Home Kimataifa CHAD VS STARS: MECHI YA KWANZA YA SAMATTA KAMA NAHODHA, ATAMBEBA MKWASSA...

CHAD VS STARS: MECHI YA KWANZA YA SAMATTA KAMA NAHODHA, ATAMBEBA MKWASSA MBELE YA RIGOBERT SONG?

768
0
SHARE

gg

Na Baraka Mbolembole

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) siku ya kesho Jumatano itakuwa na mtihani mwingine mgumu ugenini dhidi ya Chad katika pambano la mzunguko wa tatu hatua ya makundi kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika-CHAN 2017.

Michezo miwili ya kwanza kwa kikosi cha Stars haikuwa na matokeo mazuri, chini ya kocha aliyepita M-holland, Marti Nooij, Stars ilichapwa 3-0 na Misri, Alexandria, na mechi iliyofuata ambayo ilikuwa ni ya kwanza kwa kocha mzawa, Charles Boniface Mkwassa ilimalizika kwa suluhu dhidi ya Nigeria katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

CHAD NI YA 114 KWA UBORA DUNIANI, YA 22 AFRIKA…

Mshindani wa tatu wa Stars ni Chad, taifa ambalo halijawahi kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika. Wakati, Stars ilifuzu kwa fainali za Afrika mwaka 1980 (miaka 36 iliyopita) Chad ni taifa ambalo linajijenga kwa maana ya hawakushiriki mara kadhaa hatua kama hii ya kufuzu kwa sababu ya kuandaa kizazi kipya.

Nimetazama wastani wa umri wa wachezaji wa Chad, kiukweli wanaonekana kupevuka sana kiumri, sijui kimpira watakuwaje. Stars ilijilinda vizuri dhidi ya Misri kwa dakika 60, lakini kufikia dakika ya 69 timu ilikuwa imechapwa magoli 3-0, dhidi ya Nigeria, Mkwassa alijitahidi kuifanya timu ishambulie na kujilinda vizuri.

Achilia mbali bao la kujifunga kwa timu pinzani, bado hakuna mchezaji ye yote yule wa Stars aliyefanikiwa kufunga goli katika michuano hiyo hadi sasa . Lalini kuna mengi yamebadilika katika timu ya Mkwassa kuelekea mchezo wa Jumatano hii.

Mbwana Samatta anashikilia tuzo ya ufungaji bora wa klabu barani Afrika, pia ndiye mshindi wa tuzo nyingine binafsi ya mchezaji bora wa mwaka uliopita Afrika, akiwa tayari amefunga magoli mawili katika michezo minne ya ligi kuu ya Ubelgiji akiwa na klabu ya Genk aliyojiunga nayo mapema mwaka huu akitoka kushinda ubingwa wa Afrika upande wa klabu akiwa na TP Mazembe ya DR Congo.

Samatta anataraji kwa mara nyingine kuongoza safu ya mashambulizi ya Stars, lakini safari hii kwa mara ya kwanza akiwa na beji ya unahodha katika bega lake la kushoto. Wachezaji wengi wa Chad wana umri kati ya miaka 27 hadi 32, bila shaka watakuwa na uzoefu wa kucheza nyumbani katika michezo ya kimataifa.

Kama ilivyokuwa kwa Misri 3-0 Stars, Chad pia waliibana sana Nigeria katika mchezo wao wa kwanza, lakini walijikuta wakipoteza mechi hiyo ya ugenini wakati muda ‘umekwenda,’ walifungwa 2-0. Mechi yao ya pili walicheza nyumbani na Misri, walichapwa 5-1 matokeo ambayo yamewafanya kuwa mkiani mwa kundi wakiwa bila pointi yoyote.

Uwezo wao kimbinu bado uko chini ndiyo maana licha ya kuonekana kujilinda vizuri wakilazimishwa wanakubali kufungwa. Hata Stars hucheza vizuri lakini timu zote zinakutana zikiwa na viwango vya kukaribiana, umakini mdogo, makosa yasiyo na ulazima katika ngome kutaiangusha timu yeyote katika mchezo huu kwa kuwa Chad wana washambuliaji wazoefu wanaocheza nje ya nchi yao.

Nadjim Haroun ndiye kiungo mchezesha timu wa Chad, anacheza timu ya daraja la chini Ubelgiji, huyu ndiye aliyefunga goli lao pekee katika michuano hiyo hadi sasa.

Jinsi ya kupanga mashambulizi na kupiga pasi za mwisho bado ni tatizo kwa Taifa Stars lakini bado kuna nafasi ya washambuliaji wetu kufunga walau magoli mawili katika mchezo huu, ni namna watakavyochezeshwa na kupewa mipira ya mwisho na viungo kutaangaza ubora wao.

Thomas Ulimwengu na mwendo wake wa kasi na nguvu akitokea upande wowote ule, Samatta (binafsi ningependa aanze na nahodha msaidizi, John Bocco) wanaweza kuwafanya walinzi wote wa Chad kuwa na hofu.

Katika ngome, Chad hawana mchezaji wa kulipwa, wengi wanacheza ligi yao ya ndani kwa maana hiyo kwa namna yeyote watapata wakati mgumu kuwazima washambuliaji wetu watatu wafungaji (Tom, Samatta na Bocco)

Tishio kubwa kwa Stars na nafikiri kocha Mkwassa atapaswa kuchanga vizuri karata zake ni katika safu ya kiungo. Marius Mbalam kiungo mchezesha timu ya Belfort ya France National, Azrack Mahamat anayecheza Platanias ya ligi kuu ya Ugiriki, Sanaa Altama wa Petrolut ya ligi kuu ya Romania na Sylvain Idangar wa AS Lyon ya Ufaransa ni viungo muhimili wa mbinu za kocha Mcameroon, Rigoberb Song.

Song, mchezaji wa zamani wa Cameroon na timu nyingi mashuhuri barani Ulaya anaweza kuwapanga viungo watatu kati ya wanne hao. Azrack ana miaka 27, Marius ana miaka 28, Idangar ana miaka 32 na kijana pekee ni Sanaa mwenye miaka 25.

Umri wao umepevuka lakini bado kuna nafasi ya vipaji vya ligi kuu Bara kuchanua katika idara hii kama tu wachezaji wetu vijana kama Himid Mao, Jonas Mkude, Deus Kaseke, Salum Abubakary na wengineo watacheza kwa ari ya kusaka ushindi kama ilivyokuwa dhidi ya Nigeria na Algeria (kufuzu WC) jijini, Dar fs Salaam.

Kukaba, kucheza faulo za kitaalamu, kumiliki mpira, pasi timilifu, kutengeneza nafasi na kupiga pasi za mwisho kutaisaidia sana safu ya mashambulizi, na bila shaka timu itafunga magoli ya kutosha kama viungo watatimiza mambo hayo niliyoyataja.

Ngome ya Stars mara nyingi imekuwa ikiiangusha timu, rejea sare ya ajabu dhidi ya Algeria, Novemba mwaka jana, washambuliaji walifunga magoli mawili maridadi sana lakini safu ya ulinzi ikaruhusu magoli mawili ya kuchukiza sana.

Wengi walichukizwa na mabadiliko ya Mkwassa, kumtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Said Ndemla wakati timu ikiongoza 2-0, lakini Mwinyi Hajji alihusika katika goli la kwanza la Algeria kwa kupiga pasi ‘mkaa’, na safu yote ya ulinzi ilihusika katika goli la kusawazisha la Algeria kutokana na umakini wao mdogo, na kujipanga vibaya.

Magoli 8 ya Shomari Kapombe katika VPL msimu huu akicheza katika beki 2, kiwango cha juu cha kupandisha mashambulizi kutoka kwa Mwinyi katika beki 3, uwezo wa kujipanga wa David Mwantika katika beki ya kati, na ukabaji wa nguvu wa Kelvin Yondani katika beki 4, vyote havitakuwa na maana kama timu itafungwa tena magoli ya kizembe.

Nahodha wa Chad, Ezechiel N’Douassel, 27, anayechezea klabu ya Sfaxien ya Tunisia, kijana Rodrigue Ninga, 22 anayekipiga Montpellier ya Ufaransa ni washambuliaji ambao wataitumia nafasi yoyote watakayopewa na walinzi wa Stars.

Washambuliaji hawa wanacheza vizuri mipira ya juu, pia ni wamaliziaji wazuri hivyo kuanzia kwa golikipa, Ally Mustapha hadi kwa walinzi wake watapaswa kucheza na kuondosha vizuri mipira ya juu itakayoelekezwa golini kwao.

Song alikuwa mlinzi mahiri wa kati, wakati Mkwassa alifahamika kama ‘master’ wakati wake wa uchezaji kama kiungo wa dimba la kati. Chad hushambulia ikicheza nyumbani, lakini Stars ni timu isiyo na utamaduni wa kujilinda kokote inapocheza.

Kuwa na Samatta, Tom na Bocco aliye katika kiwango, kunaweza kumkumbusha Song mambo mengi wakati wa uchezaji wake na hivyo kuingiza timu yake katika umbo la kujilinda. Mkwassa angependa washambuliaji wake wachezeshwe kama yeye alivyokuwa akiwachezesha washambuliaji nyakati zake za uchezaji ili kumshinda Song.

Lakini bado pasi za mwisho hakuna katika timu, pasi za namna ile ya umbali mrefu ambayo ilipigwa na kiungo Henry Joseph kwenda kwa mshambulizi Danny Mrwanda, ambaye alifunga mbele ya Song wakati Stars ilipopata goli la kuongoza dhidi ya Cameroon (ugenini, 2009-Kufuzu WC 2010 na CHAN 2010)

Kila la heri Taifa Stars, ushindi una maana kubwa sana kwa kuwa Misri watacheza mara mbili na Nigeria wiki hii, hivyo pointi 6 dhidi ya Chad zinaweza kuifanya Stars kuwa juu ya timu mojawapo kati ya Misri na Nigeria kabla ya kurejeana nazo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here