Home Kitaifa MECHI 5 NDANI YA SIKU 14, MECHI 8 APRIL, RATIBA HAIJATENDA HAKI...

MECHI 5 NDANI YA SIKU 14, MECHI 8 APRIL, RATIBA HAIJATENDA HAKI KWA YANGA SC, AZAM FC

1122
0
SHARE
Mechi ilianza vizuri lakini kadiri muda ulivyokwenda ndivyo mambo yalivyochacha

Mechi ilianza vizuri lakini kadiri muda ulivyokwenda ndivyo mambo yalivyochacha

Na Baraka Mbolembole

Ni katika ligi kuu ya England pekee, tena kwa kipindi cha ‘ Xmass na Mwaka Mpya’ tu utakuta klabu zikicheza michezo isiyopungua minne ndani ya siku kumi. Nimesikitishwa sana na namna mpangalio wa ratiba wa ligi kuu Tanzania Bara ulivyo kwa msimu mzima na namna wahusika wanavyoendelea kupoteza uelekeo wakati huu ligi ikielekea ukingoni.

Tumeshayaona mengi ambayo hatuyapendi, lakini hili la Yanga SC na Azam FC kucheza game tano ndani ya wiki mbili linachukiza sana. Najiuliza ni kweli TFF inamakusudi salama na klabu hizo katika michuano ya CAF?

Machi 31 Yanga watapaswa kucheza mchezo wa robo fainali wa michuano ya FA, kisha April 3 watapaswa kucheza mchezo wa ligi, siku tatu baadaye-yaani April 6 watapaswa kucheza tena mchezo wa ligi, watapumzika tena siku mbili tu na tarehe 9 April watapaswa kurudi tena uwanjani kucheza mchezo wa VPL.

Yanga watacheza mchezo wa klabu bingwa tarehe 13- yaani siku nne baada ya kucheza mchezo wa ligi na watapaswa kusafiri kwenda Misri kwa mchezo wa marejeano.

Ni kweli timu inapaswa kuwa tayari kucheza wakati wowote lakini mathalani ratiba ya Azam FC (kucheza mechi 8 ndani ya mwezi April). Kila mtu anafahamu kwamba mwezi una wiki nne, kwa maana hiyo Azam watalazimika kucheza gemu 2 kila wiki kwa wiki nne mfululizo. Hii haiko sawa licha ya kwamba timu hizo zinaweza kuingia uwanjani na kucheza mechi zao.

Sababu yote ya kutokea haya ni mechi za viporo zinawahusu washindani hao wa ubingwa, lakini mechi hazipangwi mfululizo hivi kiasi cha kuvuruga kabisa programu za makocha wa timu hizo. Mechi za Yanga ziliahirishwa kwa sababu siku ya mechi zao za ligi walikuwa pia na michezo minne ya klabu bingwa Afrika.

Nafikiri, wapangaji wa ratiba ya VPL si watu wa mpira kabisa kwa kuwa hata ‘kuchomeka’ mechi za viporo wakati ligi ikiendelea hawawezi. Je, TFF inapanga ratiba zake bila kufuata kalenda za CAF na FIFA? Kama sivyo, mbona mpangalio wao ni wa kipekee kiasi cha kulalamikiwa na kila timu?

Toto Africans, Mwadui FC, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Simba SC, Coastal Union, African Sports, Kagera Sugar, JKT Ruvu zote zimelalamikia mpangalio mbovu wa ratiba msimu huu. Baada ya timu kulalamika na kupuuzwa na TFF sasa mashabiki wa Azam na Yanga ndiyo wamekuwa kifua mbele kulalamikia ratiba ya marekebisho yalivyofanywa na TFF.

Azam itapaswa kusafiri kwenda Mwanza kisha Turiani, Morogoro kabla ya kwenda Tunisia kurudiana na Esparance katika mchezo wa kombe la Shirikisho. Simba walikuwa na haki ya kulalamikia ratiba wakati walipokuwa wakichezeshwa hovyohovyo na ratiba ya hovyo hovyo.

Yanga hawana kosa kwa kweli kwa kuwa hawabadilishi ratiba wao, hivyo kuwachezesha bila kupumzika si jambo zuri. Azam wengi tulilaumu ruhusa waliyopewa kwenda Zambia kucheza michuano isiyo rasmi mwezi Januari wakati ratiba ya VPL iliwataka wabaki nchini na kucheza mechi zao kwa sababu timu ambayo walipaswa kucheza nayo katika hatua ya awali ya michuano ya CAF ilijiondoa katika michuano.

Lakini nao hawapaswi kubanwa hivi kwa sasa. Timu hizi zote mbili ikumbukwe zinaiwakilisha nchi katika michuano ya CAF. Je, TFF ambayo huwa inalalamikia upungufu wa muda wa maandalizi katika timu ya Taifa haijaliona hili kwa Yanga na Azam FC?

Bado haki haijatendeka ingawa timu hizo zitaingia uwanjani kucheza mechi zao. Wapangaji wa ratiba za mashindano wanapaswa kuondolewa sasa na TFF inapaswa kutazama upya ratiba yake dhidi ya Yanga na Azam wakati huu wakiendelea na kampeni yao katika game za CAF.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here