Home Makala UCHAGUZI SIMBA: HAYA YA AVEVA, KABURU NA ZACHARIA HANS POPPE SIJAELEWA HATA...

UCHAGUZI SIMBA: HAYA YA AVEVA, KABURU NA ZACHARIA HANS POPPE SIJAELEWA HATA KIDOGO

1086
0
SHARE

hans-poppeZacharia Hans Poppe amesema wanachama wasipomchagua Aveva na Kaburu anaacha kupoteza muda na fedha zake

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976
WAKATI Wekundu wa Msimbazi Simba sc wakiwa mbioni kufanya uchaguzi wa viongozi juni 29 mwaka huu, kumekuwa na mambo ya hapa na pale. Kwasasa kamati ya uchaguzi inasikiliza mapingamizi yaliyowekwa kwa wagombea wa nafasi tofauti.
Simba iliyododa kwa misimu miwili sasa, mwishoni mwa mwezi ujao inatarajia kumpata rais mpya, makamu wa rais na wajumbe wa kamati ya utendaji kwa mujibu wa katiba yao mpya.
Kitu kinachovutia zaidi katika uchaguzi huo ni aina ya wagombea walioomba nafasi za kuiongoza Simba katika kipindi cha miaka minne ijayo. Wengi wao walishawahi kuwa viongozi katika uongozi unaomaliza muda wake na wengine miaka ya nyuma.
Nafasi zinazovuta hisia kubwa ni Urais na makamu wa Rais. Hapa kuna upinzani mkubwa ulioanza kuonekana tangu zoezi la kuchukua na kurudisha fomu lilipoanza.
Japokuwa kampeni za uchaguzi hazijaanza kwa mujibu wa ratiba, baadhi ya wagombea walimwaga sera zao siku ya kuchukua na kurejesha fomu na kuibua minong`ono miongoni mwa wanachama wa Simba.
Baadhi ya wanachama wa Simba wanaeleza wazi kuwa kuna baadhi ya wagombea walipiga kampeni kabla ya muda na kumtaka mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa klabu hiyo, Wakili na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuyaengua majina ya wagombea hao.
Ndumbaro amekuwa akikaririwa kuwa kama mgombea anavunja kanuni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kupiga kampeni kabla ya muda basi sheria itafuata mkondo wake. Kama amepata ushahidi wa matukio hayo, basi tusubiri kusikia atalipukaje baada ya mapingamizi kusikilizwa.
Michael Richard Wambura na Evance Aveva ni wagombea wawili kati ya watatu wa nafasi ya Urais. Watu hawa wawili wanavuma kama wako peke yao. Inawezekana umaarufu wao na ushawishi mkubwa walionao ndio sababu ya kuteka Msimbazi.

vevaAtapita? : Evans Aveva alifunika mitaa ya Msimbazi wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fome

Vita ya urais inaonekana kuwa baina yao, ingawa Wambura alishawekewa pingamizi. Aveva yuko mikono salama. Wambura anasubiri hukumu yake siku chache zijazo baada ya pingamizi juu yake kusikilizwa.
Nafasi ya umakamu wa rais wapo wagombea wengi, lakini Jamhuri Musa Kiwhelo `Julio` na Geofrey Nyange Kaburu wamekuwa kivutio. Hawa wanaonekana kuchuana vikali hata kabla ya mambo kufikia patamu.
Wengi tulimsikia Julio akisema mambo mengi yaliyomsukuma kugombea na akafika mbali kwa kuwawekea pingamizi viongozi wote waliokuwepo katika uongozi unaomaliza muda wake chini ya mwenyekiti Ismail Aden Rage na wameomba tena nafasi za uongozi.
Tuyaweke pembeni hayo kwanza. Makala hii inajaribu kuakisi maneno ya Kaptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Poppe ni mwanasimba wa siku nyingi. Anaipenda Simba kutoka moyoni. Ameisaidia Simba kwa kila namna. Ametumia kiasi kikubwa cha fedha zake kuisaidia Simba. Ametoa fedha zake sana kuwalipa mishahara wachezaji na kusajili wachezaji. Ni kipenzi cha wanasimba wengi kwasababu amekuwa na ushawishi mkubwa mno katika klabu. Ni mtu wa kutuliza shari za ukata katika klabu hii kubwa nchini.
Ni moja ya watu wanaounda kundi la Marafiki wa Simba `Friends of Simba`. Hili ni kundi ambalo kwasasa limepunguza kasi yake kutokana na kushindwa kuelewana na Rage. Wamekaa pembeni kidogo, lakini baadhi yao wanaendelea kuipenda Simba kama kawaida akiwemo yeye.
Poppe kwasasa ndiye mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba. Mwishoni mwa wiki aliongea na matandao huu na kusema tayari ameshamaliza mazungumzo na wachezaji wawili wa kimataifa, mmoja kutoka Kenya na mwingine kutoka Uganda.
Poppe alisema kimsingi kila kitu kipo sawa, lakini hajawapa mikataba kwasababu anasubiri wapatikane viongozi wapya. Pia alisema wamepata wachezaji wengine 12 wa Kitanzania na kila kitu kipo sawa. Akasema katika kikosi cha msimu uliopita wamebakiza wachezaji 13 tu.
Wakati Poppe akisubiri viongozi wapya wapatikane ili aendelee kugawa mikataba kwa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu wa 2014/2015, akaibua hoja waziwazi juu ya nani awe rais na makamu wa rais wa Simba sc.

Geoffrey-Nyange-KaburuGeofrey Nyange Kaburu amechaguliwa na Zacharia Hans Poppe

Poppe alionesha mapenzi ya wazi kwa Aveva katika nafasi ya urais na Kaburu nafasi ya umakamu wa rais.
Aliweka wazi msimamo wake kuwa kama wanachama wa Simba hawatawachagua Aveva na Kaburu katika nafasi hizo mbili anabwaga manyanga katika nafasi yake ya mwenyekiti wa kamati ya usajili na ataacha kutoa fedha zake.
Mwanajeshi huyo wa zamani anawafagilia wawili hao kwa madai ya kupata mafanikio wakati wa uongozi wao. Anasema Kaburu alifanya jitihada kubwa ya kuijenga Simba B iliyozalisha akina Ramadhan Singano `Messi`, Harun Chanongo, Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo.
Kwa Aveva anampa kura yake kwasababu aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili miaka ya 2000 na katika kipindi chake Simba ilikuwa kali mno na haijawahi kutokea tena. Aveva ndiye aliyewaibua akina Juma Kaseja, Suleiman Matola, Boniface Pawasa, Ulimboka Mwakingwe, Emannuel Gabriel Mwakyusa, na wengineo.
Kama anatumia ukali wa Simba wa miaka ile ya 2000, 2002,2003 kama mafanikio ya Aveva, basi hilo halina upinzani. Ilikuwa timu bora sana na haijawahi kutokea tena.
Poppe anasema waziwazi kuwa Richard Wambura hakuifanyia Simba lolote wakati wa uongozi wake, lakini Kwa Julio ndio kabisa. Anasema hajafanya lolote kwasababu yeye alikuwa kocha na alikuwa analipwa mshahara.
Hoja hapa sio Zacharia Hans Poppe kuwa na mapenzi kwa Aveva na Kaburu. Hoja ya kujiuliza ni kwanini anawaunga mkono na kuona timu ya uongozi chini ya hawa wawili italeta maendeleo katika klabu ya Simba.
Pia lazima ujiulize na kupata majibu, kwanini Poppe anatamba kuwa wanachama wasipowachagua Aveva na Kaburu atabwaga manyanga?.
Nadhani kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba amechoka kupoteza muda wake na fedha zake katika uongozi unaomaliza muda wake bila mafanikio yake.
Poppe anatumia fedha zake nyingi kuisaidia Simba. Nadhani amechoka kumwaga pesa bila mafanikio. Ndio maana anaona kuna haja ya kumchagulia viongozi watakaoendana sawa kimawazo na anawapenda Kaburu na Aveva.
Wote wawili, Poppe alifanya nao kazi kwa nyakati tofauti, yawezekana walikuwa wanaelewana sana.
Aveva ni moja ya watu wa `Friends of Simba`kama ilivyo kwa Poppe. Kwa pamoja walifanya kazi miaka ya nyuma na kuisaidia Simba sc kifedha.
Wengi walisema Aveva anagombea urais na nyuma yake kuna watu wengi wa Friends of Simba akiwemo Kassim Dewji na Poppe. Kwa maneno ya mwanajeshi huyu wa zamani unaweza kuanza kuamini kuwa Aveva anaungwa na watu wengi wenye ushawishi ndani ya Simba.
Hata matarumbeta yaliyomsindikiza siku ya kuchukua na kurudisha fomu, unaweza kusadiki kuwa jamaa huyu ana nguvu sana kuelekea uchaguzi huo wa juni 29.
Sipingani na mtazamo wa Poppe juu ya viongozi anaowataka yeye kwasababu ana haki kikatiba akiwa mwanachama wa Simba. Ni mtazamo wake na maono yake, lakini wanachama ndio watakaochagua watu wanaowahitaji.
Lakini kama wanachama wanamuamini Poppe na hawataki aondoke katika nafasi yake ya mwenyekiti wa kamati ya usajili , basi kwa lugha nyepesi hawatachagua wao ila wataenda kukamilisha zoezi kwa kubariki kura ya Zacharia Hans Poppe kwa Aveva na Kaburu.
Kuondoka kwa Poppe kunaweza kuwa tatizo kubwa kwa Simba kifedha. Kila siku tunaandika kuwa ifike wakati Simba na Yanga zijitegemee kifedha. Wengine kutokana na mapenzi ya klabu zao wanatubatiza majina ya ajabu.
Wengine wanatuita makanjanja, mamluki , wababaishaji na mengineyo. Lakini kamwe haifuti ukweli kuwa Yanga na Simba ni hovyo katika mipango ya kujiendesha bila kutegemea mamilionea wanaamua kila kitu.
Timu zenye wanachama kila kona ya nchi, rasilimali za kutosha, mpaka leo hii zinategemea fedha kutoka mifukoni mwa watu wachache, hii ni aibu upende usipende!.
Angalia hata Yanga, kuna watu kama Abdallah Bin Kleib, Yusuf Manji, Clement Sanga, David Mosha, Seif Magari na wengineo. Hawa jamaa wakisusa hata sekundi hii unaposoma makala haya, basi hali itakuwa tete mno.
Kama klabu inaendeshwa kwa fedha zao. Maan yake hawa watu wana ushawishi mkubwa mno na hawawezi kupingwa kirahisi.
Leo hii Manji akisema hapapa! Ni hapana. Si kwasababu yeye ni mwenyekiti. Ni ushawishi mkubwa wa kifedha alionao katika klabu ya Yanga.
Watu hawa wanatumia fedha nyingi sana kuzisaidia klabu hizi mbili. Na wenyewe wana mapenzi yao. Wanataka viongozi wanaowapenda ili watoe fedha kwa faida.
Poppe yeye amechoka na ubabaishaji, sasa ameamua kuwachagulia wanachama viongozi. Yuko sahihi kwasababu anapoteza pesa zake.
Lakini kimsingi, hapa sio demokrasia. Maana yake Poppe kawashawishi wote wanamuamini yeye. Watu wanaompenda hawana ubavu wa kukimbia machaguo ya mwanaumwe huyu katika klabu ya Simba.
Kama wanafikiri ni utani basi wasiwachague waone. Hakika maneno ya Poppe yamenifikisha mbali sana na kuona ipo haja ya klabu hizi kujiuliza upya.
Kama ulimsikia Wambura alisema anataka kuiondoa Simba kutoka mikononi mwa watu wachache ili ijitegemee kiuchumi. Maana yake Wambura ana maanisha watu kama Zacharia Hans Poppe wasiwe tegemeo kwa asilimia 100.
Binafsi mawazo ya Wambura nayaunga mkono, japokuwa yapo mdomoni mwake na sijui kama anaweza kutekeleza. Sisemi ndiye achaguliwe. Lakini ukweli unabaki kuwa mawazo yake ni bora hasa kwa wakati huu Simba inapohitaji kupiga hatua.
Mara nyingi unapotaka kufanya mabadiliko lazima ukubali athari. Kama Wanachama wanataka kuibadili Simba, wakubali kuwa wavumilivu. Lakini kama wanataka mabadiliko ya haraka, basi watazingatia maamuzi ya watu kama Poppe.
Yeye ana jeuri ya fedha. Wakimpuuza sijui nani atawalipa mishahara na posho wachezaji wanapotaka kwenda Zanzibar kuweka kambi kujiandaa na mechi ya mtani wake wa jadi, Yanga SC. Daah! Inatia uchungu sana kuona mtu mmoja ana maamuzi makubwa kiasi hiki. Simpingi Poppe, ni mapendekezo yake. Lakini hili la kuondoka madarakani kama Kaburu na Aveva hawatachaguliwa, hapo sasa kuna tatizo.
Narudia tena! Simpingi Poppe hata kidogo kwasababu kweli anapoteza pesa zake. Lakini kuna haja gani kwa klabu kubwa ya Simba kuwategemea watu kama hawa?. Kwanini wasiwe katika nafasi ya wadau wa Simba wanaochangia kwa hiari?. Hata wasipochangia mambo yawe yanakwenda tu.
Nani atakuwa rais na makamu wa rais wa Simba?. Juni 29, 2014, jibu litapatikana. Poppe yeye amewachagua Aveva na Kaburu. Wanachama wanasemaje?, tusubiri siku ya uchaguzi.
Nawatakia jumatatu njema wana Simba wote na wadau wa soka.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here