Home Kimataifa “MZEE WENGER ATAKAPOKUWA SHAHIDI WA MANENO YA ERIC THOMAS PALE CATALUNYA” 

“MZEE WENGER ATAKAPOKUWA SHAHIDI WA MANENO YA ERIC THOMAS PALE CATALUNYA” 

663
0
SHARE

Wenger-disapointed Mwanafilosophia na mwanauchumi Eric Thomas aliwahi kutoa kauli yake moja maarufu (quote) akisema “winners focus on winning, losers focus on winners” akimaanisha washindi wanazingatia kwenye ushindi na washindwa wanazingatia kuwaangalia washindi. 

Nimeukumbuka usemi huu baada ya kuingalia timu ya Arsenal kwa miaka 10 ya karibuni baada ya kuondoka vizazi vya akina Viera, Eeaman, Tony Adams, Thierry Henry na wengineo kibao. Imekuwa ni timu yenye kushindwa kumaliza vizuri karata zake ikiwemo karata ya ubingwa wa ligi kuu na karata ya ubingwa wa klabu bingwa Ulaya.

Matukio kama haya yana sababu nyingi za kisoka ikiwemo sera (philosophy) mbalimbali za mzee wenger, mtisho wa kikosi(squad pressure) na ndiyo maana ni jambo la kawaida kumuona Oliver Giroud, Flamin, Sanogo, na hata Aarteta kila alfajiri wanapaki magari yao ya thamani pale London kwa ajili ya mazoezi wakati Payet, Mahrez, Lukaku wakiwa sehemu zingine. 

Anguko la mzee Wenger lina sababu nyingi ikiwemo bajeti ya klabu kutokana na ujenzi wa uwanja wao wa Emirates, lakini binafsi moja ya sababu ya anguko la mzee wenger ni kuanza kuiga na kuwaangalia wanaofanya vizuri pasipo kuwa na uhakika na anachokifanya. 

Mzee wenger aliamua kuwaiga FC Barcelona kutumia vipaji vya shule yao ya soka ya La Masia na yeye kuamua kuanza kutegemea wachezaji makinda kutoka kwenye academy yake na wengine kuwanunua, na kuamua kuwaacha akina Kolo Toure, Emanuel Adebayor, Reyes, Eboue na wengine kibao na kuanza kuwapa nafasi akina Cesc Fabrigas, Jack Wilshere na akina Gibbs.

Sahau mfumo wa kuiga academy bado akilini mwa mzee wenger anaamini maadui zake wakubwa wa mafanikio ni akina Manchester United, Liverpool na Chelsea na kusahau kuna akina Man City, Tottenham, na Leicester city. 

Sehemu ambayo Wenger anaweza akawa shahidi mzuri wa maneno ya Eric Thomas ni kitendo chake cha kuamua kumuiba na kumpa mkataba muibua vipaji (scout) wa timu ya Leicester City na kusahau mafanikio ya Leicester City msimu huu yana sababu nyingi za kisoka mbali na na muibua vipaji huyo. 

Usiku wa Jumatano ya tarehe 16/03/2016 nchini Spain katika jiji la Barcelona, mzee Wenger atakwenda kutaka kufanya jaribio la kupindua matokeo mbele ya timu yenye washambuliaji watatu wenye thamani ya pound Mil 500 (Lionel Messi 250,Neymar 150 na Suarez 100) dhidi ya timu ya washambuliaji wenye thamani ya pound Mil 130 (Mesut Ozil 65, Alex Sanchez 50 na Oliver Giroud 20).

Binafsi naamini mzee wenger atakuwa Nou Camp kama shahidi wa maneno ya Eric Thomas na siyo kama mpingaji wa maneno hayo. Mzee Wenger na koti lake maridadi atakwenda kuwa kama muangaliaji wa mafanikio ya wanaofanikiwa na siyo mpiganaji wa mafanikio yake. Kila la kheri The Gunners kwenye usiku wa Ulaya.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here