Home Kitaifa MAUMIVU YA HUSSEIN JAVU NA VISA HIVI VYA KISHIRIKINA KATIKA MPIRA WA...

MAUMIVU YA HUSSEIN JAVU NA VISA HIVI VYA KISHIRIKINA KATIKA MPIRA WA TANZANIA

1033
0
SHARE
Hussein Javu-Mshmbuliaji Mtibwa Suager
Hussein Javu-Mshmbuliaji Mtibwa Suager
Hussein Javu-Mshmbuliaji Mtibwa Suager

Na Baraka Mbolembole

WAKATI nacheza mpira katika madaraja ya chini mara kadhaa nilikuwa nikipewa kitu ‘mfano wa hirizi’ na kutakiwa kuiweka katika soksi ama bukta yangu nitakayovaa wakati wa mchezo husika.

Pili nimewahi kupoteza mechi kadhaa za hatua ya robo fainali, nusu fainali kwa njia ya mikwaju ya penalti, kwa kuwa tu kuna wachezaji walipoteza mikwaju yao ya penalti na baadaye kujitetea kwamba walishindwa kufunga kwa sababu ya kuona ‘maruerue’ katika goli.

Kuanzia kwa mashabiki, viongozi hadi kwa benchi la ufundi, katika ngazi ya chini ya mpira wa miguu hapa nchini wanaamini katika ushirikina. Ushirikina ni imani kama ilivyo imani nyingine lakini kwa mwanadamu aliyekamilika hii ni imani ‘potofu’ kuliko zote lakini ina nguvu kubwa ya ushawishi barani Afrika. Sijui sehemu nyingine duniani.

Pamoja na kucheza na mfano wa hirizi kuna michezo tulipoteza hivyo upande wangu sikuwahi kuamini kama ‘uchawi’ unaweza kuleta matokeo bora katika timu ama kwa mchezaji mmojammoja. Pamoja na yote hayo bado imani hii inaendelea kuwanufaisha watu wengi na kuwaumiza vijana wengine wengi wenye vipaji.

“Siku ya kwanza tu nilipoanza mazoezi katika timu ya Kagera Sugar nikaanza kusikia maumivu katika goti langu la mguu wa kulia. Nilichukulia ni maumivu ya kaiwada tu hivyo nikaendelea kukimbia, lakini kadiri nilivyoendelea kukimbia yale maumivu yalizidi, ilikuwa kama sindano hivi inachoma.”

Aliniambia kijana mmoja mwenye kipaji kikubwa ambaye amewahi kuwa nahodha wa timu ya Moro United. Nakumbuka maneno haya aliniambia nikiwa nafanya naye mahojiano akiwa nyumbani kwao mwaka 2011.

“Nilishindwa kuendelea na mazoezi hivyo nikapumzishwa, maumivu yale hayakukoma kila nilipoenda uwanjani kwa ajili ya mazoezi mambo yalikuwa magumu. Kocha Mayanga (Salum) akaniambia nimuone daktari kwa uchunguzi zaidi.”

“Nilipewa dawa za kupunguza maumivu na daktari akaniambia kwamba napaswa kupumzika kwa wiki mbili. Lakini baada ya muda huo, huku nikiwa sina maumivu nilipojiunga na wenzangu tu katika mazoezi, tatizo lile ambalo sikuwahi kuwa nalo likajirudia, tena safari kwa maumivu makali zaidi.”

“Nilishindwa kucheza mechi nyingi za mwanzoni mwa msimu kutokana na maumivu yale. Wakati timu ilipokwenda Turiani, Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar, mimi niliachwa kwa uchunguzi zaidi katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro.

Nilifanyiwa vipimo vya X-ray na madaktari waliona kuna mshipa mkubwa sawa na kidole cha mwisho cha mkono umeota katika goti langu. Hata wao walisema si jambo la kawaida hivyo haraka wakamshauri daktari wa timu yetu kuuangamiza mshipa huyo uliota. Nikaambiwa nifanye kila kitu nachohitaji kabla ya kuchomwa sindano ya matibabu hayo.“

“Nakumbuka baada ya kuchomwa sindano ile goti ‘lliliumuka’ na kujaa mfano wa puto kubwa. Zaidi ya masaa matano nilikuwa katika hali hiyo. Nashukuru Mungu matibabu yalikwenda vizuri na baada ya hapo nilitakiwa kupumzika kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kuanza mazoezi.

Nilikaa nje ya uwanja kwa muda uliotakiwa, na nilichukuliwa picha nyingine za X-ray na ule mshipa haukuonekana. Lakini nilipoanza tu mazoezi, maumivu yale yakarejea na kuwa makali z aidi.“

“Mwalimu, Mayanga akaniambia inatakiwa nikatazame kwa njia nyingine, akimaanisha kwa watatibu wa tiba asilia. Sikuwa nikiamini mambo ya ushirikina licha ya kukutana na vikwazo vingi katika maisha yangu ya mpira, ila kufikia pale nilianza kusadiki ‘kurogwa’ hivyo nikazungumza na uongozi nao ukanipa baraka ya makusudio yangu na kurudi nyumbani.

Anaendelea kusimulia mchezaji huyo ambaye alikuwa kipenzi cha kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars,) Mbrazil, Marcio Maximo.

“Niliporudi nyumbani, baba yangu ambaye pia hasadiki mambo ya ushirikina alianza kunihangaikia, bahati akampata ‘babu mmoja hivi’ ambaye aliponitazama akagundua kwamba nimechezewa na kwa vile nakusimulia huwezi kuamini kama nilivyokuwa siamini mimi.”

“Nilimuona muhusika (akanitajia jina la mchezaji mmoja wa muda mrefu katika timu ya Kagera lakini sasa hayupo katika timu hiyo.) Nilifanyiwa matibabu kisha nikaambiwa naweza kucheza kuanzia kesho yake kama nitahitaji jambo.”

“Sikuamini, lakini kesho yake ilinibidi nichukue vifaa vyangu vya mazoezi na kwenda uwanja wa jirani kujaribu kufanya mazoezi. Sikuwa na maumivu yo yote hivyo nikaamua kufanya maandalizi ya kurudi Bukoba kujiunga na timu.

Ligi ilikuwa imebakiza mchezo mmoja tu kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza hivyo nilitaka kuwahi mechi ya mwisho dhidi ya Coastal Union ambayo ilichezwa Tanga. Nilipoongea na mratibu wa timu, Mohamed Hussein aliniambia kwamba kwa kuwa imebaki mechi moja tu kabla ya ligi kusimama ni vyema nikaendelea kubaki nyumbani hadi wakati wa mzunguko wa pili, lakini sikukubaliana naye na nilimtoa hofu kuwa nipo fiti na nilihitaji kucheza.

“Akanikubalia kishingo upande na kuwezesha safari yangu kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba. Nilipofika kila mtu katika timu alinishangaa kwani sikuwa hata nimetumia wiki mbili kujiuguza nyumbani. Kesho yake nikaenda mazoezini asubuhi nikamuomba mwalimu Mayanga anipigie mpira, katika lugha ya utani akaniambia, ‘Wewe… si mgonjwa umerudi tena’ naye akanipigia mpira nikaupokea na kuufanyia ufundi wangu, akashangaa sana, si yeye tu hadi wachezaji wenzangu pia walishangaa kuniona nimepona.”

“Kocha akaniweka katika programu yake ya mechi ya mwisho dhidi ya Coastal. Nilikuwa na hamu kubwa sana ya kuichezea timu yangu, lakini wakati tunapasha moto misuli kabla ya kuanza kwa mchezo huo, nikaanza kubanwa na kichomi ambacho kilipelekea nishindwe kupumua vizuri.

Nikajikaza hivyo hivyo lakini hali ikawa ngumu. Nikaomba ruhusa kama naenda kujisaidia huko niliazima simu na kumpigia mzee wangu Dar kumuelezea hali yangu wakati huo. Naye akampigia yule simu yule mtaalamu akaniunganisha naye, nikamuelezea namna navyojisikia, akaniambia nirudi uwanjani kuendelea kupasha na kuniambia kwamba hali hiyo itaondoka ndani ya dakika tatu.”

“Kweli ndivyo ilivyokuwa, nikacheza ile mechi vizuri sana kiasi cha kusifiwa na kila mtu katika timu yetu. Kocha Mayanga alinisaini kwa kuwa anafahamu vyema kuhusu uwezo wangu, lakini kwa yule mchezaji mwenzangu ilikuwa ni pigo hivyo akadhamiria kujipanga zaidi wakati wa mzunguko wa pili. Mimi si mtu wa ushirikina hivyo nikaamua kukubali kushindwa na kujiondoa katika timu. Wachezaji wengi wameondoka pale kwa sababu yake.”

Mwaka mmoja baada ya kufanya interview na mchezaji huyo nilibahatika pia kuandika stori kumuhusu mchezaji wa Yanga SC ambaye alikuwa amesajiliwa katikati ya mwaka 2011. Yeye alinieleza jambo lingine linalo maanisha kwamba alikuwa akirogwa na mmoja wa wachezaji wakongwe katika timu hiyo wakati huo.

“Kila nikienda mazoezi ninasikia maumivu makali sana katika kifundo changu cha mguu, lakini nikiwa nje ya timu wala sisikii maumivu yo yote. Tatizo ni (anamtaja jina mchezaji huyo) anataka kucheza yeye tu. Imani yangu inaniambia niendelee kuvumilia kwani yatapita tu haya. Yeye hana muda mrefu wa kucheza hivyo ataondoka na nitapata nafasi inshallah.”

Wachezaji wengi wa Tanzania wanatokea katika soka la mitaani, ni huko ndiko wanapoanza kukutana na vitendo vya kishirikina, inaweza kuwa ni wao wenyewe hujihusisha navyo, makocha au viongozi wa klabu, na wakati mwingine mashabiki wakereketwa wa timu zao.

Hivyo wanakuja kucheza ligi ya juu wakiwa tayari na ufahamu fulani kuhusu ushirikina. Klabu kubwa pia hapa nchini zinaamini katika ushirika ndiyo maana kumekuwa na vitendo vingi vya uvunjwaji wa kanuni katika ligi kuu Tanzania kama vile klabu kugomea kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo katika baadhi ya viwanja kwa hofu ya kufanyiwa uchawi.

Kuna makocha wa klabu za VPL wapo mbele kushughulikia mambo ya kishirikina wakiamini unaweza kuzisaidia klabu zao kufanya vizuri. Ni kweli wachezaji wa Tanzania ‘wanarogana’ na kupeana majeraha ili wapate nafasi ya kucheza? Kamati za ufundi au tunatakiwa kuwa na mabenchi ya ufundi imara katika klabu zetu?

“Nimepima kila kitu lakini hakuna tatizo na nimetoka kwenye hospitali za Dar es Salaam hivi karibuni tu lakini nao hawakuona tatizo, nimeamua kutumia dawa za asili, hizi za mitishamba ya kawaida wanazijua wazee wa zamani ambazo angalau sasa zimenipa mabadiliko.”

“Lakini hapo kabla nimeteseka sana, nimeumwa sana kwa kweli, nasikia hamu ya mpira na keshokutwa (leo Jumatano) natarajia nikaanze mazoezi kidogokidogo ingawa wasiwasi wangu lisije kuanza tena, maana hata siku za nyuma nilikuwa napata nafuu, nikirejea mazoezini linaanza tena, sasa sijui itakuwaje, naomba Mungu anisaidie,”

Kisa kama hiki cha Javu inawezekana kisiwe cha imani ya kishirikina lakini katika mazingira mengine maumivu yake hayo yanashangaza kwa kuwa huyapata akiwa klabuni tu.

Alisema, Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Hussein Javu, ambaye ameshindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na maumivu hayo tangu walipotoka kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar miezi mitatu iliyopita.

Kuna visa vingi vya kishirikina wachezaji wa Tanzania wanakutananavyo lakini kwa sababu ushirikina ni imani potofu wengi hawataki kutajwa majina yao licha ya kwamba ni wao wanaotoa habari za mambo wanayokutana nayo. Je, wewe shabiki wa kandanda Tanzania unaamini kuwapo kwa ushirikina katika mafanikio ya klabu au mchezaji? Baada ya kisa hiki nitawapa kisa kingine…

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here