Home Kitaifa NIMEMUELEWA NAPE, HATA JAPAN WAMEFANIKIWA

NIMEMUELEWA NAPE, HATA JAPAN WAMEFANIKIWA

521
0
SHARE
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo

Na Shaffih Dauda

YOKOHAMA, Japan

Nianze kwa kuweka wazi kuwa nimemkubali sana Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kwa wazo lake la kufanya mabadiliko ya kisheria ili kuruhusu njia nyingine za uwekezaji katika soka.

Nape anataka uwekezaji huu utoe wigo mpana kwa soka la vijana ili Tanzania iweze kufanya vizuri siku zijazo. Nimeshukuru kwamba waziri anajua uozo uliopo katika soka na naamini atashughulikia kila kitu.

Waziri anajua rundo la watu walioingia katika soka kwa nia ya kujinufaisha binafsi na siyo kuifanya nchi ipige hatua katika soka, hao ndiyo wanatakiwa kuondoka katika mchezo huu.

Lazima tuwe na mfumo mzuri wa uwekezaji katika soka ili tuweze kufanikiwa, tazama tulivyopata tabu katika mchezo dhidi ya Algeria wa kufuzu Kombe la Dunia 2018. Tulicheza na nchi iliyowekeza katika soka.

Watu waliamini tungeitoa Algeria ambayo imewekeza katika soka muda mrefu huku tukiwa na timu ambayo haina uwekezaji wowote ule. Haihitaji uende Japan, Marekani, Hispania au Ujerumani ndipo ujue moja kujumlisha moja siyo kumi na moja bali ni mbili.

Ikaundwa kamati ya wiki mbili ili Taifa Stars iifunge Algeria yenye Riyad Mahrez wa Leicester City ambaye anafanya vizuri kwenye Ligi Kuu England, hatukujua kama wenzetu wamewekeza.

Tukirudi katika mada kuu leo hii ni kwamba, ni lazima tuwekeze katika mfumo mzuri wa soka ambao hutumika kote duniani na siyo kuunda kamati za kukurupuka na kutaka matokeo makubwa.

Katika soka ili ufanikiwe unahitaji vitu viwili tu, kwanza mashabiki na pili ni timu nzuri ya taifa, yaani inayopata matokeo mazuri, hivyo tu basi, vingine labda ni kwa nyongeza.

Nchi nyingi huanza na mashabiki kwanza, yaani kupata mashabiki wanaoweza kupenda soka kwa kujitokeza viwanjani na kote kwenye matukio ya soka.

Mfano rahisi ni Japan, hii nchi haikuwa na soka la kueleweka kiasi cha mashabiki kutojitokeza uwanjani na kila kitu kikawa hakiwezekani kwao maana hata timu yao ya taifa haikuwa ikifanya vizuri.

Wajapani wakatumia mfumo uleule unaotumika kote duniani kwa kurudisha mvuto wa soka lao kwa mashabiki na kwa kuanzia wakaanza kuboresha ligi yao, wakaifanya iwe kali na yenye kuvutia.

Wazo la kubadili mfumo wao wa soka lilitoka mwaka 1992 na mwaka 1993, ligi hiyo yenye mvuto ikaanza wakiachana na ile ya zamani kwa kuiboresha katika baadhi ya vitu.

Sisi Tanzania tuna bahati ya kupata mashabiki tayari lakini bado timu yetu ya taifa haifanyi vizuri, hivyo kuna tatizo lakini si kama lile la Japan, kwa maana wao walikuwa na matatizo sehemu zote, hawakuwa na mashabiki na timu nzuri hawakuwa nayo pia.

Sasa ili mabadiliko ya mfumo waliyofanya yawe chanya, wakaweka mpango au programu ya miaka 100 ili wafanikiwe kwa kuhakikisha ndani ya miaka hiyo wawe na klabu kubwa 100 ambazo zipo katika mfumo unaokubalika kimataifa.

Hapo walihakikisha timu zao zina mfumo mzuri wa soka la vijana kwa kuwa na timu za vijana kuanzia chini ya miaka 17, 20 na 23, pia uongozi ulio katika mfumo na miundombinu imara kwa soka la vijana.

Timu za Ligi Kuu Japan zinafuata mfumo huo kwani zina viwanja kwa ngazi hizo za soka na ni nadra kuona timu inaazima uwanja kwa ajili ya mazoezi, watoto wamepewa nafasi ya kucheza soka na kusoma elimu dunia.

Watoto wote wenye vipaji wanatazamwa nchi nzima na wakishapatikana wanapelekwa katika akademi za timu hizo na hapo hupata elimu nzuri ya soka na ile ya dunia ili waweze kuendana na mambo mengine ya ulimwenguni.

Watoto wamewekewa msingi wa kupenda soka, kwani hata mvua ikinyesha hawasubiri mfanyakazi kutoa uchafu uwanjani, bali wenyewe huondoa takataka na kuendelea na program zao.

Kila siku hufika mazoezini alfajiri kisha huingia darasani na wenzao wanasoma elimu dunia wakiwa tayari wamekamilisha majukumu yao katika soka.

Timu za ligi kuu zina uwezo wa kununua mchezaji kutoka kokote ulimwenguni kwani tayari ligi yao ni maarufu na inayotajwa sehemu nyingi. Klabu zina fedha za kufanya lolote katika mafanikio halali ya soka.

Klabu nyingi za hapa, zinafuata kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa timu kuwa na vitu vyote vinavyotakiwa ili kuwezesha mafanikio ya timu za vijana.

Timu zina vikosi vya vijana ambavyo kweli uendeshaji wake unaonekana upo vizuri, ndiyo maana timu zao za taifa zinafanya vizuri, kwani vijana hao ndiyo wanaotumika katika timu za chini ya miaka 17, 20 na 23.

Leo hii kutokana na ubora wa ligi ya Japan, haiwezi kuwa ajabu ukisikia nyota wa Ulaya wamesajiliwa na timu za ligi hiyo kucheza soka, hii ni mifano tu ya sera nzuri zinazotumika katika mifumo sahihi ya soka.

Kutokana na uwekezaji huo wa Japan, ndiyo maana leo hii wanasoka wao wanatamba duniani, tazama kiungo mshambuliaji Shinji Kagawa amecheza Borussia Dortmund kisha akaenda Manchester United kabla ya kurejea tena Dortmund. Pia wanaye mshambuliaji Keisuke Honda anayecheza AC Milan.

Kwa hiyo nimalizie kwa kusema kuwa, kama Nape akifanikiwa kubadili baadhi ya sheria ili kuruhusu njia nyingine za uwekezaji katika soka, tunaweza kupiga hatua katika mchezo huu.

Tukutane tena wiki ijayo!

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here