Home Kimataifa MAJAALIWA YA UEFA, TUTAKULA VILIVYOBAKI

MAJAALIWA YA UEFA, TUTAKULA VILIVYOBAKI

363
0
SHARE

Group stage come backs

Na Nicasius Coutinho Suso

Wakati makundi ya UEFA Champions League yakitangazwa kulikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa Arsenal ingekuwa inamaliza nyuma ya Bayern Munich.  Lakini hakuna aliyefikiri kuwa Arsenal ingesubiri siku ya mwisho kuitetea nafasi yake ya pili. Ungewezaje kufikiri hivyo wakati Olympiacos, Dynamo Zagreb walitakiwa kuwakaba Sanchez,  Ozil,  Carzola,  Ramsey na Olivier Giroud ambaye unabii wake unapingwa na wengi.

Kuvuka kwao linabaki kuwa jambo la heshima na suala litakalowasukuma sana na kuwapa nguvu.  Wakati unawaza na kufurahi kuwa kikosi kidogo cha Campbell kimeweza kupata ushindi basi Sanchez angeweza kuleta ushindi mkubwa zaidi, nami nakwambia hawa huwa hatari zaidi kwani hutaka kuaminisha ulimwengu kuwa hakuna lisilowezekana chini ya jua.

Msimu wa Chelsea haukuwahi kuwa mzuri mpaka goli la kujifunga la Marcano liliposaidia kazi inayoendelea kumshinda Diego Costa muda huu.

Hili ndilo tatizo hasa la Chelsea. Ni rahisi sana kuhisi hawatofika mbali,  ni rahisi sana kutabiri majaliwa yao na ni usahihi sana kuamini hawana maisha marefu ingawa ni kosa sana kuamini haya mbele ya dakika tisini.  Lakini unacheka vipi soka la uhakika wakati wachezaji wako bora wamesahau viatu vyao chumbani kwao?

Hazard hajakaribia walau nusu ya picha yake mwenyewe ya msimu uliopita,  Fabregas ni kama kabadilishwa miguu,  kinywani kwa Diego Costa kunafanya kazi kuliko miguu yake. Wakati Matic akisuasua katika kuwalinda wenzake,  Ivanovic nywele zinaondoka na kiwango chake.  Mwokozi kabaki kuwa Willian ambaye hakuwahi kuwa mfungaji mzuri, lakini ameamka wakati sahihi,  na anafanya kazi iliyo bora.

Wakati nikijaribu kuwaza maisha ya Manchester City,  nawaza maajabu katika UEFA ya mwaka huu.  Imekuwa mara ya kwanza kwao kuongoza kundi,  lakini imekuwa mara kwa mara kwao kuishi kwa bahati mbaya. Hawajawahi kuwa nje ya kundi la kifo,  na wakifuzu hukutana na mbabe zaidi yao au wanayekaribiana nguvu.

Tatizo lao kubwa ni kujua namna ya kucheza katika uwanja wao wa Etihad. Hawajawahi kuutendea haki inavyotakiwa.  Kibaya zaidi ni kuwa katika EPL walau ulikuwa na heshima lakini hata huku imeanza kushuka. Natamani kuwapa nafasi kubwa lakini hili la Etihad linanipa wasiwasi.

Bado maisha bora yapo mikononi mwa Bayern Munich na Barcelona, ingawa usiondoe jina la Benitez katika mashindano haya. Anajua sana namna ya kukabili mtoano kuliko kukimbizana katika mechi 38 za ligi.  Akili yake hufikiria mara saba zaidi ya akili zake za siku zote anapokuwa katika nafasi hii.  Lakini ukweli unabaki kuwa ni dhambi kuiweka Madrid juu ya Barcelona na Bayern Munich,  mpaka pale ambapo Bale,  James, Ronaldo na Benzema kwa pamoja wakiweza kujenga ikulu mpya.

Wakati Barcelona inatajwa sana kwa sababu ya Messi, Suarez na Neymar bado napata shaka kama Guardiola anafurahia maisha ya Munich bila UEFA. Huyu ndiye hasa silaha yao kuliko Lewandowski, huyu ndie sumu pekee inayotakiwa kufanya kazi. Kama kuna mtu ana mawazo zaidi katika UEFA basi ni huyu.

Wakati tukisubiri droo ya siku ya Jumatatu ya hatua ya 16 bora, nakushauri kama mpenzi wa soka tupa jicho lako kwa Zenith St. Petersburg. Hawasemwi sana na hawatoimbwa sana, lakini ipo siku watatajwa sana. Hiki ndicho kifurushi changu cha kustua msimu huu.

Nawatazama kama timu itakayostua mioyo ya wengi na pengine kumaliza nguvu kabisa timu nyingi. Ila ni mpaka pale ambapo droo itakuwa imewekwa ndipo tutapata kutambua kuwa ni kwa kiasi gani Juventus,  Arsenal na Paris St Germain walistahiki kuwa huko waliko.

Ni muhimu sana katika kila hatua iliyobaki ya Uefa kuwepo na mechi za kudhoofisha mioyo. Ni lazima katika hatua zilizobaki tuanze kupata ladha za kustua mapema. Na ni jambo la kheri katika hatua hizi kupata kuona tusivyovitarajia. Haya ndio maisha ya UEFA.

Tunaenda mezani kula tusichokipenda kisha kinatufurahisha na wakati tunajiandaa kula tunachokipenda upishi wake hauridhishi.  Siku ambayo utapata kutizama ubora wa Yarmolenko na Dynamo Kiev yake ndio huo ambao utakulaza ukiwa na simanzi wewe shabiki wa timu utakayokutana nayo.

Lakini hakuna namna, wewe shabiki na mimi Nicasius Coutinho Suso  haya ndiyo tuliyochagua na haya ndiyo tuliyoandaa. Wenger atalia na majeruhi, mashabiki wa Madrid wataendelea kulia na Bale,  huku wale wa Manchester City wakiendelea kumuamini Kevin DE Bryune. Kila timu itakula ilichokipika na kukiandaa, sisi mashabiki tutakula vilivyobaki, iwe furaha au majonzi.

Ndiyo majaaliwa ya UEFA hayo, unajuaje unaweza kuwakuta Arsenal au Chelsea fainali, si unakumbuka Ile Liverpool mbovu iliyoifunga AC Milan, Chelsea ya Di Matteo je au Porto ya Mourinho?  Tuendelee kusubiri, vinavyotufaa ni mabaki.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here