Home Ligi EPL ALAMSIKI LEICESTER CITY, MAISHA HAYAJAWAHI KUWA YA USAWA.

ALAMSIKI LEICESTER CITY, MAISHA HAYAJAWAHI KUWA YA USAWA.

550
0
SHARE

leicester

Kuna jambo moja tu ambalo maandiko ya kidini na maandiko ya kisayansi yamekubaliana, nalo ni usiku na mchana.  Kila mmoja anasema kivyake lakini wote wanakubaliana kwa sababu ndilo linaloonekana kwa nyama za macho. Ndio kwa sababu Kuna mambo mawili tu duniani yanayohusu ukweli,  kukubali kukubaliana au kukubali kutokukubaliana.

Hapa ndipo maisha ya Leicester city yalipo kwa sasa. Kuna giza kisha kuna jua,  kuna wanaokubali kukubaliana na wanaokubali kutokukubaliana mwisho wa siku mjadala unafia kwa Mahrez na Jammie Vardy. Bahati mbaya sana mjadala kwa wengi haumuhusu baba aliyewazaa mashabiki wengi wa Chelsea, Claudio Ranieri.

leice

Kitu cha ajabu mpaka sasa ni namna gani swala anaweza kula simba na jamii zake. Ni kwa namna ipi Leicester mpaka kipindi cha Christmas yupo pale juu katika msimamo wa ligi kuu ya Uingereza.

Binafsi sijawahi kustaajabu uwezo wao,  lakini ninastaajabu maisha yao. Ubora wao kipindi chote ulisukwa na kocha mbabe Nigel Pearson, huyu ndiye haswaa kiini cha nguzo hii anayoisimamisha Ranieri. Lakini maisha hayajawahi kuwa na usawa kiasi hiki cha Leicester city.

Hasa katika ligi kuu ya Uingereza, huwa hakutokei wepesi huu,  hasa katika kizazi hiki ambacho Justin Bieber ni maarufu kuliko R Kelly na Kuna watanzania wanasubiri MB Doggy aje kumfunika Diamond.  Bajeti za vilabu nane vya juu ukiachilia mbali Leicester wenyewe ni kubwa maradufu kuliko wao. Hapa ndipo hasa mashabiki wengi hawataki kupasikia,  ukakasi wa hapa hauvumiliki.

psg

Lakini hili linalotokea ni moja ya maajabu yanayopaswa kutokea. Hili linalotokea ni vyema litimie ili tupate imani kuwa Wenger yupo sahihi siku zote na kuwa maisha ya PSG na Manchester City sio ya lazima. Ile imani ya huwezi kupata winga bora mpaka utumie paundi 36 milioni ife kidogo.

Bahati mbaya ni kuwa kuna sehemu moja tu inayoifanya pesa iwe ndo jibu, inaitwa majeruhi.  Leicester hawajakumbana na hili bado, Sanchez au Ozil wao hajaumia, na Aguero wao bado mzima sana na anafunga anavyotaka.Hili ndilo hasa lililofanya TSG Hoffenheim isahau kama ilikuwa inagombea ubingwa msimu wa mwaka 2008-2009 mpaka mwisho wa mzunguko wa kwanza.

Ndoto yao ilihitimishwa na kitu kimoja tu, majeruhi ya mshambuliaji bora wa Bundesliga kipindi hicho kifupi Vedad Ibisevic, aliyekuwa amefunga magoli 18 katika mechi 17. Huyu ndiye aliwafanya kila mechi wacheke na kuiona Bayern Munich rika lao.

ibisev

Kila nikiwaza kwa kina moyo wangu unafadhaika kwa sababu hii. Kila nikitizama timu zote kubwa nawaona Leicester city ndo waliokuwa salama na majeruhi. Kwa kasi waliyonayo hata dirisha dogo la January ni ngumu kuwa mkombozi kwa vilabu hivi vikubwa. Lakini swali ni je, wataweza kasi hii kwa michezo 19 ya hatua inayofuata?

Wataweza kutumia nguvu hizi pasipo Vardy na Mahrez kuingia chumba cha upasuaji? Hakuna mkakati mgumu kama ule wa kupata matokeo kwa vilabu vya Manchester City,  United,  Chelsea, Arsenal, Liverpool,  Tottenham,  Southampton na Everton nyumbani na ugenini.

Na hii ndo sababu hasa ligi kuu ya Uingereza inakuwa tofauti na nyingine zote. Hali hii ingekuwa Ujerumani, Italia na kidogo Hispania ningeanza kuandika baadhi ya mambo kwenye kijitabu changu cha kumbukumbu. 

Lakini hili linanirudisha nyuma sana. Kwa ligi kuu ya Uingereza, raundi ya kwanza na ya pili huwa na mbinu tofauti, mahala pekee ambapo Sir Alex Ferguson anaishi katika ulimwengu wa peke yake.

fergie

Nipo na makabrasha yangu, natamani kuamini nachokiona, na natamani kushuhudia ninachokiwaza. Lakini mawazo mengine yananituma niishi maisha ya ndoto, maana hakuna dhamana mbaya kama ya kumuamini aina ya kina Leicester city.

Haya ndiyo nayaona maamuzi ya busara zaidi, ninarudi katika maisha ya ndoto. Kuamini siwezi ila kuota ninaweza, Alamsiki Leicester City, nikiamka naomba nikute nilichokiona na nishuhudie wengi wasichokipenda. EPL haijawahi kuwa na usawa, na Waingereza hawajawahi kuipenda top 6, nyie mnaongeza nyingine ya 7. Sitaki kuwaamini ila sitaki kukubaliana kutokukubaliana, ndo maana nimeamua maisha ya ndoto.

Tuonane mkivaa au msipovaa medali, nani anajali kwani,  hata Liverpool Wana umri wa Kaka yangu hawajauona ubingwa na hakuna anayewafikiria. Manchester City walikuja kwa ndege, nasubiri kuona kasi ya gari lenu. Ni bahati mbaya sana moyo wangu hautaki kukubaliana na macho yangu. Wazungu wanasema so far so good.

Ahsanteni.

By Nicasius Coutinho Suso

 

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here