Home Kitaifa NENDA ZAKO SAMATA, LAKINI USISAHAU KUWA TANZANIA YETU IMEKETI…

NENDA ZAKO SAMATA, LAKINI USISAHAU KUWA TANZANIA YETU IMEKETI…

1204
0
SHARE

samata

Inasemekana kuteleza sio kuanguka, lakini ukiteleza ukaanguka pia sio mwisho wa safari, sharti unyanyuke umalizie umbali uliosalia. Moja ya nchi ambazo inawezekana kabisa baada ya kuteleza ziliamua kuketi na kutizama kitakachotokea ni Tanzania. Rasilimali zinapungua,  wizi unaongezeka, uongo unazidi na maisha yanabaki kuwa ya kijanja janja. Ni Tanzania hii ambayo ndoto ya Kapombe iligeuka kutoka Ufaransa kurudi Azam.

Mawazo ambayo Rivaldo aliyapata baada ya mguu wake wa kushoto kulingana uwezo na miguu miwili ya Chombo Redondo kwa pamoja, mawazo ambayo Ronaldinho aliyapata baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa karne huku akiwa kashinda kila kitu. Ni jirani na ukweli pia kuwa ni Tanzania pekee ambayo unaweza kupata mchezaji aliyekuwa na Kipaji cha Haruna Moshi.

moshi

Kipaji bora uwanjani na Kipaji bora cha kuhairisha yaliyokuwa ya msingi juu yake na maisha yake. Hesabu zake zingekuwa sahihi miaka 7 nyuma leo angekuwa wakala wa wachezaji wa Mbeya City na sio mchezaji mwenzao. Lakini haya yote yapo ili dunia itembee katika mzani wake iliyojiwekea. Yaani hakuna usawa,  na atakayesimama sharti amkute aliyekaa.

Ni kama ambavyo bado huwa najiuliza je Thomas Ulimwengu na Samata ni marafiki wanaoshindana au ni marafiki wanaosindikizana. Hilo la kwanza ndio sahihi zaidi. Wakati Samata anatambulishwa kwa mbwembwe nyingi sana kule TP Mazembe ni dhahiri kuwa Moise Katumbi alishajua kapata dhahabu mchangani.

katu

Ni kipindi hiki ambacho kimahesabu Aden Rage alijua kapata dau kubwa lakini Katumbi akaliwahi akijua thamani ambayo simba hawakuijua kwa kijana huyu. Ni sababu hii ndiyo inampa kiburi Katumbi kumuuza Samata kwa bei anayotaka yeye hata kama katika mkataba Kuna miezi michache iliyosalia. Kwake ni sawa Samata kuondoka bure lakini sio kwa bei ambayo sio sahihi.

Na kama kuna kitu kilichompa kiburi zaidi ukiachana na tuzo ya mfungaji bora wa klabu bingwa Afrika basi ni lile goli la ligi kuu ya Uingereza alilofunga Samata dhidi ya Algeria. Lakini bado Samata anabaki kuwa Mtanzania. Mtanzania kama mimi na wewe, mtanzania kama Shaffih Dauda au Mtanzania kama Joseph Kusaga.

dauda

Mtanzania ambaye kama asiposimama kutoka Tanzania ilipoamua kuketi hatoweza kufika mbali achilia mbali kipaji chake. Mtanzania ambaye Simba aliyoichezea haijui hatima yake juu ya Mo Dewji anayetaka kuwekeza kwake.

Nilikuwa natizama suala la Samata kwenda Genk au Standard Liege. Nilikuwa nafurahi huku tabasamu nimelificha nyuma ya pua zangu. Tatizo langu ni kama amepata nafasi hii akiwa kasimama au ameketi na Tanzania yake. Wewe unaweza kusema Samata anajitambua sana lakini mimi nakwambia nilijua mwaka huu ungekuwa msimu wa pili kwake Ubelgiji.

 Samata alikuwa na uwezo wa kupishaha na Mbokani kwenye ligi Ile mapema sana. Lakini bado hainifanyi kuondoa imani yangu juu yake. Kwa umri wake bado ana miaka 8 zaidi ya kucheza kwa kiwango na kukomaa. Natamani kuwa mwandishi wa kwanza kwenda Ubelgiji kumuuliza amejipanga kumaliza na goli ngapi kwa msimu baada ya mechi mbili za mwanzo kama dili likikamilika.

mbokani

Sio swali jepesi, majibu yake yangenipa mwanga wa kipi anafanya katika mazoezi na kipi kipo akilini juu ya walio mbele yake katika uchaguzi wa kocha. Kuwa na hamu ya kufikia alipo Yaya Toure ni jambo moja, lakini kupitia njia alizopitia ni jambo tofauti. Ni kama ambavyo kuwa na Kipaji na kufanikiwa baada ya usajili ni mambo mawili yanayofuatana lakini yasiyolandana.

Mawazo ya Samata yanatakiwa kuwa katika mkataba mnono wa Nike, Puma au Adidas. Ukiwaza hivi unawaza kuwa zaidi ya Solomon Kalou na jirani kabisa na Didier Drogba. Mawazo hayo hayakuweki mbali na alipofika Divock Origi. Kila nikimtizama Yannick Bolasie sioni sababu ya Samata kutokufika ligi ya Uingereza au Bundesliga katika misimu miwili kama akisimama na kuachana na Tanzania iliyoketi.

ndemla

Singano aliketi nayo,  Ndemla ameagiza kiti aketi,  Fareed Mussa atanogewa na soga kisha ataketi mpaka akipatikana mtu wa kufanya dili lake la kwenda nje liwe la haraka. Tuliketi na kuitizama Tanzanite ikielekea Kenya na India. Tuliketi Twiga wakisafirishwa, tumeketi kipindi hiki ambacho  watoto wetu wanaweza wasipate kuwashuhudia vifaru na tunaelekea kulala walikoamkia Sudani Kusini. 

Nenda Samata, nenda kafanye kweli lakini usisahau kuwa Tanzania imeketi. Simba haina tena dili na Sunderland wala Madrid, Henry Joseph hatujui nini kilitokea na kidongo chekundu kimejengwa katikati y jiji. Usisahau kumdokeza na Ulimwengu kuwa mnahitaji urafiki wa kimashindano. Ukisimama wewe pengine na Geoffrey Mwashiuya atajua maana ya sakata la Yanga na alikotokea.

Ahsanteni.

By Nicasius Coutinho Suso.

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here