Kocha wa sasa wa Simba Jackson Mayanja yeye alikuwa Coastal Union kabla ya kutimkia Msimbazi ambako anafanya vizuri baada ya Dylan Kerr kufunguliwa mlango wa kutokea na wekundu wa Msimbazi.

Tangu kuondoka kwa makocha hao kwenye timu zao, mambo yamezidi kuwa mabaya kwenye timu hizo na kupelekea kukaa kwenye kuti kavu la VPL.

Kitu gani kinaufanya mchezo wa Mbeya  Civy vs Coastal Union kuwa mkalili?

Hali halisi ya kutaka kukwepa mkasi wa kushuka daraja utaufanya mchezo huu kuwa mkali kutokana na kila timu kutaka pointi 3 kutoka kwa mpinzani wake ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusalia kwenye ligi msimu ujao. Kukubali kichapo ni kuendelea kujichimbia kaburi wakati idadi ya mechi inazidi kupungua kila kukicha.

Kila timu itahitaji pointi tatu kwenye mchezo wa leo, kila timu inatambua ikishinda mchezo wa leo itasogea juu kutoka ilipo. Endapo Mbeya City itapata pointi tatu itakuwa imefikisha pointi 27 sawa na Majimaji ambayo ipo nafasi ya 8, Mbeya City itakaa juu ya Majimaji kutokana na wastani wa magoli. Kama Coastal Union itashinda itafikisha pointi 21 sawa na JKT Ruvu ambayo inashika nafasi ya 14 hivyo wastani wa magoli utaamua timu ipi ikae juu ya mwenzie.

Ikitokea timu zote zimetoka sare, zitajiongezea pointi moja kila timu. Coastal itafikisha pointi 20 sawa na African Sports, kutokana na wastani wa magoli, Coastal itasogea kwa nafasi moja hadi nafasi ya 15 wakati huo Sports wakishuka hadi mkiani. Matokeo ya sare yataifanya City kufikisha pointi 25 sawa na Ndanda FC na Kagera Sugar lakini City watasalia kwenye nafasi yao kutokna na wastani wa magoli ya kufunga na kufungwa.

Mbeya City vs Coastal Union head to head

Kwenye michzo mitano iliyopita ya timu hizi, kila timu imeshinda mchezo mmoja huku zikitoka sare kwenye michezo mingine mitatu.

02/04/2016 Mbeya City vs Coastal Union??

31/10/2015 Coastal Union 1-1 Mbeya City

15/02/2015 Coastal Union 0-0 Mbeya City

27/09/2014 Mbeya City 1-0 Coastal Union

22/02/2014 Coastal Union 2-0 Mbeya City

28/09/2013 Mbeya City 1-0 Coastal Union

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here