Home Kitaifa HIKI NDIO KIKOSI CHA TAIFA STARS KITAKACHOPAMBANA NA SWAZILAND

HIKI NDIO KIKOSI CHA TAIFA STARS KITAKACHOPAMBANA NA SWAZILAND

1148
0
SHARE

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland itakayochezwa Novemba 16 mwaka huu jijini Mbabane.

Akizungumza Dar es Salaam, leo (Novemba 5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na siku hiyo hiyo jioni kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.

Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika Kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba 13 mwaka huu kwenda Swaziland.

Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO, Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).

WADAU KUBUNI JEZI MPYA YA TIMU ZA TAIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
*
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja).

Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713 210242 au 0714 634838.

MPANDA UTD, UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.

Mechi hiyo ya kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Kundi B mechi za ufunguzi ni kati ya Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku Bulyanhulu FC ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga.

Abajalo FC ya Dar es Salaam itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.

Kundi D mechi tatu za ufunguzi ni kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji, Songea), Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda FC dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here