Home Kitaifa EXCLUSIVE INTERVIEW: SULEIMAN NDIKUMANA, “KUTOKA KULIPWA LAKI TATU SIMBA MPAKA MILIONI 30...

EXCLUSIVE INTERVIEW: SULEIMAN NDIKUMANA, “KUTOKA KULIPWA LAKI TATU SIMBA MPAKA MILIONI 30 KWA MWEZI ANGOLA, HAIKUWA KAZI NYEPESI”

1281
0
SHARE
Suleiman Ndikumana (kulia) kizungumza na Shaffih Dauda (katikati) na Alex Lwambano (kushoto) wakati wa kipindi cha Sports Xtra
Suleiman Ndikumana (kulia) kizungumza na Shaffih Dauda (katikati) na Alex Lwambano (kushoto) wakati wa kipindi cha Sports Xtra ndani ya Clouds FM

Jina la Suleiman Ndikumana si geni masikioni mwa wapenda soka wa Tanzania wala sura yake si ngeni machoni mwao, huyu ni mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba SC. Jina la Ndikumana lilivuma sana Tanzania wakati akiitumikia klabu ya wana Msimbazi lakini jina hilo kuna kipindi lilipotea lakini likaibuka tena wakati wa harakati za mchezaji huyo alipokuwa akijiunga na klabu ya El Mereikh ya Sudan baada ya zoezi la klabu hiyo kushindikana kumsajili Mrisho Ngassa.

Baadae jina la Ndikumana likasikika likitajwa kama ndio mbadala wa kuziba nafasi aliyokuwa amewekewa Ngassa kwenye klabu ya El Mereikh. Baada ya hapo jina hilo likapotea tena kwenye masikio ya watanzania wengi. Lakini Ndikumana bado yupo kwenye ramani ya soka la ushindani.

Shaffih Dauda na timu nzima ya Sports Xtra wamepiga story na Ndikumana juu ya safari yake soka mpaka kufikia hapo alipo huku Ndikumana akifunguka na kueleza mambo mengi juu ya maisha yake ya soka.

Timu ya Sports Xtra ya Clouds FM kutoka kushoto ni Alex Lwambano na Shaffih Dauda wakati walipofanya mahojiano maalumu na mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba Suleiman Ndikumana (kulia)
Timu ya Sports Xtra ya Clouds FM kutoka kushoto ni Alex Lwambano na Shaffih Dauda wakati walipofanya mahojiano maalumu na mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba SC Suleiman Ndikumana (kulia)

Ungana nae hapa ili kujua maisha ya soka la Ndikumana na jinsi alivyopambana kutafuta mafanikio.

Shaffihdauda.com: Tangu ulivyoondoka Tanzania sasahivi upo wapi na unafanya nini?

Ndikumana: Bado nipo kwenye maisha ya mpira na tangu kipindi hicho nimepita sehemu nyingi. Nimepita Ulaya, nikarudi Afrika na kwa sasa nipo nacheza Angola.

Shaffihdauda.com: Katika sehemu hizo zote ulizopita kunachangamoto gani au kipindi gani ambacho kwako kilikuwa ni kigumu katika maisha yako yote ya mpira?

Ndikumana: Kipindi ambacho kilikuwa kigumu kwangu ni kipindi ambacho niliumia goti nikiwa Ubelgiji na timu ya daraja la pili. Nilikaa mwaka mzima bila kucheza mpira na ndiyo sababu iliyonifanya nirudi kucheza mpira tena Afrika kutoka Europe.

Shaffihdauda.com: Ilikuwaje ukaja kucheza soka la kulipwa Tanzania, Simba walikuonaje?

Ndikumana: Kulikuwa na mashindano ya CECAFA Challenge Cup yalikuwa yanafanyika Kigali, nadhani kipindi hicho tulikuwa kwenye kundi moja na Tanzania na ndio waliniona hapo wakanifata baada ya kucheza mechi na Tanzania.

Shaffihdauda.com: Unaweza kumkumbuka ni nani alikufata kufanya mazungumzo na wewe kuja kucheza Simba?

Ndikumana: Kuna mwandishi wa habari alikuwa ni Saleh na kiongozi mmoja wa Simba anaitwa Magoli ndio walinifuata.

Shaffihdauda.com: Baada ya kuja Tanzania na kukaa mwaka mmoja, ulivyoondoka hapa ulikwenda wapi?

Ndikumana: Nilirudi nyumbani nikacheza mwaka mmoja halafu nikaenda Norway.

Shaffihdauda.com: Katika kipindi ulichokaa Tanzania ni kitu gani ambacho kinakufanya uikumbuke klabu ya Simba hadi leo?

Ndikumana: Kwanza hapa ni nyumbani. Nilipokuwa Simba nilikuwa nahisi nipo nyumbani.

Shaffihdauda.com: Ilikuwaje ukatoka tena Burundi kwenda Norway na baada ya kwenda Ubelgiji halafu tena ukaenda El-Mereikh na leo unatuambia upo Angola?

Ndikumana: Kwanza baada ya Norway nilienda Ubelgiji kufanya majaribio fulani lakini nikashindwa wakawa hawakufurahia kiwango nilichokionesha. Nikarui nyumbani baada ya miezi mitatu kukawa na mashindano tena hapa Tanzania  ya CECAFA. Nilipocheza hapa baada ya mashindano nikapata wakala na yeye pia alikuwa wa hapa Tanzania alikuwa ni Hemed Remtula tukasaini mkataba akanituma nikafanye majaribio.

Kipindi hicho nilienda na mchezaji wa Tanzania Uhuru Suleiman na wote tulienda timu moja. Baada wiki mbili mambo yakawa safi wakaanza kuongea kuhusu mkataba ila Uhuru yeye hawakuweza kumpatia nafasi nikabaki pekeangu.

Shaffihdauda.com: Umeshacheza ligi tofauti barani Afrika na umeona mazingira ya ligi ambazo umecheza yalivyokuwa wakati huo, sasahivi upo Angola ambako wamecheza nyota kadhaa wenye majina makubwa duniani kama Rivaldo, Mputu na wengine. Tofauti ya ligi ya Angola na ligi nyingine ni ipi?

Ndikumana: Tofauti ipo, naweza nikasema kwamba wanalipa pesa nyingi au wanalipa vizuri wachezaji wao na inatokana na wachezaji kujituma. Kila mchezaji anataka kucheza, hiyo inaleta upinzani mkubwa.

Shaffihdauda.com: Wakati ule wa usajili wako wa kwenda El Mereikh ya Sudan ilitokana na kufanya vizuri kwenye michuano ya Challenge nchini Uganda lakini ile nafasi ilikuwa ya Mrisho Ngassa lakini hadi kipindi dirisha la usajili linakaribia kufungwa, Ngassa alishindwa kukamilisha zoezi la kujiunga na timu hiyo. Ulikua umebki muda mfupi lakini walikufata ukamilishe zoezi hilo, ilikuaje hasa ?

Ndikumana: Kipindi hicho  mimi nilikuw ni mchezaji huruna nilipopita kwenye michuano hiyo (Challenge) nikafanya vizuri na timu nyingi zikawa zimeniona. Kabla ya mimi kuamua kwenda El Mereikh kwanza nilikuwa na mazungumzo na Azam na walikuwa wanasubiri wamuuze Ngassa kwenda El Mereikh ndio wanichukue mimi.

Lakini ikafikia kipindi meneja wa Azam akanipigia simu akaniambia mambo ya Ngassa kutoka Azam kwenda El Mereikh yamegoma kwa hiyo mimi niende El Mereikh  na tayari wao (Azam) walikuwa wamefanya mazungumzo na watu wa El Mereikh na wakakubaliana kwahiyo mimi nikamua kujiunga na El Mereikh.

Shaffihdauda.com: Wakati El Mereikh wanataka kumsajili Ngassa tayari dau lilikuwa linakaribia kuwekwa hadharani, na ilikuwa inakadiriwa kuwa ni dola za kimarekani 75,000. Wewe walikusajili kwa kiasi gani ?

Ndikumana: Itakuwa ngumu kuisema lakini ninachoweza kusema ni kwamba, mimi niliwakamata palepale kwasababu walikuwa hawana muda wa kusajili mchezaji mwingine halafu walikuwa na shida na mchezaji wa kuziba nafasi ya Ngassa na mimi nikawakamata nikawaambia waniongeze. Wakasema hakuna shida kwasababu hata rais wa klabu alikuona kwahiyo hakuna tatizo.

Shaffihdauda.com: Kuna kipindi wakati upo Simba kulikuwa na mechi moja kubwa ya fainali ya Tusker kati ya Simba dhidi ya Kagera Sugar wewe uligoma kwenda uwanjani ikabidi ifanyike kazi ya ziada. Kwa nini uligoma kucheza mechi hiyo ?

 Ndikumana: Nakumbuka kipindi hicho, ilikuwa ni tatizo la fedha za mshahara na kulikuwa na mechi kubwa yenye upinzani ikabidi niwakamatie hapo kwasababu kulikuwa na mishahara miwili au mitatu sijalipwa.

Nikazima simu yangu halafu nikajifungia ndani kwangu, wakawa hawanipati ikabidi wapitie kwa ndugu yangu Medi. Medi akanitafuta kwa simu akanikosa ikabidi aje kwangu.

Kwakua yeye ni mpenzi wa Simba na alikuwa anafahamiana na wapenzi wengi wa Simba wakaongea nae aje anishawishi nikacheze mechi halafu badae tutaongea. Nilikubali kwasababu yake.

Lakini nilikuwa sina kitu, miezi mitatu nilikuwa nimekaa tu, hata kula wala kwenda mazoezini ilikua ngumu kipindi hicho.

Shaffihdauda.com: Ulikua unalipwa shilingi ngapi na Simba kipindi hicho kama mshara?

Ndikumana: Laki tatu (huku akicheka).

Shaffidauda.com: Sasahivi unalipwa mshahara kiasi gani huko Angola?

Ndikumana: Zaidi ya dola 15,000 za kimarekani kwa mwezi.

Shaffihdauda.com: Changamoto gani ulikutana nazo ukiwa unacheza soka Ulaya (Norway) na kuamua kurudi tena kucheza Afrika ?

Ndikumana: Nilikutana na ugumu fulani kucheza kule kama hali ya hewa watu wanavyojituma, mazingira ya timu ni vitu kama hivyo.

Shaffihdauda.com: Unawaambia nini wachezaji ambao wakiulizwa ndoto zao ni kucheza wapi wanasema Ulaya ?

Ndikumana: Kucheza soka Ulaya sio kitu chepesi, unatakiwa ujipange na uwe mvumilivu. Kwasababu mimi nilipoenda Norway nilikutana na changamoto ya baridi, ikawa ngumu sana mwanzo lakini tukawa tunaambiwa tutazoea. Sisi wenyewe tulikuwa tunaomba turudi nyumbani lakini wakawa wanatusisitizia tuvumilie tutazoea.

Wakatupa muda wa miezi mitatu wakasema kilakitu kitakua shwari, tukakomaa na mazoezi badae tukaanza kuizoea hali ya hewa baada ya kuzoea mambo yakaenda sawa.

Wasifu wa Selemani Ndikumana

Jina kamili: Selemani Yamin Ndikumana

Tarehe ya kuzaliwa: 28 Machi, 1987 (miaka 28)

Mahali alipozaliwa: Bujumbura, Burundi

Urefu: 1.86 m (6 ft 1 in)

Klabu anayochea sasa: Primeiro de Agosto (Angola)

Anavaa jezi namba: 17

Alianza kucheza soka: 2003-2006  timu ya vijana (AS Inter Star)

Timu ambazo ambazo amewahi kuzichezea:

2006–2007 Simba 36 (19)
2008 Molde FK 1 (0)
2009–2010 Lierse S.K. 13 (1)
2010–2011 Fantastique Bujumbura ? (?)
2011–2012 APR FC ? (?)
2012 Shenzhen Ruby ? (?)
2013 Al-Merrikh ? (?)
2013 Vital’O FC ? (?)
2014–2015 KF Tirana 42 (12)
2015 1º de Agosto    

Timuu ya taifa

2006– Burundi 47 (13)

Comments

comments