Home Makala COSTA RICA WANA JIPYA GANI MWAKA HUU…

COSTA RICA WANA JIPYA GANI MWAKA HUU…

948
0
SHARE

Unapotaja neno La Sele ama Los Ticos moja kwa moja utakuwa unaizungumzia timu ya taifa ya Costa Rica, ambayo ni timu ya tatu kwa mafanikio katika ile kanda ya CONCACAF baada ya Mexico na Marekani.
Jamaa hawa wametinga kwa mara ya nne katika fainali za kombe la dunia ambazo safari hii zinafanyika nchini Brazil, wakiwa na kumbukumbu ya kufuzu kwa duru ya pili ya fanali za kombe hili mnamo mwaka 1990, pale fainali hizi zilipofanyika nchini Italia.
Moja kati ya vizazi vya kukumbukwa kwenye taifa hili, ni vile vya miaka ya arobaini, pale kikosi cha wanandinga wafupi waliokuwa na vipaji, wakichaguliwa kwa kikosi cha timu ya taifa wakipachikwa jina la utani, “The Gold Shorties”.
Kwenye miaka ya hamisini na sitini, walikuwa ni timu ya pili yenye nguvu, kwenye kanda ya CONCACAF nyuma ya Mexico, wakishika nafasi ya pili kwenye michuano ya kufuzu ya fainali hizi, katika miaka ya 1958, 1962 na 1966 na nyota bora waliojulikana kama Ruben Jimenez, Errol Daniels, Leonel Hernandez na Edgar Marin.
Kwenye historia ya kabumbu la nchi hiyo, kati ya wanandinga ambao wanaonekana kuwa na jina kubwa, ni staa wake, na mshambuliaji hatari aitwae Rolando Fonseca ambae kwenye kikosi cha timu ya taifa, amekwishasalimiana na nyavu mara arobaini na saba.
Costa Rica wamekwishashiriki mara mbili mfululizo kwenye michuano ya Olimpiki ya majira ya joto, ile iliyofanyika jijini Moscow nchini Russia mnamo mwaka 1980 na ile iliyofanyika jijini Los Angeles nchini Marekani, mnamo mwaka 1984.
Ukitaja Costa Rica, basi moja kwa moja huwezi kuacha kukumbuka majina kadhaa makubwa yaliyoiweka nchi hiyo kwenye medani ya kimataifa katika soka la kulipwa, kama Leonidas Flores, Evaristo Coronado, Juan Arnoldo Cayasso, Paul Wanchope , Rolando Fonseca, Hernan Medford,na wengine…
Baada ya kushiriki katika fainali za mwaka 1990 kule nchini Italia, na kufuzu kwa duru ya pili, na baadae kwenye fainali za mwaka 2002 kule Korea ya kusini na Japan, na 2006 nchini Ujerumani, Costa Rica hawakupata nafasi ya kushiriki kwa fainali za mwaka 201 nchini Afrika ya kusini, sasa wanarejea kwa fainali hizi za mwaka huu, kule Brazil.
Wacosta Rica safari hii walifuzu huku wakiwa wameshika nafasi ya pili ya kundi lao kwa kujikusanyia jumla ya pointi kumi na nane, nne pungufu ya waliokuwa vinara wa kanda yake ya CONCACAF Marekani, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Honduras na ya nne Mexico, wote wakifuzu.
Kwa mujibu wa utaratibu wa kuwania kufuzu kwa timu za kanda hiyo ni kwamba, timu tatu za juu toka CONCACAF zinafuzu moja kwa moja kwa fainali za kombe la dunia, na yule anaeshika nafasi ya nne, anakutana na yule aliyeshika nafasi ya tano toka CONMEBOL.
Pamoja na kushindwa kufuzu kwa fainali za mwaka 2010 kule nchini Afrika ya kusini, bado kikosi cha vijana chipukizi walio na vipaji, akina Bryan Ruiz, Keylor Navas, Cristian Bolaños, Randall Azofeifa, Michael Barrantes na kipaji cha kijana mdogo zaidi Joel Campbell, viliiweka kwenye ramani Costa Rica.
Rónald González alikuwa na vijana hawa kama kocha wa muda, kisha akamuachia kijiti Ricaldo la Volpe, mnamo September 2010, ambae alikaa kwa miezi kumi tu, na ndipo kocha wa sasa raia wa Colombia Jorge Luis Pinto, akatwaa mikoba, na sasa anaipelekea timu Brazil.
Mnamo December 2013, pale mamlaka kuu za soka la dunia zilipopanga ratiba na makundi kwa ajili ya fainali za Brazil za mwaka huu, Costa Rica ikajikuta ikiangukia kundi la D, lililo na timu ngumu za Italia, England na Uruguay, wote mabingwa wa zamani wa dunia…
Kuchomoza kwa Costa Rica kwenye kundi hili kuelekea duru ya kumi na sita bora, ama kutochomoza kwenda huko, sote tunasubiri kuona itakavyokuwa..

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here