Home Ligi EPL MANCHESTER UNITED: NAOMBA TUENDELEE NA SAFARI YA IBIZA

MANCHESTER UNITED: NAOMBA TUENDELEE NA SAFARI YA IBIZA

1328
0
SHARE

man

Mchezaji wa Kiingereza katika klabu ya Arsenal ambaye pengine ana kila sababu ya kuwemo kikosini siku zote ni Aaron Ramsey, huyu naye ni raia wa Wales. Pale Chelsea yupo anayeelekea ukingoni John Terry pamoja na asiyeeleweka kwa siku za karibuni Garry Cahill. Liverpool wanajaribu kuishi kiuongouongo na kina James Milner na Jordan Henderson na mgonjwa Daniel Sturridge.

Manchester United yupo Wayne Rooney anayefukuzia rekodi zake tofauti kuliko ubora wa miaka mitatu nyuma, na Smalling anayeonekana kukomaa. Picha gani inakuja kichwani?  Hakuna uongo tena, bali ni ngumu sana kwa nchi ya Uingereza kupata mafanikio kwa siku za karibuni zinazokuja.

Wachezaji bora watakaounda timu yao ya Taifa itabidi watoke Tottenham,  Leicester,  Everton kisha waokotwe baadhi katika timu hizi kubwa. Hata Man City wana Hart na Sterling. Nimepata kumbukumbu ndefu sana za kizazi cha dhahabu. Kizazi ambacho Owen na Gerrard walikuwa Liverpool,  Lampard alikuwa Chelsea na Terry bila kusahau Joe Cole, Beckham, Scholes,  Rooney na Ferdinand walitoka United.

england

Ni kipindi hiki ambacho Ferguson alikuwa kocha wa United. Ni wakati huu ambao big Lamp na Terry walikuwa miamba ya Chelsea, na ni saa hizo ambazo Gerrard alikupa kila sababu ya kuamini ni kiungo bora zaidi achilia mbali umaridadi wa Owen. Ulitaka nini zaidi ya kumwona Becks akielekea kupunga mkono wa kwaheri huku wakibaki Scholes na Rooney na kisiki Ferdinand?

Lakini maisha tuliamua kuyabadili wenyewe. Lilikuwa swala la Muda tu mpaka kila klabu itamani kuachana na Waingereza. Lilikuwa jambo la kusubiri tu kushuhudia mipira ya krosi ikiwa inaelekea kuzikwa katika kaburi lake la milele. Kitendo cha soka kuingiliwa na pesa kilikuwa ni kipigo tosha kwa Waingereza.

Kwanza hawakuwa wakizalisha vipaji halisi,  na pia soka lilianza kuhitaji ladha sana.  Kila klabu na kila mwekezaji alitaka kufanana na Barcelona kiuchezaji. Liverpool ikaachana na asili yake na hata alipotaka kuirejesha King Dalglish alionekana kupishana na saa ya kisasa, alichokiacha Ferguson alijua kukitumia yeye mwenyewe, ndo maana Cleverley yupo huko alipo leo.

cle

Dakika zimesogea sana,  mahala pa Carrick pale United anacheza Muda mrefu sana Schnerderlin,  Young anafaa kwa beki kuliko winga na akina James Wilson ni nadra sana kuwakuta uwanjani. Wakati wa Ferguson usingemshuhudia Martial pale Carrington kwa kiwango kile cha pesa,  asingejisumbua kuhangaika kujaza “watoto” wa kisasa wakati kuna raia wa kumpa asilimia 200 ndani ya uwanja.

Ndo maana Nani alimpisha Young,  Cleverley alikabana mara nyingi na Xavi na Jones alikuwa kipenzi chake kikubwa. Maisha hayajawa Sawa tena tangu Moyes aone kuwa Fellaini alistahiki kuingia kikosini. Hutakiwi kumkumbuka tena Ferguson katika kipindi kama hiki,  unamkumbuka wa nini wakati haupo tayari kushuhudia Herrera akimpisha Jones?

Soka limeanza kuhitaji wachezaji walaini kuliko wenye ugumu wa Valencia. Ligi kuu ya Uingereza sio ngumu tena kutokana na watu wake bali kutokana na ushindani wa kina Firmino na Ericksen. Wakati uwanja wa Old Trafford ukipata heshima chini ya babu,  wajukuu wameamua kuutumia wanavyotaka,  wajomba wanaufanya wanavyotaka.

wood

Pesa nyingi ya Woodward imeleta mabishoo wasiotaka kukimbia uwanjani Muda wote, imeleta wasiojua utamaduni wa Manchester United. Unapojaribu kujilaumu kwanini United haifanyi vyema,  Unapojaribu kuwaza kwanini hakuna nguvu nyingi na uchu katika eneo la ushambuliaji, inabidi ujiulize nani anaweza kurushiwa kiatu au nani anaweza kurusha kiatu kwa goli la kijinga alilosababisha Depay?

De Gea yupo vile baada ya kuishi katika makala mengi ya Ferguson. Yupo vile kwa sababu alikuja akiwa mtoto na akafundwa na Ferguson asiyetaka mchezo na masikhara. Nani amesahau matukio ya kufungwa kizembe De Gea wakati akitoka Atletico? Ferguson alimfanya kila mchezaji aamini kuwa Old Trafford ilikuwa nyumba yao na Carrington ilikuwa ni sehemu yao ya Maombi.

de gea

Lakini hayo maisha hayapo tena,  hizo kumbukumbu zipoteze Muda huu. Utamaduni wa kuwa na dakika ndefu zaidi pale Old Trafford umeondolewa na usasa,  mbio za muda wote pale Liverpool zimebaki Historia. Hata mashabiki wao wanawahi kutoka uwanjani siku hizi huku wale wa Manchester United wakibaki kuzomea ndani ya uwanja.

Ni wakati mpya ambao Arsene Wenger aliutabiri Muda mrefu tangu anaachana na kina Tony Adams Kisha Sol Campbell. Alishatabiri hili na akaamua kuanza kulea watoto wale walaini na mabishoo. Wakati hata Bayern Munich wanamlea Alcantara badala ya kung’ang’ana na Kroos au kutokumruhusu Schweinsteiger unapata picha la maisha ya soka la kisasa.

Barcelona pekee ndio wamebaki kubanana na mizizi ya nyumbani kwao lakini nao hawana Muda mrefu sana huko,  kila eneo wanasajili kidume Sasa hivi. Muda umekwenda sana kwa Sasa hivi kumlilia Ferguson, naamini hata yeye anajua akirudi mambo hayatokuwa sawa tena, na anajua fika kuwa aliondoka wakati sahihi kabisa

barcelo

Ule wakati ambao hakukupatikana aina za Wayne Rooney japo tano Uingereza. Ni ukurasa mpya kwa Sasa,  ukurasa wenye umaridadi kuliko uimara. Wakati ambao beki wagumu wamebaki Chelsea peke yake nayo ni kutokana na tabia za Mourinho. Huku Liverpool kazi Ile ya Mascherano kapewa Emre Can ambaye hataki nywele zake ziguswe.

Unaanzaje kutamani maisha ya Ferguson wakati hata Stoke City wameamua kubadilika na sasa wanaye Bojan. Usahihi uliobaki sio kurudi zama zile tena,  usahihi wa Sasa ni kuwekeza vyema tu kwa watoto wa Rio De Jenairo,  Monte Video au kuvuka mpaka kuwafuata walaini wa Hispania kule katika beach ya Ibiza.

Hata Nike au Adidas hawataki kumuona Phil Jones mbele ya Herrera we unataka kwa sababu zipi?  Hakuna maisha ya Fergie tena,  tuendelee na Ibiza tu hata kama ni kwa kufukuzwa Van Gaal. Ni ngumu kuzoea lakini ndio raha ya Ibiza na upepo wake.

Ahsanteni

By Nicasius Nicholaus Agwanda ( Coutinho Suso )

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here