Home Kitaifa MKASA WA YANGA NA ENEO LA JANGWANI UNAFANANA NA MKASA WA LIVERPOOL...

MKASA WA YANGA NA ENEO LA JANGWANI UNAFANANA NA MKASA WA LIVERPOOL NA ENEO LA ANFIELD

877
0
SHARE

Yanga-makao makuu

Na Zaka Zakazi

Halmashauri ya jiji la Liverpool iliisaidia sana Liverpool FC ilipotaka kufanya upanuzi wa uwanja wao wa Anfield. Kikwazo kikubwa kilikuwa udogo wa eneo la pembeni ya uwanja huo uliozungukwa na makazi ya watu…kama ilivyo Jangwani.

Anfield kama uwanja wa moja ya klabu kubwa za Ulaya, hauna hadhi ya kuandaa mechi kubwa za kimataifa ikiwemo fainali za mashindano ya Ulaya. Hii inaiumiza sana klabu hiyo ya kihistoria.

Kwa viwango vipya vya UEFA, uwanja wa hadhi ya fainali ya Ulaya unatakiwa angalau uwe na uwezo wa kubeba watazamaji 50,000, miundombinu ya kisasa ya kijamii pamoja na mambo mengine.

Anfield ina uwezo wa kuchukua watazamaji 45,522 huku ikiwa na miundombinu ya kizamani kidogo.

Ili kulimaliza tatizo hilo, klabu hiyo ilipanga kuufanyia ukarabati uwanja wake ikiwemo kuongeza nafasi za watazamaji mpaka kufikia 59,000 lakini ikakutana na upinzani kutoka kwa wakazi wa pembeni ya uwanja ambao hawakutaka ardhi yao ichukuliwe.

Meya wa jiji la Liverpool, mstahiki Joe Anderson, akaingilia kati kufanikisha mazungumzo na hatimaye wakazi hao wakakubali kuziuza nyumba zao kwa klabu hiyo.

Halmashauri ya jiji la Liverpool ikaenda mbali zaidi kwa kuingia kwenye ushirikiano na klabu ya Liverpool pamoja na wadau wengine kufanikisha mradi huo utakaogharimu pauni milioni 260.

Mradi huu ni sawa na ule wa Yanga pale Jangwani, ukiwa na maana ya kuboresha eneo zima la Jangwani. Siyo tu kuboresha uwanja wa michezo bali mfumo mzima wa miundombinu na maisha ya watu kwa ujumla.

Halmshauri wa wilaya ya Ilala inapaswa kufanya kila iwezalo kuhakikisha timu pekee kubwa iliyobaki wilayani humo, Yanga, inafanikisha mpango wake ili isihame wilayani humo. Mpango huu ukikamilika, atakayekuwa wa kwanza kunufaika ni wilaya yenyewe.

Hoja ya kwamba Jangwani kwa sasa ni katikati ya mji kwa hiyo hapafai kwa uwanja wa michezo, ni dhaifu mno. Santiago Bernabeu ni uwanja uliopo katikati ya mji kama Posta mpya.

Ukisema hivi utasikia watu wanagunia chinichini kwamba “kule ni Ulaya na huku ni Afrika”. Kule miundombinu iko poa sana kwa hiyo siku ya mechi foleni inadhibitika. Hapa kwetu foleni ya kwenda mjini itakuwa kubwa sana siku ya mechi.

Hiyo ni hoja dhaifu pia kwa sababu siku zinasonga mbele, hazigandi. Tanzania ya miaka ijayo itakuwa na miundombinu mizuri na tatizo hilo halitokuwepo!

Halmashauri ya wilaya ya Ilala ilitakiwa kukaa meza moja na Yanga pamoja na kualika wadau wengine kuangalia namna bora ya kufanikisha mpango huo.

Kama kiu ya Yanga kufanikisha ndoto yao itakwama pale Jangwani, wanaweza wakafanya uamuzi mgumu kama Simba na wao wakahamia wilaya nyingine halafu Ilala ikabaki na usingizi wake.

Ilala inatakiwa kuacha kulala na kuhakikisha vivutio vyao vya Simba na Yanga havitoroshwi kama wale tumbili waliokamatwa uwanja wa ndege.

0718171079

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here