Home Kitaifa TFF, MALINZI NA AZAM, WATANZANIA WANAYO MIGUU YA KUYAFUATA MAJI.

TFF, MALINZI NA AZAM, WATANZANIA WANAYO MIGUU YA KUYAFUATA MAJI.

950
0
SHARE

jamalShule ni ngumu sana,  na wanaoifanya kuwa ngumu zaidi ni wale walioamua kutufanya tukubaliane na Hali kuwa elimu haina mwisho. Hilo ndo haswaa jambo linalofanya wapatikane watu wanaochukizwa na goli la Frank la Lampard kisha wanaamua kuja na Goal line Technology. Hilo ndilo haswaa lililowafanya Serbia kunyoosha mikono juu na kuamua kuwekeza soka lao kuanzia mashuleni, huko ndiko wameanza kupatikana hawa akina Grujic waliosajiliwa Liverpool.

Maisha ya kisasa hayakwepi upanuzi wa ubongo wako. Hata masikini ili ayafurahie maisha yake ya kimasikini yampasa kuishi kwa akili nyingi, akili ya kukubaliana na Hali kuwa hawezi kuja kuwa Dangote. Ukikubali akili ifanye kazi unakubali kujifunza Kisha unakubali kuwa Algeria walisubiri miaka 20 na zaidi kustaajabu kizazi hiki cha akina Mahrez na Brahimi.

alg

Walisubiri ndio lakini wakifanya jambo sahihi, na kwa akili ya upembuzi na moyo wa kuhitaji mafanikio. Haitokei siku tiketi yako ya basi ukaitumia katika ndege,  hapa unakuwa hujatendea haki akili yako. Ni jambo la kusikitisha hasa kushuhudia kila wino wa mwandishi wa habari, kila ulimi wa wadau wa soka unasema tofauti kuhusiana na soka la Tanzania.

Inauma kushuhudia hasi nyingi kuliko chanya katika kila lisemwalo juu ya Taifa hili kimichezo achilia mbali sekta nyingine ambazo hapa sio mahala pake. Ni kweli Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu? Ni sahihi Tanzania kuwa hapa ilipo? Ni sahihi kuwa na mchezaji mmoja tu ambaye ndio kwanza mwaka 2016 anaenda kujaribu maisha ya Ulaya katika kizazi hiki cha Utandawazi.

Na hivi ni kukosa shule ndo kunafanya tusithamini kilichokuwa Chetu na kusimamia misingi yetu? Nilikuwa nafuatilia suala la Azam kuondoka nchini kwa ruhusa maalumu kwenda kushiriki michuano ya “ghafla”  nchi ya jirani Zambia. Unapopata nguvu ya kumlaani mwanao basi jiandae kumtaka radhi mjukuu wako. TFF ni kweli ni sahihi Azam kuwa huko walipo Sasa?  Ni sahihi kuwepo na viporo kwa sababu tu ya mechi za mwaliko.

azam

Mtoto wenu soka mnamkosea sana,  matunda ama mafanikio ambayo kimsingi ndiyo mjukuu wa kila shirikisho naye kakosa adabu. Hana mbele wala nyuma, hajulikani lini kaamka na lini kalala. Upande wa pili wa shilingi vilabu navyo vinakula kwa kutumia nyuma ya kiganja. Havijawahi kuthamini umuhimu wa soka la kisasa, si ajabu Fareed Mussa ameketi hapo alipo.

Utaratibu upi unakufanya kuchukua ruhusa rasmi ya kwenda kushiriki mashindano yasiyo rasmi na kusitisha ligi yako unayoshiriki na kugombea ubingwa. Ni sehemu ya upangaji matokeo au ni sehemu ya kukosa shule na elimu sahihi ya soka. Ingeenda timu ya vijana ya Azam huko Zambia lisingekuwa jambo la kheri zaidi?  Mshale wa saa uambatana na ule wa dakika achilia mbali upi unawahi kufika kwenye 12, lengo lao ni moja kukupa taarifa ya Muda.

Hata yanga wanaomba, simba wangeomba na ilee Toto African ingekuwa njiani kufanya hivyo hivyo. Utandawazi unatuharibu,  uwekezaji unatupoteza na ujanja ujanja ndio unashika hatamu. Sina hakika kama Azam itakuwa tulivyoidhania miaka 5 iliyopita, nitakuwepo kushuhudia wakiniaminisha kuwa sikuwa sahihi. Inawezekana kabisa kuna wenye nia njema TFF lakini wenye silaha kali ni wengi kuliko wenye ngao dhaifu.

sy

Sizitaji Simba na Yanga sio kwa nia mbaya lakini kuna haja gani ya kumtega kikongwe wakati ukimnyang’anya fimbo pekee unamwangusha. Mabadiliko ya soka ilikuwa lazima yaje nje ya hawa lakini TFF wamekumbatia Jeneza la maendeleo yetu,  Azam wanachepuka na hawana haja na njia kuu bahati mbaya ndugu zangu Mbeya City hata jezi zao zimepungua barabarani.

Utangulizi wa Ilani ya Malinzi wakati anaelekea kugombea Urais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, uliambatana na maneno,  “ili tuweze hatuna budi kuiga mfano hususani waliyofanya wenzetu na wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira wa miguu”.  Tuige,  tujifunze, tufuate na neno lolote ambalo angependa kutumia, yote ni shule hii.  Malinzi mwalimu wako ni nani katika hili?

Nchi gani iliyoendelea soka linaendeshwa hivi? Hizi Ilani nani anaandika,  na ni nani anawatuma kugombea kama hakuna nia ya dhati ya kufuta machozi ya wanaoathirika zaidi na mambo mabovu haya ambao ni mashabiki?   Njaa haiitwi njaa mpaka uhitaji chakula, na kicheko lazima kiambatane na meno kuwa nje.

Jezi za timu ya taifa zikitambulishwa na wadau badala ya wachezaji
Jezi za timu ya taifa zikitambulishwa na wadau badala ya wachezaji

 

Hapa ndipo Tanzania tulipo, hatuna njaa tena kisoka kwa sababu hatujaamua kuwasha jiko la upishi,  na tumefumba midomo makusudi kwa sababu furaha na kicheko sio jadi yetu. Tumenuna,  tumefedheheka Kisha tumeyakubali maisha haya. Maisha ambayo ligi kuu inazipisha ligi ndogondogo nje ya ratiba.

Zawadi mpya Nicasius aliyojaliwa kuishuhudia ni kituo cha kidongo chekundu ambacho hata timu yangu ya shule ninaweza kuipeleka pale kufanya mazoezi. Magroup ya whatsapp mabonanza yao yapo pale, wenye pesa wanaenda kuruka mpira pale (maana sio kucheza) na kisha kinaitwa kituo rasmi mahususi kwa kukuza vipaji maridhawa kwa siku zijazo.

kid

Kipofu huongozwa na anayeona hili safari iwe yenye usalama lakini ni Tanzania ambayo kipofu amekuwa TFF na anawasimamia wenye mboni za macho wasitende yaliyomaovu, atayaona vipi? Utanashati wa mheshimiwa Malinzi bahati mbaya umesimama katika mavazi na sio uongozi. TFF angeivisha suti zake, leo hii ningekuwa naandika kuhusu namna ipi inatufaa kwenda mbele zaidi kama Taifa la kisoka.

Ukitizama ramani, jirani wa kipekee wa Tanzania ni Kenya,  Burundi, Rwanda na Uganda lakini katika hili wala hawako na sisi. Kule kwenye msimamo wa Fifa wao wanatukimbia,  hata baada ya Rais wa shirikisho lao kuonekana ni Mwizi wa Muda mrefu Kenya hatuwakaribii. Ni kweli watanzania ni wakimya,  ni kweli Tanzania inaishi kwa kudanganywa, ni dhahiri njaa zetu zimegeuka shibe, lakini haina maana hatukuwa na miguu ya kusimama kuyafuata maji.

TFF tafadhalini, Malinzi nakuomba wakati Watanzania wanahitaji mpishi sahihi wa soka lao,  msitake kuwaua kwa kiu ya soka maana kiu haivumiliki. Wengi hawakuelewi kwa sababu hata Twitter unatumia lugha ya Kiingereza kutoa taarifa Muda mwingi. Wanayo miguu ya kuyafuata maji,  waambie na Azam, hatuweki urembo wa matundu kwenye paa la Nyumba, mvua ikinyesha wataloa tu.

Ahsanteni.

By Nicasius Nicholaus Agwanda ( Coutinho Suso)

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here