Home Ligi EPL MOURINHO SI MTU WA ‘MANCHESTER’ ILA HAKUNA MENEJA BORA WA KIINGEREZA

MOURINHO SI MTU WA ‘MANCHESTER’ ILA HAKUNA MENEJA BORA WA KIINGEREZA

764
0
SHARE

Jose-Mourinho-United

Na Baraka Mbolembole

JOSE Mourinho si mtu hasa wa Manchester lakini hata Sir Alex Ferguson mwenyewe atakuwa mwenye matumaini ya kuona mpinzani wake huyo wa  zamani anapewa kazi ‘iliyowashinda’ David Moyes na Luis Van Gaal.

Tangu kujiuzulu ghafla kwa Fergie mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2012/13 Manchester United imekuwa timu ‘isiyo na uhakika wa  kumaliza katika nafasi 4 za juu katika ligi kuu ya England.’

Ryan Giggs anatajwa pia kuwa huenda akawa kocha wa United katika siku za  usoni na kiungo huyo mshindi wa mataji 13 ya EPL na mawili ya ligi ya mabingwa Ulaya kwa sasa ndiye meneja msaidizi wa Luis Va Gaal.

Pia aliwahi  kukaimu nafasi ya kocha mkuu katika michezo minne ya mwisho wakati Moyes alipotimuliwa mwishoni mwa msimu wa 2013/14. Chaguo la Giggs  linaweza kuwa ‘kamari’ na kama itakuwa na matokeo mabaya ni wazi kuwa United itakuwa imerudi nyuma kwa hatua nyingi.

Fergie alitengeneza rekodi zake mwenyewe Old Trafford katika kipindi cha miongo miwili na nusu. Mbinu zake za kipekee zilizokuwa za Kiingera ziliipaisha Manchester United.

Wakati, Moyes alipoandamwa na mashabiki, vyombo vya habari kufuatia matokeo mabaya mfululizo, Jammie Carragher alisema kuwa ‘Mscotland huyo’ alipaswa kupewa muda zaidi na kama United ingemfuta kazi ingeonekana wazi kuwa Waingereza wameshindwa kusimamia klabu kubwa duniani.

Kwa maana nyingine alimaanisha kuwa ni aibu kubwa kwa Waingereza ambao walibebwa zaidi na Ferguson. Napendezwa sana na uchambuzi wa mlinzi huyo wa zamani wa Liverpool na timu ya Taifa ya England kwa kuwa amekuwa mkweli daima. Kinachoendelea kumkuta, Gary Neville pale Valencia ni dalili ya kile alichowahi kusema Carragher.

Neville hajapata ushindi wowote katika michezo 9 ya La Liga tangu alipopewa kazi ya kuwanoa Los Che mwezi Disemba, 2015 na kama atashindwa na kutimuliwa itakuwa anguko lingine la nyota wa muda mrefu aliye kuwa chini ya Ferguson katika maisha yake yake ya uchezaji. Tayari, Steve Bruce ameshindwa, Mark Hughes alishindwa pale Man Cty.

Roy Keane ambaye alianza vizuri kazi ya ufundishaji kiasi cha kuipandisha ligi kuu timu ya Sunderland lakini katika ngazi ya juu zaidi kiushindani alishindwa. Hawa ni baadhi tu ya wachezaji waliokuwa msingi wa mafanikio ya Ferguson kiufundishaji.

Neville ameendelea kuwa mjasiri kwa kusisitiza kuwa hawezi kujiuzulu kufuatia mwanzo mbaya pale Mestalla lakini ni wazi anaelekea kushindwa. Giggs, Paul Scholes wanaweza kuonekana wakombozi wa United siku za mbele.

Wakati klabu kubwa Ulaya kama Real Madrid, AC Milan, FC Barcelona, PSG, Atletico Madrid zikiwaamini waliokuwa wachezaji wao nyota, na kuwapa majukumu ya ufundishaji kwa England hakuna klabu kubwa inayoweza kuwaamini wachezaji wao wa zamani na kuwapa majukumu ya umeneja.

Waingereza wote wangependa kumuona Mourinho akibaki England, tena katika klabu kubwa. Giggs anaweza kuwa mtu hasa wa Manchester lakini ujio wa Pep Guardiola katika timu ya Manchester City msimu ujao, ubora wa mameneja wa kigeni pia umezorotesha maendeleo ya mameneja Waingereza waliotabiriwa kuwa makocha bora kama Allan Pardew na Big Sam.

United kwa sasa haihitaji tu mtu wa Manchester kama alivyowahi kusema Ferguson wakati alipompendekeza Moyes kuchukua kazi yake. Jose ni mtu ambaye ana hamu na matanio ya kuifundisha United.

Nafikiri baada ya kuangushwa na wachezaji wake muhimu msimu huu pale Chelsea kiasi cha kutimuliwa kazi, Mourinho anadhani atajenga heshima nyingine kubwa duniani akiwa na United hasa ukizingatia atakuwa ameichukua timu iliyoshindwa kuwika kwa misimu mitatu mfululizo.

Huyu ndiye mtu ambaye United inamuhitaji wakati huu na si kucheza kamari nyingine kwa kumpa majukumu hayo Giggs.

Baada ya kufanya kazi na Moyes na sasa Van Gaal itakuwa muhimu zaidi kwa Giggs kufanya kazi tena na Mourinho ili kuendelea kujifunza mbinu mpya kutoka kwa makocha wengine. Kumbuka kuwa alikuwa chini ya Ferguson tangu angali yosso hivyo ni lazima apate mbinu nyingine mpya.

Mourinho amejijengea tabia ya kushinda mataji na kuondoka katika klabu anazokuwa anazifundisha, na watu wa United hawapendezwi na meneja wa namna hiyo, ila kwa hali ilivyo naunga mkono kwa asilimia moja ujio wa Special One.

United itacheza namna gani? Hilo ni jukumu la Mourinho mwenyewe lakini bila shaka tayari atakuwa amesoma mwenendo wa Moyes ulivyokuwa baada ya kuuondoa utamaduni wa kiuchezaji pale Old Trafford, Van Gaal aliuza wachezaji wote wa ‘Manchester United’ na kutumia zaidi ya pauni milioni 200 kusajili wachezaji aliowataka.

Lakini naye ameshindwa kuirudisha United katika ‘tabia yake’ ya kumaliza mechi kupitia pembeni mwa uwanja. Jose atakutana na changamoto nyingi ila amini ni mtu ambaye klabu inamuhitaji zaidi wakati huu kama yeye anavyosubiri kwa hamu kutangazwa kuwa meneja wa klabu hiyo.

Baada ya Moyes kushindwa ningempendekeza Giggs ila kwa kile kinachoendelea kumtokea Van Gaal ni wazi wakati wa mtu mwenye mbinu na uwezo wa kuichezesha United ‘Kiingereza’ ndiye mwafaka, na Jose sina shaka naye.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here