Home Kitaifa KAMBI YA AFRIKA KUSINI ITAWASAIDIA SIMBA SC

KAMBI YA AFRIKA KUSINI ITAWASAIDIA SIMBA SC

1284
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole,

Timu ya Simba SC imeelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya wiki moja. Ikiwa imekusanya pointi tatu katika michezo mitatu ya kwanza msimu huu katika ligi kuu ya Tanzania Bara, timu hiyo itakuwa J’burg kwa siku kadhaa ili kujiwinda na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa soka la Tanzania, timu ya Yanga SC mwishoni mwa wiki ijayo.

Presha ni kubwa kwa mabingwa hao mara 19 wa zamani, safari hiyo imelenga kuiandaa timu katika hali ya utulivu hasa wakati huu kuelekea mchezo dhidi ya ‘ Watani wao wa Jadi’. Simba haijaifunga Yanga katika misimu miwili iliyopita, mara ya mwisho walishinda, Mei 7, 2012, wamepoteza mara moja katika michezo minne iliyopita dhidi ya Yanga na mara tatu wamefanikiwa kupata sare.

Kiwango kidogo kutoka kwa wachezaji wazoefu kimeambatana na majeraha mfululizo kwa baadhi ya wachezaji muhimu, lakini kubwa zaidi ni uchezaji wa kutoridhisha katika safu ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao manne katika uwanja wa Taifa. Majina makubwa yamekuwa ni majanga kwa timu hiyo kocha, Patrick Phiri amekuwa na hofu ya majeraha katika siku za karibuni, golikipa namba moja, Ivo Mapunda, kiungo, Pierre Kwizera, mshambulizi, Paul Kiongera wote hao wapo nje ya uwanja wakiuguza majeraha yao tofauti.

Mganda, Emmanuel Okwi ambaye amesajiliwa kwa mara ya pili msimu huu akitokea kwa mahasimu wao Yanga tayari amefunga bao moja katika michezo mitatu iliyopita, Okwi amekuwa akichezeshwa sambamba na Amis Tambwe katika safu ya mashambulizi. Kambi ya Afrika Kusini inaweza kuwahimarisha wachezaji hao wa kimataifa na kufanya kazi kwa ushirikiano.

Beki wa kati na nahodha wa timu hiyo, Joseph Owino amekuwa na kiwango kibovu msimu huu ,Licha ya Phiri kuwa na wasiwasi na kiwango cha sasa cha Mganda huyo, Simba imepania kuhakikisha inashinda katika mechi ijayo dhidi ya Yanga ndiyo maana wamekwenda nje ya nchi kufanya maandalizi yenye utulivu na kuwasahulisha wachezaji kuhusu matokeo yaliyopita.

Safari bado ni ndefu msimu huu, kuna mambo yatakuja kutokea. Unaweza kuwa na hatua ngumu mwanzoni mwa msimu na kufanya vizuri kadri ligi inavyokuwa ikiendelea. Majeraha ni bahati mbaya waliyoanza nayo Simba hali inayofanya watoe maswali mengi kuliko majibu kutokana na matokeo yasiyotarajiwa ambayo tayari timu hiyo imeyapata.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here