Home Ligi EPL PEP GUARDIOLA YUPO CITY KWENYE MBUYU WAKE

PEP GUARDIOLA YUPO CITY KWENYE MBUYU WAKE

679
0
SHARE

Pep Guardiola-City

Na Athumani Adam

Ni hulka ya binadamu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwenye maisha. Ndiyo kitu ambacho kimetokea kwa kocha mkuu wa Bayern Munich anayelamalizia mkataba wake pale Allianz Arena. Mafanikio yake na uwezo wake mkubwa wa kufundisha ndio chanzo cha yeye kuhama.

Alianzia Barcelona akaipa mataji ya kutosha kisha kuacha athari ya tik-tak ile staili ya uchezaji wa pasi nyingi, baadaye akaondoka zake. Baada ya kumaliza kile kipindi kirefu cha mapumziko, alirudi zake Ulaya kuinoa Bayern Munich kwa takribani misimu mitatu hadi mwisho wa msimu huu.

Amepata taji la Bundesliga kila msimu, ingawa bado changamoto aliyonayo ni kushinda taji la ligi ya mabingwa Ulaya. Msimu uliopita Bayern ilitoka hatua ya nusu fainali, ilitolewa na mabingwa wa sasa Barcelona lakini bado Pep ana nafasi msimu huu tusubiri muda utatuambia.

Kama ilivyo kwa Pep na makocha wengi vijana hawana tabia zile za akina Alex Ferguson na Arsene Wenger, ile tabia ya kufundisha timu moja kwa muda mrefu. Makocha wa sasa hawazidi miaka mitano kwenye mikataba yao.

Kwasababu hiyo ya kutopenda kukaa kwenye timu muda mrefu, sasa Pep yupo ndani ya Manchester City. Yupo kwenye EPL kuanzia msimu unaofuata. Unaweza kujiuliza swali dogo, kwa nini Pep amekubali kuifundisha City na siyo Chelsea, Man UTD au kuendelea Munich? Jibu sio pesa pekee kwamba ndio kitu kimemfanya Pep aikubali City

Wakati mwingine pesa sio kila kitu kwenye maisha, kuna kipindi mwanadamu anakuwa na furaha ya kufanya kazi na watu watakao thamini mchango wa kazi yako. Bahati nzuri watu hao wapo Man City, wao ndiyo ushawishi mkubwa wa Pep kuikubali City. Wapo wawili pale City  Ferran Soriano na Txiki Beginstain

Huyu Ferran Soriano ndiye afisa mtendaji mkuu (CEO) wa Manchester City, New York City  ya America pamoja na Melbourne FC. Kabla ya kujiunga na City Soriano aliwahi kuwa makamu wa raisi pia meneja mkuu wa klabu ya FC Barcelona kuanzia mwaka 2003 hadi 2008.

Huyu ndie mtu aliyempatia kazi Pep Guardiola baada ya kuondoka Frank Rijkaard. Pep angekataa vipi kufanya kazi na mtu ambaye alikupa kazi kwa mara ya kwanza kwenye klabu kubwa? Unakataa vipi kufanya kazi sehemu ambayo baada ya pesa lakini pia bosi mkuu ni rafiki yako wa karibu?

Mtu wa pili ni huyu Txiki Beginstain yupo City tangu mwaka 2012, gwiji huyu wa zamani aliyetwaa ubingwa wa UEFA akiwa na Barca mwaka 1992 aliwahi kufanya kazi na Pep pale Camp Nou pia alichangia Pep kupewa kazi pale Barcelona.

Kama kweli kila shetani na mbuyu wake kama wasemavyo waswahili, basi Pep Guardiola ameifuata mibuyu yake miwili pale Etihadi. United walimtaka Pep wakamkosa, Chelsea wamemkosa lakini nguvu ya Soriano na Beginstain pale City wamempata.

Pep yupo City, tunasubiri project mpya kipindi hiki ambacho Yahya Toure akielekea mwisho wa ubora wake, tunasubiri kuona timu inayocheza soka la uhakika yenye makosa machache mithili ya mashine uwanjani. Pep yupo kwenye mbuyu wake.

Email: athumani46664@gmail.com

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here