Home Kitaifa IBRAHIM AJIB,  WEWE NI NANI NA NI YUPI? 

IBRAHIM AJIB,  WEWE NI NANI NA NI YUPI? 

4203
0
SHARE

ajibHakuna siku ambayo dunia imewahi kushuhudia mvua ya maua waridi, lakini kwa sababu ni moja ya maua yanayohitajika sana namna pekee ya kuendeleza upatikanaji wake ni kuyapanda zaidi na zaidi. Hakuna kitu kizuri kinachokuja bure na wala hakuna jema lisilo na gharama. Ili ufike unapotaka kufika lazima uamue kusafiri na yakupasa uambatane na mizigo yako.

Tanzania sasa inameremeta na mapambo yaliyotokana na maamuzi ya Samata. Vijana wengi wanaona lakini sina hakika kama wanatizama, wengi wamesikia lakini napata shaka kama wameelewa. Sababu kubwa ya wasiwasi huu ni Utanzania wetu ulivyotuathiri.

Utanzania ambao sina hakika kama umemtoka Elias Maguli tangu alipoachana na simba mpaka kwenda Stand United. Utanzania ambao tabia yake kubwa ni kutokuthubutu.Niliwahi kutamani sana Mungu angenijalia miguu ya Humud, miguu ambayo naamini fika Obi Mikel wa Chelsea hana.

Lunyamila enzi za ubora wake
Lunyamila enzi za ubora wake

 

Lakini ipo wapi miguu hii?  Usishangae kuwa nchini Uganda kuna vijana wengi wa rika langu wanaojiita Lunyamila kutokana na mambo aliyoyafanya mtu huyu miaka ya 90 lakini huku kwetu hata Ubungo thamani yake ishasahaulika achilia mbali kuwa wengi hatumfahamu hata sura yake.

Katika kipindi hiki ambacho naanza kuukwaa utu uzima, macho yangu yamekuwa shuhuda wa miguu kadhaa inayosisimua. Achilia mbali kijana Farid Mussa ambaye anatafunwa na mchwa wasio na macho, umemshuhudia Ajib?  Kila nikimtizama najiuliza kama anatambua kuwa nafasi anayocheza viumbe wanaoipatia nafasi hiyo wanaelekea kupotea katika uso wa dunia.

Kila nikiona anatembea kwa mikogo uwanjani nawaza kama anajua kuwa hata Brazil iliyokuwa na kina De Lima ilibidi kuwachukua akina Fred na Jo. Uso wa dunia unashuhudia ongezeko la jangwa katika ardhi na pia katika eneo la ushambuliaji kwenye soka.

tegete

Ukizaliwa na kipaji cha kufunga kama Tegete basi inabidi utambue tu kuwa ukiamua kufa na njaa au kumiliki Vitz ni maamuzi binafsi wala sio ya muumba wa mbingu na nchi.  Kukosekana kwa washambuliaji bora wa asili wengi ndio kumezalisha kwa wingi namna mpya ya soka ya kutumia mawinga na viungo kama wafungaji.

Hii ndio sababu Divock Origi yupo Liverpool, Sanogo anatua Arsenal na Harry Kane wa Tottenham anaonekana Mungu pale Uingereza. Kila ambapo Ibrahim Ajib akigusa mpira unaamini kabisa anaweza kukupa ladha ya Ndemla na Lyanga kwa wakati mmoja. Lakini swali linakuja ataamua kukupa?

Ilimchukua Samata dakika 45 tu kuhitajika na Mazembe, alikuwa anatoa alichonacho, lakini pia alikuwa na bahati nzuri safari yake haikuhitaji kuwa ndefu sana, lakini pia alikuwa amejiandaa na safari yoyote ya ghafla. Huyu Ajib sidhani kama yupo tayari kwa safari na Sina hakika kama mizigo yake ipo tayari.

sam

Hivi ni kweli bado wachezaji wa Tanzania hawatambui huu ni ulimwengu ambao video zipo karibu kupindukia?  Hawaoni ving’amuzi vya Azam vinawapeleka hewani? Mtandao mmoja unaoitwa Wyscout unatumika sana kwa Sasa kusaka vipaji.

Mtandao una wafanyakazi zaidi ya  200 na unakusanya video zaidi ya 1300 kwa siku. Si haba unatembelewa na maafisa wa vilabu vikubwa ulaya zaidi ya 32000. Huku ndiko kapatikana Martial anaeshangiliwa pale Manchester United kwa Sasa. Hii mitandao ipo mingi sana kwa Sasa, inaumiza tu kuona kuwa vijana wengi wa soka hawapo tayari kwa safari.

Sio kila siku Mazembe au Al Ahly watakuja uwanja mpya wa Taifa kucheza wakuone. Na imefika hatua Sasa kuwa Ile haitakiwi kuwa ndio mlengo wa mwisho wa kufikiri wa vijana wetu. Ndoto zimeanza kuwa za Mazembe kwa vijana wengi na sio St. Etienne tena. Siungani na wale wanaoamini kuwa Samata kafungua njia ya wengine.

Ninachoamini mimi ni kuwa Samata yupo katika safari yake mwenyewe.Kila mtu ashike funguo yake na atumie mafuta yake. Nikipewa kipaji cha kuandika na nisipoandika zamani na ningekatwa mikono. Umasikini wa Mtu upo kichwani kwake mwenyewe. Sihitaji kujua ndoto ya Ibrahim Ajib, lakini nahitaji kujua kazi ya miguu yake.

shaffih na mbwiga
shaffih na mbwiga

Inaweza kukutia hasira na ni dharau iliyoje, mchambuzi wa soka Shaffih Dauda au Edo Kumwembe ikiwezekana pamoja na Mbwiga Mbwiguke wameenda Santiago Bernabeu mara nyingi zaidi kuliko ndoto za mchezaji kinda wa kitanzania anavyoota kwenda pale. Fundi ujenzi hatakiwi kulala nje, na wala fundi wa viatu hatembei peku.

Mashabiki wanaweza kufurahi kila akifanya ubunifu wa Neymar pale Amaan, lakini mnajua Neymar anafanyia wapi na kwa pesa ipi? Samata kuwa mchezaji aliyefanikiwa zaidi Tanzania ni kukosa nidhamu ya utekelezaji mambo. Ajib ana kipaji, Farid ni maridadi na Ndemla ni hazina.

far

Ni dhambi kubwa kuwashangilia hawa na wenzao uwanja wa Taifa na kuridhika kuwaona pale.  Moyo wangu unachuruzika machozi ndani kwa ndani, akili yangu imesimama nusu mlingoti, naomboleza rohoni kwa namna gani Wanyama ataenda kupokea mshahara wa Yaya Toure karibuni huku Telela akitolewa kwa mkopo kwa sababu ya Kamusoko.

Njia ya motoni binadamu anajiandalia mwenyewe, hutaki kuamini shauri zako.  Mwanaume anayeamini anaweza na yule anayeamini hawezi wote wapo sahihi. Ajib wewe ni nani na ni yupi?

Ahsanteni.

By Nicasius Coutinho Suso

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here