Home Kitaifa SIMBA YAVUNJA REKODI YA YANGA DAR

SIMBA YAVUNJA REKODI YA YANGA DAR

947
0
SHARE

REKODI zinaonyesha kwamba Simba  haijawahi kushinda kesi ya kumwania mchezaji yeyote kati yake na Yanga au Costal Union kwa takribani miaka 20.

Mara kadhaa timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam imejikuta ikibwagwa katika vita ya kugombea mchezaji kati yake na klabu hizo, lakini hukumu za wachezaji Emmanuel Okwi na Abdul Banda zilizotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF Jumapili iliyopita kwa mara ya kwanza imewapa  Simba ushindi dhidi ya Yanga na Coastal Union.

Hapa chini ni baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kugombewa na timu hizo dhidi ya Simba.

Mtemi Ramadhani Mwaka 1980;

 Simba ilimgombea kiungo huyo na Yanga. Mchezaji huyo alikuwa akichezea Waziri Mkuu ya  Dodoma  lakini alijikuta akisajili katika timu za Simba na Yanga.

Akiwa na Taifa Stars iliyokuwa imekwenda Nigeria kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), Mtemi alizua balaa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati Stars walipokuwa wakirejea.

Viongozi wa Simba na Yanga na wale Pan African walikuwa kiwanjani hapo kuwalinda wachezaji waliowasajili na kuwafanya washikane mashati.

Mbali na Mtemi,Yanga pia walikuwa wakimgombea, Rashid Idd ‘Chama’  waliokuwa wamemsajili wao pamoja na Pan African.

Chama cha Mpira wa Miguu (FAT, sasa TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Said El Maamry waliwawataka wachezaji hao kuchagua timu za kuchezea.Mtemi alichagua kuchezea Simba na Chama aliichagua Pan African lakini Yanga hawakukubali wakakata rufaa Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

BMT iliamua kuwafungia wachezaji hao kwa mwaka mmoja, baada ya hapo Mtemi alirudi Waziri Mkuu na baada ya msimu mmoja akajiunga na Simba. Chama naye aliendelea kuchezea Pan African.

Yussuf Bana; Mwaka 1981

Simba ilimgombea beki Yussuf Ismail Bana katika vita na Yanga. Beki huyo alicheza Simba  msimu mmoja tu na kuamua kujiunga na Yanga mwaka 1982 kitu kilichozua utata mkubwa. Inadaiwa, Yanga ilimsajili  kwa jina lake halisi la Yussuf Ismail na Simba walimsajili kwa jina la Yussuf Bana ambalo lilidaiwa kuwa ni jina la la  utani.

Baada ya vita ya chinichini hatimaye, Bana ambaye kwa sasa ni marehemu aliruhusiwa kuchezea Yanga.

Francis ’Fura’ Mwikalo;

Simba ilipoteza matumaini ya kunyakuwa ubingwa wa Tanzania Bara  mwaka 1985/86 baada ya kumsajili mchezaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, Francis Mwikalo.

Katika kutaka kuonyesha kwamba mchezaji huyo alikuwa ni tofauti na Mwikalo wa Coastal Union, Simba walimbadilisha jina na kumsajili kwa jina la Fura Mwikalo.

Sakata la mchezaji huyo lilikuwa kubwa sana na kufikia hatua ya kuamuliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jijini Dar es Salaam. Siku ya hukumu, mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba walifika mahakamani  wakiwa na  ngoma ya Kizaramo aina ya Mdundiko wakiamini kwamba watashinda kesi hiyo na kutangazwa kuwa mabingwa.

Baada ya hukumu kutolewa na Simba ilibwagwa na kupoteza pointi zote walizomchezesha Mwikalo ambaye awali walidai kuwa walimsajili kutoka Muheza Shooting ya Tanga.

Athuman Idd ‘Chuji’;

 Yanga iliiwaduwaza tena watani zao kwa kumnyakuwa beki wa  zamani wa Polisi Dodoma, Athumani Idd Chuji ambaye aliikacha Simba katika hatua za mwisho mwaka 2006.

Pamoja na Mwenyekiti wa Simba wakati huo, Hassan Dalali kudai kwamba Chuji hatacheza soka, mchezaji huyo alisema ni heri akauze ndimu kuliko kurudi Simba.  TFF ilimwidhisha kuchezea Yanga. 

Mbuyu Twite;

 Agosti, 2012  aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisafiri kwenda DR Congo kumsajili beki Mbuyu Twite. Hata hivyo, Yanga waliwazidi akili na kumsajili beki kwa kile kilichoelezwa kwamba Simba walishindwa kufuata sheria za usajili.

Simba ilidaiwa kukurupuka bila ya kufuata sheria za CAF na Fifa, hivyo TFF kumwidhinisha kuchezea Yanga.

Kelvin Yondani;

 Mwaka huohuo, Simba ilipata pigo lingine kubwa baada ya beki wake wa kati Kelvin Yondani kusajiliwa na Yanga.

Awali, Yondani aliondoka Simba na kwenda kujichimbia Mwanza ambako alipoibuka alitua Jangwani kwa  dau la  Sh30 milioni.

Pamoja Rage kudai kwamba Yondani asingeweza kucheza soka TFF ilimwidhinisha mchezaji huyo kukipiga Yanga.

Mrisho Ngassa;

Baada ya kumchukua kwa mkopo kutoka Azam, Simba walimwongezea Ngassa usajili wa mwaka mmoja na kumpa gari pamoja na Sh25 milioni.

Msimu wa kutolewa kwa mkopo Simba ulipoisha, Yanga ilimsajili Ngassa kwa ada ya Dola 30,000.Simba hawakukubali, lakini TFF ilimwidhinisha Ngassa kuchezea Yanga na kumtaka kurudisha fedha za Simba alizopewa, piaalifungiwa  michezo sita.

Iliwabidi Simba kusubiri hadi Jumapili iliyopita kuibadili kibao.

Chanzo: Mwanaspoti

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here