Home Kitaifa YANGA Vs KAGERA, SIMBA Vs MAJIMAJI, MTIBWA Vs MWADUI…KIVUMBI KINAENDELEA

YANGA Vs KAGERA, SIMBA Vs MAJIMAJI, MTIBWA Vs MWADUI…KIVUMBI KINAENDELEA

1069
0
SHARE

taifa
NA Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Bara, Yanga SC watakuwa na nafasi ya kurejea kileleni mwa msimamo Jumamosi hii kama tu watafanikiwa kuishinda Kagera Sugar katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora. Kikosi cha mkufunzi Hans Van der Pluijm tayari kimeangusha alama nne katika mechi 8 msimu huu baada ya kukubali sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui FC siku ya Jumatano iliyopita.

Mabingwa wa msimu wa 2013/14. Timu ya Azam FC iliichapa JKT Ruvu mabao 4-2 katika uwanja wa Karume, Dar es Salaam siku ya jana Alhamis na kukalia kiti ya uongozi wakiwa na alama 22, mbili zaidi ya Yanga wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.

Wakati Yanga ikiwavaa Kagera, jijini Dar es Salaam, timu ya Simba SC itawakaribisha Majimaji FC ya Songea katika mchezo mwingine wa ligi hiyo. Simba ipo katika nafasi ya nne ikiwa na alama 18 inaweza kusogea kwa nafasi moja au mbili zaidi juu ya msimamo kama watashinda na timu za Mtibwa Sugar na Yanga zikipoteza mechi zao.

Mtibwa iliyo nafasi ya Tatu na alama 19 inaweza kushika nafasi ya pili endapo wataishinda Mwadui FC katika mchezo mwingine utakaochezwa Manungu, Turiani, Morogoro . Mechi hizi Tatu zitafuatiliwa zaidi wikiendi hii licha ya kuwepo na mechi nyingine Nne katika miji tofauti.

Katika mchezo wa Kagera na Yanga kinachotazamwa ni kama Yanga itaweza kurejea katika mwendo wa ushindi baada ya kupata sare katika gemu dhidi ya Azam FC na Mwadui FC. Kagera imekuwa dhaifu msimu huu na haijafanikiwa kushinda mchezo wowote tangu Septemba 12 waliposhinda ugenini dhidi ya Mbeya City FC.

Timu hiyo ya Bukoba ilifungwa 1-0 na Mtibwa Sugar siku ya Jumatano tayari imemfuta kazi kocha Mbwana Makatta. Imepoteza mechi 6, imeshinda mara moja tu na kuambulia sare mbili haijawahi kupata ushindi katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi ambao wameuchagua kuwa uwanja wao wa nyumbani.

Kwa namna timu za Mtibwa na Simba zinavyopata ushindi, Yanga watalazimika kuishinda Kagera ili kuendelea kuwakimbia wapinzani wake. Ni tofauti ya alama 1 tu kati ya Yanga na Mtibwa, na kuna tofauti ya alama 2 tu dhidi ya Simba na nne dhidi ya Stand United iliyo nafasi ya 5.

Tanzania Prisons wamefikisha alama 16 pia baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports. Watacheza na Ndanda FC katika uwanja wa nyumbani Sokoine, Mbeya siku ya Jumapili pia wanazidi kuongeza presha kwa timu za juu kiasi cha kufanya michezo ya wikendi hii kutazamwa kwa ‘ umakini mkubwa’.

Simba watalazimika kuishinda Majimaji ambayo ipo nafasi ya kumi na alama zao 11, Mtibwa italazimika kuishinda Mwadui FC iliyo nafasi ya 6 na alama 15, na Yanga watatakiwa pia kuishinda Kagera Sugar iliyo nafasi ya 14 na alama zao 5.

Ratiba Kamili ya mechi za wikendi hii

Kagera Sugar vs Yanga SC
Simba SC vs Majimaji FC
Mtibwa Sugar FC vs Mwadui FC
Tanzania Prisons vs Ndanda FC
Coastal Union vs Mbeya City FC
Africans Sports vs JKT Ruvu
Azam FC vs Toto Africans
JKT Mgambo vs Stand United

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here