Home Kitaifa YANGA SC: SIMBA SC ILISHABEBWA SANA TU, TFF ITUTAZAME KWA JICHO LA...

YANGA SC: SIMBA SC ILISHABEBWA SANA TU, TFF ITUTAZAME KWA JICHO LA TAHADHARI

683
0
SHARE
Jerry Muro-Afisa habari klabu ya Yanga
Jerry Muro-Afisa habari klabu ya Yanga
Jerry Muro-Afisa habari klabu ya Yanga

Na Baraka Mbolembole

Ikitaraji kucheza mchezo wa robo fainali ya michuano ya kombe la FA dhidi ya Ndanda SC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mkuu wa kitengo cha habari wa klabu bingwa bara, Yanga SC, Jerry Muro amesema kwamba ratiba mpya iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa miguu nchini, TFF si rafiki kwao hasa wakati huu wakiwa katika michuano mitatu tofauti.

Baada ya mchezo wa Alhamis hii katika kombe la FA, Yanga inataraji kucheza michezo miwili ya ligi kuu kati ya tarehe 3 na 6 mwezi hujao, kisha kucheza na Al Ahly ya Misri tarehe 9 katika mchezo wa klabu bingwa Afrika, kisha watapaswa kucheza tena mchezo wa VPL tarehe 12.

“Sisi kama Yanga tunaona ratiba iliyotolewa safari hii si rafiki sana kwa sababu ratiba inaelekeza tutacheza tarehe 31 siku ya Alhamisi hii katika kombe la FA, Machi 3 pia tutacheza mchezo wetu wa kiporo katika ligi, tutacheza tena tarehe 6, halafu Machi 9 ratiba kutoka Shirikisho la mpira Afrika (CAF) inaonesha tutacheza na Al Ahly kutoka Misri na mara baada ya mchezo huo, tutacheza tarehe 12”, anasema Jerry Muro ambaye timu yake inashika nafasi ya pili katika msimamo wa VPL pointi 7 nyuma ya vinara Simba SC.

Yanga ina michezo mitatu ya kiporo sawa na Azam FC lakini kitendo cha kupangwa kucheza mfululizo ndani ya wiki mbili hawakifurahii licha ya kwamba kikanuni wanapaswa kucheza michezo yao. Miaka miwili iliyopita chama cha soka nchini Misri kilihairisha baadhi ya mechi za ligi kuu zilizokuwa zikizihusu klabu za Al Ahly na Zamalek ili kuwapa muda wa kujiandaa zaidi katika michuano ya CAF, lakini kwa Yanga hakutakuwa na nafasi hiyo.

“Ukiangalia kikanuni Shirikisho la mpira wa miguu na bodi ya ligi wako sawa sawa, lakini ‘usawa’ hakuna. Kwenye ligi yenye ‘Chata’ inayoongoza mpira wa miguu duniani kote ni chata ya ‘fair play.’ Namaanisha mchezo wa ungwana ndani na nje ya uwanja na hasa katika kipindi hiki ambacho tunatayarisha timu. “

“Sisi hatushindani na kanuni. Kanuni inasema ndani ya masaa 72 timu inatakiwa kucheza mchezo mwingine mara baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza. Na kikanuni wenzetu (TFF na bodi ya ligi) wako sawasawa, lakini niwaambie tu kuwa, kanuni si msaafu, kanuni siyo biblia, kanuni siyo kitabu ambacho hakibadiliki tena.”

“Kanuni imetengenezwa,pia kanuni zinaboreshwa. Ukiangalia kanuni hii na miundo mbinu na jiografia ya Tanzania si kanuni rafiki sana kwetu sisi kwa sababu unapocheza tarehe 31, unapocheza tarehe 3, unapocheza tarehe 6, unapocheza mechi ya CAF tarehe 9, kwa wachezaji si haki.”

“Mechi zote tunazocheza ni ngumu na muhimu. Kombe la FA tupo hatua ya robo fainali, klabu bingwa tupo hatua ya kufuzu kuingia katika hatua ya makundi, kwenye ligi ndiyo tuko ukingoni kwa hiyo kiujumla michezo yote inayotukabili ni muhimu. Kwa hiyo sisi kama Yanga tunaona ratiba hiyo kwetu si sahihi, TFF na bodi ya ligi wanatakiwa kuitazama upya.”

Wakati, Muro akilalamikia ratiba yao hiyo ambayo TFF imesema watalazimika kucheza hivyohivyo kwa kigezo cha kuwahi muda, Muro ametolea mfano namna mahasimu wao Simba walivyopewa nafasi ya kujiandaa zaidi kwa mechi yao ya marejeano ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri mwaka 2003.

“Tunajenga hoja yetu kwa kutolea mfano wa Simba walipoifunga Zamalek katika mchezo wa kwanza walipewa ruhusa ya kwenda Oman na kuweka kambi ya muda mrefu kujiandaa na mchezo wa marejeano. “

“Walipewa ruhusa wakati ligi ikiendelea. Sisi tunatoa mfano huu kuwaeleza umma wa Watanzania kwamba hiki kinachotokea (kulalamikia ratiba) si kigeni. Kama ni kulelewa na kama kubebwa timu zetu zilikuwa zikibebwa na kulelewa vizuri tangu miaka ya nyuma, ila linapokuja suala la Yanga inakuja ‘nongwa.’

Muro akuhishia hapo tu bali alisema zaidi kwamba maana yote ya ligi kuu wanayo wao Yanga.

“Hoja yetu nyingine, tunacheza ili kumpata bingwa ambaye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika, na tunacheza kombe la FA ili kumpata mwakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, na Yanga tayari ni mwakilishi wa Taifa kwenye michuano ya kimataifa, tena michuano mikubwa zaidi barani Afrika.”

“Ukiangalia malengo makuu ndiyo sisi tunatekeleza sasa hivi, tupo kwenye klabu bingwa Afrika. Hivyo tulidhani kwa hatua hii tuliyofikia sasa tutapewa jicho la tahadhari kwa sababu sisi ndiyo wawakilishi wa Tanzania, hatupo katika michuano hiyo kujiwakilisha kama Yanga, kwa hiyo tunaomba kwa T FF na bodi ya ligi japo wapo katika kanuni, watutazame pia kwa jicho la tahadhari wakati huu tukijiandaa na michezo ya klabu bingwa Afrika.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here