Home Kitaifa MAONI YA MDAU IBRAHIM MKAMBA JUU YA SAKATA LA KUENGULIWA MICHAEL WAMBURA.

MAONI YA MDAU IBRAHIM MKAMBA JUU YA SAKATA LA KUENGULIWA MICHAEL WAMBURA.

785
0
SHARE

“Michael Wambura ameenguliwa kwenye uchaguzi wa Simba kwa kuelezewa kwamba si mwanachama halali baada ya kusimamishwa uanachama mwaka 2010 kwa kuifikisha Simba mahakamani. Tukiwa na dhamira ya kutenda haki, tutafakari haya:-
1) Mwaka ule 2010 Wambura aliomba Mahakama iwatake wanaodai yeye ni mchafu waileze Mahakama uchafu wake na wakishindwa basi yeye abaki kuwa msafi aendelee na uchaguzi. Kuulizia uchafu wako kwa mahakama kunahusiana nini na soka hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa akitajwa kuwamchafu bila kuelezwa uchafu wake?
2) Aliposimamishwa uanachama alipewa haki ya msingi ya kujieleza ikifahamika kwamba “audi alteram partem” (sikiliza pande zote za kesi) ni msingi mmoja mkubwa wa maamuzi ya haki? Je, alisimamishwa uanachama bila kupewa haki hiyo? Kama hakupewa haki hiyo kusimamishwa kwake ni batili.
3) Kwa kuwa mgogoro uliohusu kusimamishwa kwake ulihusu uchaguzi uliomhusisha Aden Rage. Je kwenye kikao cha kumsimamisha uanachama, Rage alikuwepo? Kama alikuwepo ina maana alikuwa mwamuzi kwenye kesi iliyomhusu wakati msingi mmoja mkubwa wa maamuzi ya haki ni “nemo judex in causa sua” (mtu asiwe jaji kwenye kesi inayomhusu). Kwa hiyo kusimamishwa kwake kunakuwa batili.
4) Baada ya kusimamishwa uanachama, Wambura hakufanya mambo yoyote yanayohusu uanachama wake kama kuhudhuria mikutano, kulipia ada nk ikiwemo kuchukua fomu za kugombea uongozi (zinazotolewa kwa wanachama tu)? Kama alifanya mambo hayo, ina maana impliedly uamuzi wa kumsimamisha uanachama ulikuwa umefutwa. Vinginevyo,angezuiwa asifanye lolote kati ya hayo kwa kusimamishwa uanachama.
5) Kwa kufuata kanuni ya Estoppel, kwa kumfanya Wambura aamini kwamba ni mwanachama halali, mamlaka ya Simba inazuiwa kutangaza kinyume chake kwani imemshawishi aamini kwamba ni mwanachama halali na yeye ametekeleza mambo yote mwananachama wa Simba anayopaswa kutekeleza ikiwemo kuchukua fomu za kugombea uongozi
6) Baada yakusimamishwa uanachama hakuna hatua iliyoendelea na hivyo kuzua utata wa endapo kusimamishwa huko kunaendelea au hapana na utata huo unaimarishwa na Wambura kuendelea kushiriki shughuli za Simba kama mwanachama. Katika suala lolote la kisheria, kukitokea utata, utata huo humnufaisha mlalamikiwa ambapo katika kesi hii aliyelalamika ni mamlaka ya Simba dhidi ya mwanachama Wambura. “in pari delicto potior est conditio defendentis” (panapotokea utata kwenye kesi,utata huo humnufaisha mdaiwa)
7) Itasemwa hatua zote za misingi ya haki zilizoelezwa zinapaswa kuchukuliwa si katika kumsimamisha mwanachama bali katika kesi ya kumpa adhabu. Hapana, hoja hii haina nguvu kwa sababu huku kusimamishwa tu kunasababisha mwanachama huyu apoteze haki zake nyingi ikiwemo ya kuchaguliwa, hivyo taratibu hizo zilipaswa zifuatwe kuanzia hatua hii ya kumsimamisha uanachama kwani ni hatua kubwa dhidi ya haki zake.
8) Haki ya kikatiba ya mtu kujumuika na wenzake,kuchagua na kuchaguliwa isichezewe kwa hoja za kuungaunga.
Sina urafiki wala ujamaa na Michael Wambura na zaidi ya yote hatufahamiani ila siku zote napenda kuona haki ikitendeka kwa yeyote. Yeyote kwenye uchaguzi huu na wa Yanga akichezewa faulo, nitapaaza sauti kama mwaka ule alivyochezewa faulo Kifukwe wa Yanga, nilivyopaaza sauti kwenye gazeti la Bingwa.
Narudia kueleza niliyoeleza siku kadhaa nyuma, Mambo ya Wambura sasa yametosha, mwacheni awe huru, ajisikie kuwa sehemu ya Simba na sehemu ya Watanzania.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here