Home Kitaifa WANANDINGA SIMBA, YANGA, AZAM FC, MBEYA CITY FC…..KOMBE LA DUNIA LIWE DARASA

WANANDINGA SIMBA, YANGA, AZAM FC, MBEYA CITY FC…..KOMBE LA DUNIA LIWE DARASA

1314
0
SHARE

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
FAINALI za kombe la dunia zimeanza kutimua vumbi jana nchini Brazil kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Croatia.
Mabao mawili ya Neymar na moja la Oscar yalitosha kumpa usingizi Luiz Felipe Scolari pamoja na wabrazil wote waliofurika uwanjani kuwashuhudia vijana wao wa `Samba`.
Marcelo aliizawaida bao Croatia ya akina Dravko Logarusic wa Simba sc baada ya kujifunga katika hekaheka za kuokoa mpira wa krosi.
Michuano hii ni mikubwa zaidi katika ulimwengu wa soka na inawakutanisha wachezaji wengi wa viwango vya juu duniani.
Mashabiki wa soka dunia wakiwemo Watanzania wanafuatilia kombe la dunia. Wengine wamebahatika kwenda Brazil na waliowengi wanafuatilia kwa njia ya luninga.
Siku zote kuwaangalia wengine ni njia ya kujifunza. Ukiona nchi fulani imefanikiwa katika soka na kucheza fainali za kombe la dunia, basi ujue wana mipango sahihi ya soka.

Nyota wa Simba, Ramadhani Singano 'Messi' Ramadhan Singano (Simba sc)  anatumia jina kubwa la Lionel Messi anayeichezea Barcelona na timu ya taifa ya Argentina

Hili linatakiwa likupe changamoto zaidi na kutafakari namna ya kujiendeleza ili uwafikie wao. Inaweza isiwe leo wala kesho kulingana nao, lakini ni muhimu kujifunza.
Uzuri fainali hizi zinaangaliwa na wachezaji wa mpira, makocha, viongozi na mashabiki.
Tanzania ni taifa linalochechemea katika mpira wa miguu. Safari imekuwa ndefu na timu yetu imekuwa tia maji tia maji. Kuna jitihada zinafanyika wala hatutakiwi kuzibeza, lakini haizuii kusema bado hatuna mipango mizuri katika soka
Jambo moja linalonivutia kwa watanzania wengi ni kuwa na matumaini na mambo yao, lakini kuna watu wachache wanaharibu mipango.
Uongozi ni tatizo kubwa mno. Mpira wa Tanzania unakosa viongozi wenye utashi wa kimaendeleo. Wanatumia muda mwingi kufanya mambo yasiyoweza kutufanikisha na kusahau kujenga mifumo sahihi ya mpira.
Ukiwatazama wachezaji wa Tanzania na ukahojiana nao, hakika wanaonekana kuwa na matumaini ya kufika Ulaya, lakini wamekosa vitu vingi mno vya kiufundi. Na hii inatokana na taifa kukosa misingi ya soka la vijana.
Kombe la dunia limeanza, kuna vipaji vingi. Kuna wachezaji wenye umri mdogo kama ilivyo kwa wachezaji wa Tanzania katika klabu za Simba, Yanga, Azam fc, Mbeya City fc na nyinginezo.
Simba na Yanga ndio klabu zenye mvuto zaidi kwa soka la Tanzania. Azam fc na Mbeya City pia zinafuatia, lakini haziwezi kugusa hata robo ya Simba na Yanga.
Wachezaji wengi wanapenda sana kucheza Yanga na Simba. Hakina ni heshima kwa mchezaji kuzichezea timu hizi mbili.

CANANadir Haroub anatumia jina la Cannavaro aliyewahi kutamba miaka ya nyuma

Leo hii nataka kuwakumbusha wachezaji kitu kimoja tu wakati huu wa fainali za kombe la dunia.
Najua wachezaji wengi wapo likizo na wana muda wa kutosha kutazama fainali za kombe la dunia. Zinapochezwa ligi za Ulaya, hata ligi yetu inakuwa inaendelea, hivyo wachezaji wanakuwa kwenye majukumu mazito , lakini sasa wengi wana muda wa kutosha.
Nazungumza na ndugu zangu wa kibongo wanaopenda kujibebesha majina ya wachezaji wakubwa duniani, lakini wanashindwa kuonesha hata robo ya watu wale.
Imekuwa kawaida kwa wachezaji kujiita majina ya wachezaji wa Ulaya na wakati mwingine wanabatizwa majina hayo na mashabiki wao, sina hakika kama wanaangalia aina ya uchezaji au ni mapenzi binafsi tu.
Nafurahia sana nikisikia mtu anajiita Lionel Messi, Cristiano Ronaldo au jina lolote kubwa. Wakati fulani wachezaji wanatumia majina ya wachezaji waliofanya makubwa duniani kwa miaka ya nyuma na wengine miaka ya sasa kama vile akina Canavaro, Boban, Vidic, na mengineyo.

Yanga YondanKelvin Patric Yondani anatumia jina la Mserbia Nemanja Vidic

Ni jambo jema kujiita au kuitwa jina la mtu mkubwa. Nakumbuka wakati nacheza soka la mchangani nilikuwa najiita Zinedine Zidane na mashabiki wangu walikuwa wananifahamu kwa jina hilo.
Nilimpenda sana Zidane na kila anapocheza nilikuwa namfuatilia kwa vitu vingi, lakini nilishindwa kutumia mambo yake kivitendo. Kinadharia nilijifunza mengi kutoka kwake, ilipofika uwanjani, nilikuwa nachemka kucheza kama yeye.
Halikuwa tatizo kwangu, lakini nilijifunza vya kutosha kutoka kwa Zidane ambaye kwasasa ni kocha msaidizi wa Real Madrid.
Wachezaji wa Tanzania huu ni wakati wenu wa kujifunza kwa wale watu mnaowapenda kwasababu wapo Brazil kwenye fainali za kombe la dunia na ninyi mna muda wa kutosha sasa. Sijui mnafanya nini, lakini naamini mnatazama kombe la dunia. Kama haiko hivyo basi hiyo ni ajabu kubwa mno.
Ni jambo jema kujifunza kwa kuiga. Ni muhimu sana kuwaangalia wachezaji wakubwa kwenye luninga. Kumtazama mwingine ambaye ana mafanikio makubwa kuliko wewe ni njia nzuri ya kujifunza.
Kuwaangalia wachezaji wakubwa kutakufanya ujue namna mpira unavyochezwa na kukuongezea ubora.
Kama unacheza nafasi fulani, tumia muda mwingi kuwatazama wachezaji wanaocheza nafasi yako ili kuchukua vitu muhimu kutoka kwao. Pia angalia kwa makini maamuzi ya waamuzi ili ujue makosa ya mpira.

JOHNBOCCO1John Raphael Bocco yeye aliamua kutumia jina la Mwafrika mwenzake, Emmanuel Adebayor  wa Togo na Tottehham ya England

Kama wewe ni beki, tumia muda wako kuwatazama mabeki, kama wewe ni kiungo basi komaa na viungo na kama wewe ni mshambuliaji basi kazania kuwaangalia washambuliaji, unaweza kutoka na kitu kizuri.
Itumieni michuano ya kombe la dunia kujifunza mpira kutoka kwa wachezaji wakubwa ili ligi ikianza wale wenye majina ya wachezaji wakubwa angalau waonekana kuwa na vitu vipya.
Sisemi uwe kama Messi kabisa au Ronaldo au Neymar, bali uwe angalau na kitu kidogo kumuhusu mchezaji unayempenda na pengine kutumia jina lake.
Pia wakati huu wa mapumziko, nendeni kwenye makitaba kusoma vitabu vinavyohusu soka. Kuna vitabu vizuri sana na mojawapo ni kitabu cha “Soccer for Dummies”. Hiki ni kitabu kizuri na kinaweza kuwasaidia wengi. Kupata taarifa na maarifa ya juu ya kile ukipendacho ni jambo jema.
Mkirudi kwenye michuano ya ligi kuu onesheni mliyojifunza, lakini msisite kuomba ushauri kutoka kwa makocha wenu. Ni rahisi kujua makosa kwa kukaa na mtu anayekutazama muda mwingi.
Mbali na kupata ushauri kutoka kwa makocha wenu, kumbukeni kufuata ratiba ya mazoezi. Kufanya mazoezi mara 3-4 kwa wiki kutawafanya muwe bora.
Kila la kheri katika kutazama kombe la dunia nchini Brazil.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here