Home Makala YANGA MNATAKA KUTUKUMBUSHA `UHONDO` WA MARCIO MAXIMO, NI KOCHA BORA ANAYEWEZA KUWAFAA...

YANGA MNATAKA KUTUKUMBUSHA `UHONDO` WA MARCIO MAXIMO, NI KOCHA BORA ANAYEWEZA KUWAFAA JANGWANI

1244
0
SHARE

maximo+2Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976
YANGA SC ipo katika mchakato wa kusaka kocha mkuu ili kuziba pengo lililoachwa wazi na Mholanzi, Hans Van der Pluijm aliyetimkia Saudi Arabia baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Hata hivyo, Pluijm alikuwa na mkataba mfupi wa miezi sita na baada ya kumaliza, hakuona haja ya kuongeza kwa sababu alikuwa amepata kazi mpya Uarabuni.
Namna ambavyo Pluijm aliondoka Yanga, lilikuwa jambo jema kwasababu walikaa meza moja, wakaongea, akawaeleza nia yake ya kutaka kuondoka na viongozi wa Yanaga wakabariki.
Aliondoka `kiroho safi` na hakukuwa na tatizo lolote baina yake na viongozi wa Yanga. Pluijm alifika mbali na kuwaahidi Yanga kuwa atawasaidia kupata wachezaji nyota kutoka nchini Ghana alikofanya kazi miaka ya nyuma.
Kuondoka kwa Pluijm kumewalazimu Yanga kuhaha kusaka mrithi wake na jana katika mkutano wa mabadiliko ya katiba uliofanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi Osterbay jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa Yanga, Yufus Manji amesema Kamati ya Mashindano imemkabidhi mapendekezo yao na kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na Marcio Maximo aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania kuja kukinoa kikosi cha Jangwani.
Suala la Maximo kuhusishwa na mpango wa kurejea nchini kwa majukumu ya kuinoa Yanga halijaanza jana wala juzi. Tetesi hizi zilikuwepo mwaka 2012 ambapo alikuwa anatajwa kuja kurithi mikoba Mserbia, Kosta Papic, lakini kibarua kikaangukia mikononi mwa Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Hakika ujio wa Maximo kwa wakati ule ulivuta hisia za mashabiki wa Yanga na watanzania wengi waliokuwa na mapenzi makubwa kwa kocha huyo wakati alipokuwa anafanya kazi Taifa stars, lakini ndoto za wengi kumuona Marcio zilizima ghafla baada ya uongozi wa Yanga kumleta Saintfiet.
Sasa Yanga wapo katika jaribio la pili kumleta Maximo. Kama bosi mwenyewe ndiye ameshikilia suala hilo, kuna uwezekano mkubwa wa Brazil huyo kutua jangwani.
Juni 29, 2006, Maximo aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Tanzania, Taifa Stars. Uteuzi wa kocha huyo ulitokana na ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alisema serikali yake italeta kocha wa timu ya taifa ya Tanzania.

maximoMhe. Kikwete aliahidi kuliokoa soka la Tanzania na kusema serikali yake itakuwa inalipa mshahara wa kocha na mambo mengine ya msingi. Alifanikisha dhamira yake baada ya kumleta Maximo kutoka nchi inayonukia soka, Brazil.
Wakati Maximo anakuja Tanzania, Taifa Stars ilikuwa hofi bin taabani. Soka letu lilikuwa bovu na mashabiki wa soka walikuwa wameshakata tamaa na timu yao.
Haikuwa rahisi kuwakuta mashabiki kwenye mechi za Taifa stars kwenye uwanja wa `Shamba la Bibi`. Kila kukicha kauli ilikuwa `Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu`.
Ni Maximo aliyekuja kuwaunganisha tena mashabiki wa soka nchini. Alifanya kazi ya kuiboresha Taifa stars kwa kiwango kikubwa. Timu ilipendwa chini ya Maximo. Mashabiki walifurika uwanjani na kuishangilia Taifa stars.
Maximo alifanya kazi kubwa na mwaka 2009 aliisaidia Taifa Stars kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN.
Fainali hizi zilifanyika nchini Ivory Coast kuanzia February 22 mpaka machi 8 mwaka 2009. Tanzania ilifuzu baada ya kuitoa Sudan kwa wastani wa mabao 5-2.
Wakati huo, mashabiki wengi walibadilisha mtazamo wao kuhusu timu ya taifa. Waliipenda na nyimbo mbalimbali zilitungwa kuwasapoti wachezaji na kumshangilia Maximo.
Baada ya fainali za CHAN, Maximo aliongeza mkataba wake na TFF mpaka mwezi julai 2010, lakini baadaye aliondoka na mikoba yake kuchukuliwa na Jan Borge Poulsen.
Kuondoka kwa Maximo kulichukuliwa kwa mitazamo tofauti. Wengine walisema kocha huyo ameishiwa uwezo wa kuisogeza mbele zaidi Tanzania. Yaani mbinu zake zimefika kikomo. Lakini wengine walipinga na kudai kocha huyo angepewa muda zaidi.
Desemba mwaka jana aliteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Brazili ya Democrata. Alifukuzwa kazi katika klabu hiyo desemba 13 mwaka 2012.

mpiraMwezi juni 2012 alikuwa kwenye tetesi za kumrithi Kosta Papic katika klabu ya Yanga, lakini kazi hiyo ilitua mikononi mwa Mbelgiji, Tom Sainfiet. Lakini mwezi novemba 2012 alichagua kukaa Brazil ambapo anaiongoza klabu ya Francana.
Tangu Maximo aondoke, Taifa Stars haijawa na mvuto kama kipindi chake. Watu wanaipenda timu, lakini huwezi kufananisha na kipindi kile.
Inawezekana Maximo alikuwa na mvuto kwasababu aliitoa timu shimoni na kuipandisha sehemu fulani, wakati wenzake waliikuta ikiwa sehemu fulani.
Marcio Maximo anaweza kutua nchini safari hii kwa majukumu ya ngazi ya klabu. Binafsi naona litakuwa jambo jema kwasababu ni kocha mzuri.
Uzuri wa Maximo kwa klabu ya Yanga na soka la Tanzania unatokana na mambo mengi, lakini machache kati ya hayo ni haya hapa;
Mosi: Ni Kocha mwenye mvuto kwa mashabiki; duniani kote, kocha akiwa na mvuto lazima atapendwa na mashabiki. Leo hii angalia Jose Mourinho anavyopendwa na mashabiki na waandishi wa habari. Kuna faida ya kocha kuwa na mvuto akiwa kazini. Hii inapandisha morali ya wachezaji na mashabiki katika kuisaidia timu.
Enzi zake akiwa Tanzania, Maximo alikuwa anazungumzwa kila kona. Alikuwa anaimbwa na mashabiki dakika zote uwanjani. Watu walimpenda kwa kazi yake. Hii ilisababisha muunganiko mkubwa kupitia jina lake. Hata waandishi wa habari walipenda sana kumhoji kocha huyu. Alijua kuongea na waandishi wa habari na alijua kucheza na maneno. Aliwatia hamasa mashabiki kwa maneno yake matamu na watu walifurika uwanjani kushuhudia matokeo ya maneno yake.
Mvuto ni jambo muhimu mno kwenye timu. Kama Maximo atakuja na kasi ile ya Taifa stars katika klabu ya Yanga, hakika mitaa ya jangwani itakuwa na shamrashamra kubwa wakati wa uongozi wake.
Pili; ni kocha mwenye msimamo mkali. Maximo ana falsafa yake ya kazi. Hataki hata siku moja kuingiliwa katika maamuzi yake. Unakumbuka alivyoweka ngumu kumuingiza Mrisho Ngassa katika kikosi cha Stars?. Watu waliongea mengi, lakini akasema siwezi kumuingiza mchezaji timu ya taifa kwa kumuangalia mechi moja tu. Lakini baadaye alipojiridhisha alimuita. Pia alizinguana na Juma Kaseja nchini Senegal alipofungwa mabao 4-0, kutoka hapo alisema hatamuita tena Kaseja na alifanya hivyo.
Msimamo wa Maximo umejikita katika nidhamu. Kama mchezaji hana nidhamu kwa mujibu wa vigezo vyake, hawezi kucheza chini yake. Kama atakuja Yanga, basi atawanyoosha baadhi ya wachezaji wasiokuwa na nidhamu. Maximo hana masihara katika kazi yake. Maamuzi yake ni magumu. Na viongozi wa Yanga wajipanga kumuacha afanye kazi yake.
Tatu; Maximo ni kocha anayejua mbinu ya kulinda lango lake. Enzi zake akiwa Taifa stars, safu ya ulinzi ilikuwa imara mno. Achana na kipigo cha mabao 4-0 alichopata nchini Senegal, Maximo hakuwahi kufungwa zaidi ya mabao 2 katika mechi zote za mashindano.
Alisuka safu bora ya ulinzi iliyosheheni wachezaji wenye nidhamu kubwa ya mchezo kama Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub `Canavaro`, Meck Mexime, Salum Swedi `Kussi`, Victor Costa `Nyumba` na wengineo.
Soka la kisasa linahitaji timu ijilinde, icheze mpira na kushambulia. Kanuni hii ndiyo inayotumiwa duniani kote. Ili timu ishinde, lazime ijilinde sehemu yake ya ulinzi, lazima imiliki na kucheza mpira na kushambulia ili kupata mabao.
Kama unashindwa kujilinda, utafunga lakini utafungwa zaidi. Ili kupata matokeo lazima uwe na safu nzuri ya ulinzi. Kwa aina ya mabeki waliopo Yanga kwa sasa, kama Maximo atapewa kazi na kukaa nao, Yanga inawezekana Yanga ikwa na safu bora mno ya ulinzi kwasababu ndio staili ya mwalimu huyo.
Nne; Maximo anaijua vizuri Tanzania, anajua utamaduni wa mashabiki wa Tanzania kwasababu alikaa muda mrefu nchini. Anajua namna ya kuwakonga nyoyo mashabiki na kuwakera mashabiki wa Tanzania.
Kutokana na uzoefu wake na soka la Tanzania, inakuwa rahisi kuendana na mfumo mzima. Kwa hili Maximo atafanikiwa na Yanga watakuwa chini ya kocha mzuri.
Pia Maximo ni mtu wa watu. Anajua kuishi na watu. Ndio maana aliigiza moja ya filamu nchini Tanzania. Haya yalikuwa mambo nje ya taaluma yake, anajua kukaa na watu na anapendwa na watu kila anapofanya kazi.
Yapo mambo mengi ambayo nitaendelea kukueleza kuhusu Maximo, lakini nimalizie makala hii kwa kutoa tahadhari kwa Yanga.
Maximo anaweza kuja Tanzania, hatukatai!, lakini lazima Yanga wajiandae kwa mambo mawili.
Maximo anaweza kufanikiwa au asifanikiwe. Mpira umebadilika na katika maisha ya ukocha kuna kushindwa pia.
Kocha anaweza kuwa na historia nzuri, lakini akashindwa kufanya vizuri kwasasa. Kwahiyo, Maximo anapokuja, mashabiki na viongozi wa Yanga wasitegemea makubwa. Anatakiwa kuaminiwa na kumuacha aweke mipango yake kwa mujibu ya falsafa yake ya ufundishaji. Yanga wasije kuwa na papara.
Kila la Heri Yanga katika mchakato huo wa kusaka kocha mpya. Kama mtafanikiwa kumleta Maximo,hakika mtatukumbusha mambo matamu ya Mbrazil huyu.

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here