Home Kitaifa STEVEN MAZANDA, KIUNGO FUNDI ANAYESUMBULIWA NA ‘PEPO MBAYA’

STEVEN MAZANDA, KIUNGO FUNDI ANAYESUMBULIWA NA ‘PEPO MBAYA’

984
0
SHARE
Steven Mazanda-Kiungo wa Mbeya City FC (Picha nawww.mbeyacityfc.com)
Steven Mazanda-Kiungo wa Mbeya City FC (Picha nawww.mbeyacityfc.com)
Steven Mazanda-Kiungo wa Mbeya City FC (Picha na www.mbeyacityfc.com)

Na Baraka Mbolembole

Moja kati ya vipaji ambavyo Wajerumani walitegemea kingekuja kuipaisha nchi yao katika soka ni kiungo wa pembeni, Sebastian Deisler. Alitajwa kama kipaji cha karne mpya lakini majeraha yalimaliza mchezaji huyo akiwa na miaka 27 tu akatangaza kustaafu soka jambo ambalo liliwaumiza sana Wajerumani.

Aliichezea timu yake ya Taifa michezo 33 tu na kufunga magoli matatu kati ya mwaka 2000 hadi 2006, lakini hapa sitazungumzia kuhusu mchezaji huyo wa zamani wa Borussia Monchengladbach, Hertha Berlin na FC Bayern Munich bali nitamzungumzia zaidi mmoja wa wachezaji bora ambao nimepata kuwashuhudia nchini.

Bila shaka wengi wetu watakuwa wanamfahamu kiungo ‘maestro’ Steven Mazanda. Kwa mara ya kwanza nilimuona Mazanda pale Morogoro mwaka 2006 akiwa na kikosi cha Moro United chini ya mkufunzi Abdallah ‘King’ Kibadeni.

Moro United ilikuwa imekimbiwa na wachezaji wengi kutokana na ukata ulikuwapo katika timu hiyo lakini kundi la wachezaji ‘watiifu na wavumilivu’ wasiozidi 15 walibaki klabuni ili kumalizia msimu wa mwaka 2006. Nilikuwa na miaka 20 wakati huo na nilikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza katika timu yangu ya Jamaica FC.

Polisi Morogoro, Jamaica na timu ya vijana iliyokuwa chini ya marehemu Yahya Berlin wote tulikuwa tukifanya mazoezi yetu katika uwanja wa shule ya sekondari ya Morogoro hivyo Moro United walikuwa wakiomba kwa muda mfupi tu kufanya mazoezi katika uwanja huo.

Kila walipokuwa wakimaliza mazoezi ya timu yao wachezaji, Boniface Pawassa, Shekhan Rashid, Mazanda, Mcongo, Pitcho Nkongo na Idrissa Rajab walikuwa wakijiunga nasi na kufanya pia mazoezi na sisi.

Ni hapo ndipo kwa mara ya kwanza nilicheza na Mazanda na kutokea kumkubali sana kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga pasi safi akiichezesha timu. Nilipendezwa naye sana na kujiweka karibu yake.

Mazanda alikuwa akifanya mazoezi ya nguvu na hakuwa mtu wa masihara katika mazoezi. Baada ya msimu kumalizika sikupata tena nafasi ya kucheza kando ya mchezaji huyo, na kwa wakati huo (2006) sikuwahi kumdadisi kujua historia yake kiuchezaji hadi nilipofanikiwa kumpata na kufanya naye interview hii ndefu ambayo kwa kweli inasikitisha kwa msimuliwa na kukatisha tamaa msimuliaji ambaye ni Mazanda mwenye.

Kwanza nilitaka kujua, Huyu Steven Mazanda alitokea wapi hadi nilipokutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 2006.

“Kipindi hicho Steven Mazanda alikuwa ametokea timu ya Kahama United.” anaanza kuniambia Mazanda ” Nilianza kucheza ligi kuu nikiwa na miaka 18 katika timu ya Tukuyu Stars ‘Banyambala’ mwaka 2002. Nakumbuka kipindi hicho kuna mashabiki wa Tukuyu walinifuata nyumbani na kuniomba nikasaini kuichezea timu yao. Kocha wangu wa kwanza blikuwa ni Athumani Juma Kalomba na mwalimu Juma Mwambusi.” anasema Mazanda.

Tukuyu Stars ilikuwa timu maarufu sana nchini wakati huo Mazanda akisajiliwa, pia ndiyo timu iliyokuwa na mashabiki wengi mkoani Mbeya zaidi ya Tanzania Prisons.”Nilikutana na changamoto nyingi baada ya kusajiliwa katika timu hiyo nikiwa kijana mdogo. Lakini siku zote changamoto huwezi kuzikwepa katika maisha cha muhimu ni kupambana nazo. Mazoezi yalikuwa magumu, lakini nilikubali hali hiyo nb nikafanikiwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.”

“Nilivutiwa na kaka zangu niliowakuta katika timu kwa sababu walitokea kuniamini sana. Lakini nilichukizwa siku za mwanzo na namna wachezaji niliowakuta katika nafasi nayocheza kwa sababu hawakupendezwa na uwepo wangu katika timu kwa kuwa niliingia moja kwa moja katika timu ya kwanza”, anasema Mazanda ambaye alichezea Tukuyu hadi mwaka 2004 alipojiunga na Kahama United ya Kahama.

“Nilicheza Tukuyu kwa misimu miwili na kujiunga na Kahama United, niliondoka Tukuyu ili kujitafutia riziki mahali pengine kwa kuwa katika timu yangu ya kwanza nilikuwa nikicheza bure-namaanisha sikupata kitu.”

Baada ya msimu mmoja katika timu ya Kahama United, Mazanda alijiunga na Moro United wakati huo ikitamba kama ‘Chelsea ya Bongo’ na kucheza kwa misimu miwili. Mazanda kwa mara ya kwanza alivunjika mguu mwaka 2007 wakati akiitumikia timu ya mkoa wa Mbeya wakati alipopata nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya FC Lupopo ya DR Congo.

“Niliumia sehemu ya kifundo changu cha mguu ‘ankle’ na katika kufanya tiba, kaka yangu ambaye namuheshimu sana akajitolea pesa yake mfukoni kunipeleka hospitali ya Agha Khan na kulazimika kukubali kuchomwa sindano, lakini ni sindano zile ndizo zikaniletea matatizo makubwa zaidi kwani kifundo changu cha mguu kikaanza kukua na kuwa kikubwa.”

“Nilikaa nje ya uwanja kwa muda kidogo na nikajiunga na Tanzania Prisons katika mazoezi yao. Wakati naendelea na mazoezi pale Prisons nikapigiwa simu na mtu mmoja ambaye nilicheza naye Moro United anaitwa Pitchou Kongo, tukasalimiana kisha akaniuliza, uko wapi kwa sasa, nikamjibu nipo kambini na timu yangu ya Prisons, akaniulia tena, ‘unataka kuwa askari?’ nikamjibu, ndio.”

“Akaniambi, ‘sikia Mazanda, Patrick Katalay yupo Lubumbashi na wametuma tiketi mbili, yangu (Mazanda) na yake (Pitchou) maana kipindi hicho (2007) yeye Pitchou alibaki Dar es Salaam. Pitchou na Katalay hawakuwa marafiki zangu ila walitokea kuubali sana ushirikiano wetu katika timu ya Moro.”

“Wakati tunaenda Lubumbashi, Pitcho aliniambia ‘tumekuchukua sababu eneo unalocheza unaweza kutusaidia. Hatukuwa karibu sana nje ya uwanja, ila ndani ya uwanja ulitusaidia sana sisi kama sisi’ akimaanisha yeye na Katalay. Nikamjibu asanteni sana tuko pamoja tuombeane uzima, huku nikijua nina maumivu. Nilirudi Tanzania nikiwa na plasta ngumu (P.O.P) na nikakaa nyumbani kwa miezi miwili.”

“Nilienda Lupopo lakini naweza kusema sikuwa na bahati nayo sababu wakati naenda Lubumbashi nilikuwa tayari nimevunjika mguu nikiichezea timu ya mkoa wa Mbeya. Nawashukuru sana Wa-congo kwani walinifanyia upasuaji lakini ilikuwa kama ‘pepo mbaya’ sikuweza kupona kabisa mpaka nikaamua kurudi Tanzania.  Maumivu yamekuwa kikwazo kikubwa sana kwangu.”

Baada ya kurejea nchini 2007, Mazanda alipumzika kwa muda akijiuguza. Mwaka 2009 akiwa na miaka 26 alijiunga na timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

“Mwaka 2009 nilisaini kuichezea Mtibwa lakini wakati nipo mazoezini katika wiki ya pili ya maandalizi niligongana na mchezaji mwenzangu nikaumia goti. Yakaanza maneno ‘huyu jamaa amezeeka’ na bosi wa timu akasitisha mkataba wangu, nikarudi nyumbani na kukaa msimu mmoja na nusu bila kucheza.”

“Wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu wa 2010/11 nikaitwa na Kagera Sugar nikacheza kwa msimu mmoja na nusu. Baada ya kumaliza mkataba nao mwalimu Mwambusi (Juma) akanipigia simu na kuniambia ‘njoo tusaidiane kuipandisha Mbeya City,’ nikakubali.”

“Lakini katika maandalizi ya mwanzo nakumbuka yalikuwa mazoezi ya asubuhi, wakati naenda kunyang’anya mpira kwa mpinzani wangu, ile nimenyang’anya mpira na kuondoka nao yule mchezaji mwenzangu si akanipiga ‘mkasi,’ nikavunjika enka na kulazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu.”

“Nilipona na kumalizia gemu za mwisho na kuisaidia timu kupanda VPL mwaka 2013. Baada ya timu kupanda, nikacheza na kumaliza mzunguko wa kwanza salama kabisa, lakini wakati naanza maandalizi ya mzungo wa pili ghafla nikahisi maumivu madogomadogo ya misuli, nikaamua kucheza nayo maumivu yale hadi nilipoamua sasa kupumzika ili nipate matibabu.” anamaliza kusema Mazanda ambaye alijiunga na City mwaka 2012 na msimu huu amecheza gemu 7 tu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here