Home Kitaifa YANGA MNAMENYEA NDIZI VYUMBANI?

YANGA MNAMENYEA NDIZI VYUMBANI?

737
0
SHARE
Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima (kulia) akizungumza na waandishi wa habari makaomakuu ya klabu hiyo, kushoto ni afisa habari wa Yanga Jerry Muro
Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima (kulia) akizungumza na waandishi wa habari makaomakuu ya klabu hiyo, kushoto ni afisa habari wa Yanga Jerry Muro
Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima (kulia) akizungumza na waandishi wa habari makaomakuu ya klabu hiyo, kushoto ni afisa habari wa Yanga Jerry Muro

NI nadra sana kushuhudia kipaji kama cha Haruna Niyonzima kwa wachezaji wengi butu wa kigeni wanaosajiliwa Tanzania. Lakini si nadra kuona vipaji hivi vikigeuka kuwa karaha kwa namna vinavyolelewa hapa Tanzania.

Hii ni kutokana na sababu nyepesi tu, hatujui kusajili wachezaji wa kimataifa na pindi tunapopatia tunawadekeza mithili ya tausi wanavyoranda maeneo ya Ikulu.

Hii ni sababu ya kuzaliwa kwa kiburi chao, mishahara yao mikubwa inazaa majivuno na mashabiki wanaamua kuwaaminisha hawa wachezaji kuwa Tanzania hawajazaliwa kama wao.

Hakuna kama Emmanuel Okwi, hakuna kama Thabani Kamusoko na hajatokea kiungo mshambuliaji mwenye umaridadi wa Niyonzima. Huo ndio mlinganyo sahihi kabisa wa namna ya tunavyoamua kuwaweka wachezaji wa kigeni. Bahati mbaya ambayo ni kubwa ni kuwa wachezaji hawa wana mawasiliano ya kiurafiki na wafadhili na viongozi wa klabu hizi.

Anaishi akijua kabisa hata siku atakapochelewa kambini kuna kiongozi atakutana naye kwenye baa fulani kisha wapate whisky na kuambizana namna ya kukwepa adhabu. Nani wa kupinga wakati anayelipa mshahara au posho kwa kiasi kikubwa siyo timu ila huyu mfadhili aliyeamua kuwa rafiki wa mchezaji na ndiye anayemtetea.

Wakati sakata la Niyonzima likiibuka nilipata faraja kubwa kwa maana ya Yanga kukomaa. Niliamini Yanga sasa imeiva kama timu kiuongozi kuanzia katika benchi la ufundi mpaka uongozi wa juu wa klabu. Unahitaji kiburi cha uweledi kumpiga chini mchezaji wa kariba ya Niyonzima.

Unahitaji akili yenye utambuzi sahihi kuamua kuachana na Niyonzima. Unapoamua kukataa saini yake wala usiwaze kuwa Simba na Azam watamtwaa, huo ndiyo hasa ukomavu wa kisoka kiuongozi. Wakati msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro akiweka bayana maamuzi ya klabu, nilijipiga kifua, nikafuta uso kisha nikaongeza sauti ya kiabarishi changu.

Sikuwa nimesikia vibaya, sikuwa natizama kwa wasiwasi TV yangu, na wala masikio yangu hayakuwa na uchafu. Niliketi sawia kabisa na kutaka kuamini kuwa sasa pengine lugha ya kitaifa itabadilika kuhusiana na wachezaji hawa wageni.

Siwachukii, lakini nahitaji wafanye kilichowaleta. Hata mitandao ya kijamii haikuongopa, waliounga mkono uamuzi wa kufungiwa Niyonzima walikuwa wengi kuliko waliopinga. Hata vyombo vya habari vilipokea suala hili kama njia mojawapo ya kuonesha kuwa sasa pengine nchi hii ilianza kushuhudia uongozi sahihi katika soka.

Lakini Mtanzania habadiliki, wala haambiliki, na ni mwepesi kusahau. Maisha haya ambayo tumeishi kwa uhuru wetu kwa miaka 55 sasa yanatuharibu. Tumezoea kuuishi uongo ambao unatutafuna. Tunaamini katika tunachoona kuliko  tunachotizama.

Hivi ni kweli Yanga haina maisha baada ya Niyonzima? Ni kweli Haruna alistahili kuzungusha akili za wenye uweledi kiasi hiki? Hapana labda kama thamani ya Yanga imebadilika.

Yanga hii ambayo ipo kileleni ndiyo inateseka na kumweka sawa Niyonzima? Hili ni swali lililoukurupusha ubongo wangu, likarejesha fikra zangu mbali kisha likanifanya niwaze kwa kina zaidi, nini kinatokea? Yanga walidanganya? Yanga hawawezi kuendelea bila Niyonzima au Niyonzima ni muhimu zaidi Yanga? Nikitizama fomu yao sioni ni wapi jina la Niyonzima limekosekana.

Macho yangu ni shahidi wa anachokifanya Kamusoko na akili yangu inatambua mabao ya Tambwe kwa sasa. Lakini uongozi wa Yanga umenipa jipya la kufikiria, je, Watanzania tupo tayari kusimamia soka letu kikamilifu? Ni kweli Niyonzima alifungiwa pasipo na sababu nzito zilizokuwa hazivumiliki na kama zilikuwepo ni kweli zinasameheka kirahisi hivi kwa kurudi kwa waandishi na kufuta tu tamko la awali?

Vazi tulilovaa siyo rasmi, ya nini kuingia kikaoni? Kama Yanga haikuwa tayari kuachana na Niyonzima, basi ingetafuta namna nzuri ya kuweka mambo bayana. Wala siyo jambo geni katika soka. Kuna kipindi unamvumilia Luis Suarez na utukutu wake, kuna wakati unamvumilia Wayne Rooney na karaha zake kwa sababu unaamini katika kile anachokupa.

Lakini akifika mahala ambapo David Beckham anaondoka basi hakuna njia nyingine zaidi ya kumpa baraka zinazouma na zitakazomuuma siku zote. Adhabu zipo nyingi sana, unaweza kumsimamisha mchezaji, unaweza kumkata mshahara, na unaweza pia kumfanya acheze na kikosi cha pili.

Adhabu zinazofahamika kwenye soka, lakini pindi unaposema hili limefika kwa Herode basi hakuna namna nyingine malaika anaweza kujitokeza. Hii ndiyo inatakiwa kuwa thamani ya chapa ya klabu kama Yanga, timu ambayo inaamini imekamilika kimashindano yote ya ndani na kimataifa na inayoamini kuwa inaendeshwa kisasa zaidi.

Hakuna kosa kubwa kama kumenya ganda la ndizi ukalitupa ndani ya nyumba kisha ukalikanyaga. Lisipokuangusha na kukuumiza basi litakuchafulia nyumba. Badala ya kumfunza Kamusoko mmempa sababu ya msimu ujao kuchelewa atakapokwenda kwao Zimbabwe.

Donald Ngoma kapata kiburi cha kugomea mazoezi na kisha Amissi Tambwe anaweza kuonekana na meneja wa Azam FC bila shida. Utawafanya nini, wakati umehalalisha dhambi ndani ya klabu yako? Yanga endeleeni kumenyea maganda ya ndizi vyumbani, athari zake tutazijua, mnaweza msiseme mkiteleza lakini yakiwaangusha chini kishindo chake tutakisikia. Hivi hata barua ya wazi kuwaomba radhi mashabiki Niyonzima kaandika?

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here