Home Kitaifa BAKHRESA, BINSLUM WANAVYOTUMIA UBONGO WA KEVIN O’LEARY KUFUNGA MAGOLI MAWILI KWA ...

BAKHRESA, BINSLUM WANAVYOTUMIA UBONGO WA KEVIN O’LEARY KUFUNGA MAGOLI MAWILI KWA SHUTI MOJA.

1309
0
SHARE

“Kitu cha kwanza na muhimu kwenye vita ni pesa,Pesa inamaanisha vitu vingine vyote,Askari,bunduki na risasi”.Maneno ya hekima ya miongoni mwa wanawake majasiri kuwai kutokea Duniani.Ida Tarbell,Mwalimu na mwandishi wa habari za siasa wa zamani wa marekani.Miaka sabini sasa tangu Mungu amchukue,Lakini maneno yake yanaishi mpaka leo.Pesa ndio kila kitu bwana.Tafuta pesa kwanza,Vingine vitatengenezwa na pesa uliyopata.Pesa ni silaha kuu ya kumshinda adui yako.Hakuna kitu bora kinachoendeshwa bila pesa.Kwa ufupi Pesa ndio alama kuu ya mafanikio.Hata kwenye soka pesa inacheza zaidi kuliko miguu ya wachezaji.
Mpira wa leo umetawaliwa na watu wenye pesa zao, Lakshmi Mittal, Alisher Usmanov, Roman Abramovich ni miongoni mwa mabilionea Duniani wanaomiliki na kudhamini vilabu mbalimbali kwenye ligi kuu ya England. Ligi ya uingereza inapendeza kutokana na mchango wa vigogo hawa wenye pesa zao.Bila jeuri ya pesa kusingekuwa na ubingwa wa Chelsea wala Manchester City.Makombe ya Chelsea yamenunuliwa na Pesa chafu za Roman Abramovich,Pesa hizo hizo ndio zimeleta mapinduzi ya soka nchini Uingereza.Ni jambo la kawaida sasa kuona vilabu vikongwe uingereza Liverpool na Manchester united vikitupwa mbali na mbio za ubingwa.Hakika pesa imetengeneza ligi kuu ya uingereza.
Patrice Motsepe, Kaizer Motuang, Moise Chapwe, Irvin Khoza ni miongoni mwa wamiliki wa vilabu maarufu barani Afrika.Pia watu hao ni miongoni mwa matajiri wakubwa Afrika.Ukiachana na Moize Chapwe waliobaki watatu yaani Patrice Motsepe, Kaizer Motuang, Irvin Khoza wote wanamiliki na kudhamini vilabu vya nchi ya Afrika kusini.Kwanini ligi kuu ya Afrika kusini isiwe ligi bora barani Afrika?.Pesa za kina Patrice Motsepe, Kaizer Motuang, Irvin Khoza ndio chagizo kubwa ya ligi hiyo kua bora na yenye mvuto kwenye bara letu pendwa la Afrika.
bakhresa

Hakika tangu kuzaliwa kwangu sijawai kuona ligi ya Tanzania inapendeza kama miaka hii miwili ya karibu.Mvuto wa ligi unaongezeka kadiri miaka inavyosonga.Ligi kuu ya mwaka jana ilikua nzuri kuliko ya mwaka juzi,pia bila shaka ya mwaka huu mpaka ilipofika inaelekea kunoga kuliko ya mwaka jana.Nyuma ya kuimalika kwa ligi hii kuna watu na pesa zao wamesimama.Wapo wengi ila leo napenda kuutambua mchango wa Bakhresa na Binslum.Kama ningekuwa tff ningeandaa tuzo kwa ajili ya watu hawa.Bakhresa na Binslum ni mikongoni mwa matajiri wachache wenye mapenzi ya dhati na mpira wetu.Hawa watu bila shaka wana malengo ya dhati kukuza soka la Bongo.Kaizer chief, si timu kongwe kama Simba na Yanga,ila ni timu bora kuliko simba na Yanga.Kaizer Motuang alipata maono ya kuanzisha kaizer chiefs mwaka 1970,Bakhresa alivyoanzisha Azam ni kama Kaizer alivyoanzisha Kaizer Chiefs.Mapinduzi ya soka la Afrika Kusini yalianzia kwa Kaizer chiefs kama Tanzania yalivyoanzia kwa bakhresa.Licha ya bakhresa kumiliki timu ya azam pia tajiri huyo ametoa udhamini kwa klabu zote zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara.Pesa za bakhresa zimehamasisha miguu ya wachezaji wengi wanaoshiriki ligi kuu.Pesa zake zimepunguza ukata uliokua unazikabiri timu zisizo na wadhamini.Hakika pesa za Bakhresa zinacheza ligi kuu yenye mvuto.Ukiachana na Bakhresa kuna mtu anaitwa Binslum, Binslum ametumia zaidi ya million 450 kuwekeza kwenye soka.
naye amefanya kwa sehemu yake.Ametoa udhamini wa vilabu vitatu Tanzania bara,Tena kati ya vilabu hivyo vitatu ,viwili ndio kwanza vimepanda ligi kuu msimu huu.Stand united na Ndanda zimepanda ligi kuu huku zikijihakikishia mamilioni kutoka kwa bakhresa na Binslum.Hii ni tofauti na zamani timu inapanda daraja inakosa hata pa kuanzia,Jambo hili lilipelekea timu kubwa kutumia udhaifu wa timu ndogo kupenyeza kirusi kinachoitwa rushwa.Hata kama Binslum na Bakhresa hawajamaliza tatizo la rushwa lakini watakua wamepunguza kwa asilimia kubwa.
binsl

Kama kungekua na bakhresa watatu na binslum watano hakika ligi yetu na soka letu kwa ujumla lingekua mbali. “Hivi ndivyo nnavyofikiri kuhusu pesa yangu,pesa yangu ni kama askari,nawatuma vitani kila siku nataka iende ikakamate mateka na kuwarudisha nyumbani”.Maneno ya bilionea jeuri Duniani,Raia wa Canada Kevin O’Leary. Matajiri na Makampuni makubwa inabidi wajifunze kuwekeza na kujitangaza kupitia soka.Soka ni biashara nzuri,Bakhresa, Patrice Motsepe, Kaizer Motuang, Moise Chapwe na Irvin Khoza wanajua umuhimu wa kutumia askari pesa kupata mateka(faida) kwenye vita ya soka(biashara).Bila shaka Bakhresa na Binslum walimuelewa vizuri Kevin O’Leary.
Licha ya Bakhresa na Binslum kusaidia soka letu bali pia na wao kuna faida wanapata kupitia kutangaza biashara zao.Watanzania wengi wanapenda soka,Bidhaa za Binslum na Bakhresa zinapendwa na watu wengi kwasababu ya kujitangaza kwao haswa kupitia soka. Wito wangu kwa matajiri na makampuni makubwa kuamka na kuanza kuwekeza kwenye soka.Uwekezaji wao kwenye soka utakua na faida kwa Taifa lao pia na kwao binafsi.Bakhresa na Binslum wanapiga shuti moja na kufunga magoli mawili,yaani wanatumia pesa zao kwenye soka kufunga magoli mawili,la kwanza wanafunga kwa soka la Tanzania na la pili kwenye biashara zao.Tusiwaache Binslum na Bakhresa pekee wafaidi akili za Kevin O’Leary kwenye vita(biashara) ya soka la Bongo.Tusiwaache watu hawa watumie peke yao ubongo wa Kevin O’Leary kufunga magoli mawili kwa shuti moja.
Na
Allen kaijage
0655106767
kaijagejr@gmail.com

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here