Home Kitaifa HASSAN ISIHAKA, ‘NAHODHA MTOTO’ ALIYESHINDWA KUWA VICTOR COSTA MPYA SIMBA SC

HASSAN ISIHAKA, ‘NAHODHA MTOTO’ ALIYESHINDWA KUWA VICTOR COSTA MPYA SIMBA SC

1140
0
SHARE
Beki wa Simba Hassan Isihaka (kulia) akijaribu kumdhibiti striker wa Azam FC John Bocco
Beki wa Simba Hassan Isihaka (kulia) akijaribu kumdhibiti striker wa Azam FC John Bocco
Hassan Isihaka (kulia) akijaribu kumdhibiti striker wa Azam John Bocco wakati timu hizo zilipokutana kwenye VPL raundi ya kwanza msimu wa 2015-26

Na Baraka Mbolembole

Walinzi wangapi namba 5 wakali umewahi kuwaona Simba SC? Siwezi kuzungumza kuhusu George Masatu mmoja wa ‘ma-libero’ wanaotajwa kuwa mahiri zaidi kuwahi kutokea ndani ya kikosi cha Simba. Nyakati za Masatu nilipata kusikiliza mechi ya Simba dhidi ya Araab Contranta ya Misri, mechi hiyo kama kumbukumbu zangu ziko sawa ilikuwa mwaka 1997, mechi ya michuano ya kombe la CAF.

Mtangaji kama sijapoteza kumbukumbu alikuwa ni marehemu Ahmed Jongo na mechi ile ilipigwa Misri. Kutokana na umahiri wake wa kuipanga ngome, kuruka juu na kucheza mipira ya hatari licha ya kuwa na kimo kifupi, kutibua mipira ya hatari ya timu pinzani, mchezo wa nguvu na utulivu, Waarabu walikuwa wakimpiga makwenzi Masatu ili kumuondoa mchezoni.

Masatu alikuwa amenyoa upara na Mtangazaji (Jongo, Mungu amrehemu) alikuwa akisimulia kila tukio kwa usahihi. Nilijikuta nikimuuliza marehemu baba yangu kuhusu mchezaji huyo (Masatu) naye akatoa sifa zake nyingi kumuhusu Masatu pia hazikutofautiana na zile zilizokuwa zikitolewa na mtangazaji.

Zinanifanya niamini kuwa ni kati ya mlinzi wa kati wa kukumbukwa sana  klabuni Simba kutokana na kazi yake. Nilikuwa darasa la pili wakati  huo, sikuwahi kumuona Masatu, ila kuna nyakati nilimshuhudia mlinzi  mahiri wa kati Amri Said ‘Stam’ kisha Boniface Pawassa, Lubigisa  Madata Lubigisa, Patrick Betwel.

Wote hawa walikuwa bora, walikuwa  wenye nguvu, uwezo wa kujiongoza na kuongoza safu yote ya ulinzi, ila  kuna walinzi ambao naweza kusema walijitahidi kufikia sifa ya Masatu  ambaye sikuwahi kumuona.

Unamkumbuka, Mrundi, Said Koko’o? Nilipenda sana utulivu wake, Nilipenda sana kumuona  Betwel akicheza kama beki  wa kati, alijiamini sana kama ilivyokuwa kwa Koko’o, Betwel naye alikuwa mahiri katika uchezaji wa mipira ya juu, lakini kwangu ‘hakunaga’ kama Victor Costa ‘Nyumba’.

Mchezaji mtulivu, mkimya,  mwenye kujiamini wakati wote, makini katika kuipanga ngome yake na mtu aliyeweza kujiongoza mwenyewe uwanjani. Nani kama Costa? Labda  Masatu. George Owino, Juma Nyosso, Kelvin Yondani wote hawa walikuwa walinzi makini lakini walikosa utulivu na uwezo wa kuiongoza safu ya ulinzi.

Costa alikuwa mlinzi mahiri wa kati na uwezo wake wa kuusoma mchezo ulimfanya kuwa maeneo mengi ambayo wapinzani walitegemea kufunga. Unapokuwa na Costa katika safu yako ya ulinzi si rahisi kufungwa goli ndani ya maeneo ya hatari lakini naye alikuwa dhaifu kama tu asingepata walinzi wasikivu katika ngome.

Majeraha yalitibua kipaji hiki cha aina yake, lakini aliporudi tena msimu wa 2011/12 aligeuka suluhisho la muda mfupi katika ngome iliyokosa kiongozi na kuisaidia Simba kufika fainali ya Kageme Cup, Julai akiwa mchezaji muhumi katika kikosi cha Moses Basena.

Costa ndiye aliyeifanya Simba kuwa na beki ya uhakika tena hadi alipopatwa na majeraha kiasi akashuka tena lakini huwezi kuitaja Simba ya 2011/12 na mafanikio yake bila kumuhusisha Costa. Yondani alikimbia timu sababu ya Costa na alirudi baada ya Costa kupata majeraha.

Nimeona taarifa ya uongozi wa Simba kumsimamisha kwa muda usiojulikana nahodha wake msaidizi, Hassan Isahaka kwa kosa la kumtolea lugha chafu kocha Jackson Mayanja. Isihaka hakupangwa katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Yanga SC wiki iliyopita na wala hakuwepo katika orodha ya wachezaji wa akiba licha ya kwamba alikuwa timamu kimwili na kiakili.

Lakini hata kama ningekuwa mimi katika nafasi ya Mayanja nisingempanga Isihaka katika mechi ambayo najua nakwenda kukutana na washambuliaji wabunifu kama Amis Tambwe na Donald Ngoma. Isihaka tangu alipopandishwa timu ya kwanza kutoka kikosi B na kupewa unadhoha wa Simba akiwa na miaka 20 mwanzoni mwa msimu wa 2014/15 hadi sasa hajajipambanua kuthibitisha ubora wake wa uhakika.

Amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka. Ni kama ‘kipima joto’ ambacho hubadilika badilika hali yake kutoka na hali ya hewa ilivyo. Mchezaji ambaye unacheza kikosi cha kwanza kwa misimu mitatu mfululizo ni lazima upande kiwango chako ila kiwango cha Isihaka kimebaki palepale, anafanya makosa yaleyale kila mara na si kiongozi makini kwa wenzake.

Mlinzi ambaye alichangia matokeo mabaya chini ya kocha Patrick Phiri kutokana na mchezo wake wenye umakini mdogo aliendelea kupewa nafasi na Goran Kuponovic, kisha Dylan Kerr lakini  taratibu akaanza kukwama kwa Mayanja.

Kwa muda aliocheza Simba na umri alio nao, Isihaka bado ana mengi ya kujifunza na kuwa mlinzi mahiri klabuni Simba lakini anapaswa kupandisha kiwango chake uwanjani na si kujikweza nje ya uwanja wakati timu haijawahi kupata mafanikio yoyote chini ya unahodha wake zaidi ya kutwaa kombe la Mapinduzi Cup mwaka 2015.

Kufikia kiwango walau cha Koko’o itakuwa hatua kwa Isihaka ila kufikia walau nusu ya sifa za uchezaji wa Costa kunahitaji, umakini, nidhamu, utulivu, ukimya na uwajibikaji.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here