Home Kitaifa HILAL ABEID: MATATIZO YA SIMBA SC NI WANACHAMA WENYEWE WA KLABU

HILAL ABEID: MATATIZO YA SIMBA SC NI WANACHAMA WENYEWE WA KLABU

1482
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole
WAKATI baadhi ya wanachama wa klabu ya soka ya Simba wakihitaji kukata rufaa ngazi ya juu zaidi kupinga uamuzi wa Michael Wambura kurudishwa kuwania nafasi ya urais wa klabu ya Simba katika uchaguzi mkuu, juni 29, mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Hilal Abeid amesema kuwa ni wakati wa wanachama wa klabu hiyo kuamka na kwenda kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ambao utawaingiza madarakani viongozi wapya kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Alizungumza kwa kirefu wa mtandao huu siku ya jana jumanne, hivyo msomaji wetu unaweza kupata mawazo mapya kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ambao unataraji kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
SWALI; Nini mtazamo wako kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba SC?
HILAL: “Watu wanazitumia Simba na Yanga kutaka umaarufu wao. Zimekuwa klabu ambazo mtu akitaka umaarufu anaingia tu pale. Anakuwa pale kwa madhumuni yake, apate umaarufu pia kutafuta pesa wakati mwingine. Hakuna mtu ambaye hasa ana nia ya kukaa pale na kuendeleza mpira. Nawalenga hasa hao watu kama wakina Azim Dewji wote ni wababaishaji tu.”
SWALI; Nani mwenye wajibu huo sasa, na unafikiri sakata la Wambura linabeba ujumbe gani”
HILAL; “ Mimi nimefurahi kuona Wambura amerudishwa katika uchaguzi. Na sisi kama wanachama tutaamua ni nani hasa anayeweza kutufaa kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Wambura ana kazi kubwa kuwashinda hawa watu. Huu ni wakati wa kuzungumza ukweli, sasa kila upande utaandaa mashambulizi lakini yawe ya kisera zaidi na hoja na mtazamo wa mgombea vitapewa kipaumbele”

SWALI; Unafikiri Simba inahitaji kiongozi wa aina gani kwa wakati wa sasa?

HILALI; “ Tusimuweke mtu ambaye atawanyamazisha wanachama kwa kuwafunga Yanga au kuchukua ubingwa wa ligi kuu. Kwa kuwahadaa wanachama kwa kuwaletea kocha mzungu ambaye hata kama hajui mpira kwa kuwa ametoka ulaya, au kuchukua mchezaji ‘ wanasema mchezaji kifaa’ sijui kutoka Kenya, Uganda ili kuwaonesha wanachama wamefanya kitu”
SWALI; Unafikiri viongozi wanaokuwa wakipewa nafasi huwa na mtazamo wa kuifanya Simba kujitegemea?
HILALI; “ Baada ya hapo, magazeti, jezi, mabango ya klabu vitu hivi ni vingapi na vinakwenda wapi?. Hivyo tunataka mtu ambaye anaweza kutusaidia katika udhitibi wa vyanzo muhimu vya mapato vya klabu, ili iweze kujitegemea. Mimi nimecheza mpira tangu mwaka 1969 wakati huo ikiitwa Sunderland. Alafu timu ikabadilishwa jina kutoka Sunderland hadi Simba na nikacheza pale hadi mwaka 1973. Mimi ni mchezaji wa pili wa Tanzania kucheza mpira wa kulipwa nje ya nchi. Sasa nakwambia viongozi wa miaka ya karibuni wanaingia kuongoza Simba kwa malengo ya ‘ kuchuma’ huku wakiwadanganya wanachama kwa kuwafunga Yanga, kuleta kocha wa kigeni au kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi hakuna zaidi ya hapo”

IMG_4521
SWALI; Unawaambia nini wanachama wa klabu ya Simba?
HILAL; “ Kuelekea uchaguzi huu niliwafuata wale Simba Taliban nikawaambia kuwa matatizo ya Simba siyo mtu mwingine yoyote zaidi ya Wanachama wenyewe wa klabu. Matatizo ya Simba ni wanachama na siyo viongozi. Niliwaambia wazi kuwa kama ‘ mimi nikisimama katika uchaguzi bila kupita kwao na kuwapa hata senti moja hamtanichagua’. Nikawaambia mtamchagua mtu ambaye atawapeni shilling 5000, hadi 50, 000. Mtu akichaguliwa anaingia pale anafanya mambo yake anawafurahisheni ninyi kwa kuwafunga Yanga au kuchukua ubingwa, basi.”
SWALI; Unafikiri, Simba inaweza kutoka katika utegemezi wa kiuchumi?
HILAL; “ Tukitaka timu hii ifike kama Zamalek ya Misri, El Hilal ya Sudan, El Meirrikh ya Sudan, klabu iwe na uwanja wake kama ilivyo timu hizo. Timu hizi zina clinic zao, viwanja vyao, miradi yao ni klabu zinazojiendesha zenyewe. Sisi tuna miaka 78 tupo vilevile tu. WAkati fulani nikiwa nacheza mpira Uarabuni kuna kikundi cha watu fulani kiliamua kujitoa katika timu na kuanzisha Nyota Nyekundu. Baada ya muda mfupi Nyota Nyekundu walijenga timu, na wakajenga jengo la maana tu pale Kariakoo. Walijenga ghorofa zuri, upande wa pili kwa watani zetu Yanga pia kikundi cha watu kiliamua kujitoa Yanga na kuanzisha timu ya Pan Africans. Pan Africans ilifanya vizuri na hadi sasa wana jumba lenye thamani ya mabillioni pale Mtaa wa Swahili na Odoyo, kariakoo”
SWALI; Kuna tofauti gani kati ya Simba ya miaka ya 1960 hadi miaka 1970 wakati wewe ukicheza soka?
HILALI; “ Uongozi wa zamani walifanya vitu ambavyo tunaviona hadi sasa, kulikuwa na migahawa ya klabu lakini yote imeuzwa. Tujiulize kwa miaka mingapi hali hiyo ilivyo, vingozi wa miaka ya karibuni wamefanya nini? Klabu kubwa kama Simba inashindwa hata kuwa na clinic yake ya kuwatibu wachezaji. Simba inahitaji viongozi ambao wanakuwa na uwezo wa kutafuta njia ili klabu ijitegemee, na si klabu kuwategemea watu., au kutegemea kikundi cha watu. Itazame leo, Yanga inaendeshwa na mtu kama Yusuf Manji, kila anachofanya sasa hivi watamsikiliza watake wasitake, hawana kitu. KLabu haina kitu. Viongozi wengine hawana kitu na Yanga haina kitu, hivi tutakwenda mpaka lini, mpira hauwezi kuendelea kwa mtindo huu”
Ahsante sana
HILAL; Asante pia kwa kunipa nafasi hii
0714 08 43 08

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here