Home Kimataifa KWAHERI PEP GUARDIOLA, WALAU SASA HIVI UMEKUNA KICHWA KWA NGUVU….

KWAHERI PEP GUARDIOLA, WALAU SASA HIVI UMEKUNA KICHWA KWA NGUVU….

851
0
SHARE

PEP

Kuna baadhi ya vitu ambavyo kama mwanadamu inabidi uvikumbuke sana, na ni muhimu kumshukuru Mungu kuwa ulipata kuvishuhudia. Mojawapo ni kuona Sir Alex Ferguson akitetemeka sio kutokana na baridi ama ugonjwa uliokuwa unamwandama hapana bali ni kile alichokuwa akishuhudia kikifanyika dhidi yake na timu yake.

Alikutana na Barcelona iliyokuwa na vina mwanzo kati na mwisho. Mtiririko wake haukutofautiana sana na misingi inayozingatiwa katika utunzi wa mashairi ya HipHop.  Kila aliyekuwa anagusa mpira ungejiuliza alikuwa anaelekea kupeleka wapi na ungekuwa umekosea.

fergie

 

Pengine Fergie hakufadhaishwa na pasi zilizokuwa zinapigwa bali namna ambavyo timu yake isingeweza kumiliki mpira kwa walau sekunde 40. Ni kumbukumbu ambayo mwisho wake lazima ungehitimisha kwa neno Guardiola. Mtu ambaye alifanya ulimwengu usahau kama Johan Cruyff aliwahi kutamba na Total Football.

Ni katika kipindi hiki ambacho yalianza majina ya Xavi, Iniesta kabla ya kina Pirlo, Gerrard, Lampard achilia mbali Messi ambaye alikuwa analala Pluto na kufanya mazoezi Catalan. Ni kipindi hiki ambacho timu ya taifa ya Hispania ilishinda kila kitu huku robo tatu ya kikosi cha kwanza ikiwa ni ya kikatalunya.

barcel

 

Siku ambazo dunia ilifurahi kuwashuhudia Barcelona zililetwa na Pep,  kipindi ambacho Hispania inautawala ulimwengu kilikuja na Pep. Kila akiwaza kumpandisha Busquet alikuwa anaandaa usalama wa taifa lake pia. Wakati anamwingiza Pedro pahala pa Henry alikuwa ananoa makali ya taifa lake na mwisho akafanya pasi za muda mwingi zionekane kuwa na tija kuliko umaridadi wa Ronaldinho na Deco.

Dunia ikafuata mkondo aliotengeneza ikatelezea huko, bahati mbaya hata wale wabunifu mavazi akawachota akawaweka anapotaka na mavazi yake yakawa maarufu. Kama ilivyoada akili yake hufanya kazi kwa kasi ya mwanga,  aligundua siku za mwisho zinakaribia kwenye utawala wa Barcelona.

ron

Ndio alibakiwa na Messi aliyekuwa bora lakini uti wa mgongo ulianza kudhoofika. Iniesta alianza kukumbwa na majeruhi na Xavi misuli ilianza kujikunja. Akasema kwaheri kabla hatujagundua kuwa katika kisima chake kulikuwa na mafuta na karibuni vingejitenga.

Yulee akaenda zake Marekani kula raha, mahesabu yake yakawa wapi atapata malisho yaliyokuwa bora. Kwa sababu hakukuwa na namna anaweza kwenda Madrid, mahala salama zaidi palikuwa Bayern Munich. Ndo maana wala hakujiuliza kupokea ofa ya kumrithi Jupp Heynckens.

Lakini hapa kulikuwa na tatizo,  tatizo la ubarcelona. Mashabiki walitaka waone hatari Ile ikirejea, utawala ule ukisimama na pengine dhidi ya kizazi alichokikomaza mwenyewe cha katalunya. Bahati mbaya ni kuwa katika maisha haya ambayo dunia inaongezeka joto kwa kasi,  ni ngumu sana kuzaliwa Messi mwingine.

jupp

Ni ngumu kuzaliwa mwanadamu ambaye Wenger ataamini ni mchezaji wa Playstation. Ungeweza kupata robo tatu ya kina Iniesta na Xavi kwingineko, lakini nje ya Cristiano Ronaldo ni karibu na haiwezekani kupata miguu ya kufanya anachofanya Messi.

Hii ndio changamoto ambayo alijua itampa wakati mgumu achilia mbali Ile ya kubadili soka la Ghetto la kijerumani, na kuweka kina Alcantara mbele ya Martinez na Schweinsteiger.Wakati anamweka Lahm katika kiungo alijua anawakera wengi hasa wajerumani kama Franz Beckenbauer lakini walikubali kwa sababu ya wakichokiona kabla.

Walitamani kutengeneza ambacho hakikuwepo kabla. Walitamani kupata atakayetetemeka tena. Lakini maisha siku zote hayawi katika mstari mnyoofu. Ni ngumu kuwa Carlo Ancelloti katika Uefa,  ni ngumu kuchukua ubingwa wa ulaya katika timu mbili tofauti.

Kipaumbele cha Rummenigge ni utawala wa ulaya,  ubingwa wa Bundesliga wanajua fika upo ndani ya uwezo wao.Ilikuwa rahisi kutabiri kuwa Pep asingeweza kubaki pale Allianz Arena bila taji la Ulaya. Ilikuwa burudani mpya kuona anavyohaha kushindana na Messi.

carlo

 

Wakati anacheka tobo alilopigwa Milner alijua fika anakichekea kifo chake pia. Huu unaweza kuwa mwisho usio na furaha kwake. Alikuna kichwa kuliko Muda wowote ule maishani mwake. Wakati anamaliza nywele zake kichwani, kisayansi hakuwa tayari kufanya yale ya Jupp heynckes.

Kwaheri Pep, nyumbani kwako kupya kutakuwa Uingereza, lakini ninafurahi kuona walau ulikuna kichwa kupita kiasi. Messi alikupa kiburi,  usinyoe nywele huku Uingereza ukifika Westham hawatabiriki unaweza kuhitaji kukuna kisogo wakati huu, maana ni mbio za nyikani.

Ahsanteni.

By Nicasius Coutinho Suso

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here